ADV

ADV

ADVERTISEMENT CORNER

HUDUMA YA KUKATA TICKET ZA NDEGE ONLINE


SOMA HABARI

SOMA HABARI

Wednesday, November 21, 2012

Askari 10 JWTZ Mbaroni Kwa Mauaji


 Kamanda wa Polisi mkoani wa Mbeya, Diwani Athuman 
JESHI la Polisi mkoani Mbeya linawashikilia  watu 10 wanaodhaniwa kuwa ni askari wa Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ) kikosi cha 44 KJ  Kambi ya mji mdogo wa Mbalizi  kwa tuhuma za mauaji ya mkazi wa mji huo, Petro Sanga (25).

Askari hao wanadaiwa kumuua Sanga kwa kumchoma kisu shingoni na mdomoni, kisha kuwajeruhi watu wengine sita kwenye Baa iitwayo Power Night, ambako walikwenda kwa lengo la kulipiza kisasi cha kupigwa kwa askari mwenzao, Geodfery Matete (30).

Hata hivyo, Matete anadaiwa kwamba alikuwa amepigwa na walinzi wa kilabu cha pombe cha DDC kilichopo katika mji huo wa Mbalizi, Novemba 18 mwaka huu saa 3 usiku.

Mauaji hayo yamekuja siku moja baada ya Mahakama Kuu Kanda ya Dar  es Salaam  kuwahukumu adhabu ya kunyongwa hadi kufa askari  watatu wa JWTZ na JKT, baada ya kupatikana  na hatia ya kumuua, Swetu Fundikira.

Hata hivyo, askari hao waliohukumiwa kunyongwa, jana waliwasilisha taarifa ya kusudio la kukata rufaa katika  Mahakama Kuu ya Tanzania.

Kamanda wa Polisi mkoani wa Mbeya, Diwani Athuman alithibitisha mauaji hayo mapya yaliyotokea katika Mji wa Mbalizi na kwamba marehemu Sanga alikutwa na mauti akiwa anakunywa pombe kwenye baa iitwayo Power Night.

“Marehemu na wenzake walivamiwa na askari hao na kuanza kuwashambulia. Askari hao waliwashambulia wananchi waliokuwapo kwenye baa hiyo na Sanga alifariki dunia baada kupigwa sehemu mbalimbali za mwili wake kwa mateke, mikanda, marungu, sime na mapanga,” alisema Kamanda Athuman na kuongeza:

“Baada ya kumpiga walimchoma  kisu mdomoni. Katika jitihada zake za kujiokoa, marehemu alikimbilia katika baa nyingine ya  Vavenemwe.”

Kwa mujibu wa Kamanda Athuman, baada ya marehemu kufika katika baa hiyo alipoteza fahamu na wasamaria wema walimbeba na kumkimbiza katika Hospitali Teule ya Ifisi iliyopo katika mji huo mdogo.

“Alifariki wakati akipatiwa matibabu na hiyo ilitokana na kuvuja damu nyingi,” alisema.

 Chanzo cha vurugu

Kamanda Athuman alisema chanzo  cha vurugu hizo, ni askari wa JWTZ, Matete (30)  kushambuliwa na walinzi wa kilabu cha pombe za kienyeji  kilichojulikana kwa jina la DDC Novemba 17 mwaka huu.

Alisema kuwa  kutokana na tukio hilo, Polisi wanawashikilia  walinzi wanne kwa mahojiano zaidi ambao ni Frank Mtasimwa (25), Mure Julius (26), Omari Charles (28) na Regnad Mwampete, wote wakazi wa Kijiji cha Izumbwe Wilaya ya Mbeya.

Kamanda Athuman alisema majina ya askari waliokamatwa kwa tuhuma hizo yatatajwa baadaye kwani bado uchunguzi unaendelea huku akivitaka vyombo vya dola kuacha kujichukulia sheria mkononi kwa kuwa hali hiyo inaweza kusababisha uvunjifu wa amani.

“Uchunguzi wa tukio hili ukikamilika waliokamatwa watafikishwa mahakamani” alisema.

Msemaji wa JWTZ, Kanali Kapambala Mgawe alisema kuwa hana taarifa za wanajeshi hao kufanya mauaji huku akisisitiza kuwa kama wanashikiliwa na Jeshi la Polisi ni wazi kuwa watakuwa wanahusika na tukio hilo.

“Bado sijapata taarifa rasmi kuhusu tukio hilo kwa kuwa hivi sasa sipo katika eneo la kazi, polisi ndio wanaweza kusema lolote na kama kweli wanawashikilia basi watakuwa wamehusika,” alisema Mgawe.

Walioua na rufaa
Wakati huohuo, askari  watatu wa JWTZ, waliohukumiwa kunyongwa hadi kufa baada ya kupatikana  na hatia ya kumuua Swetu Fundikira, jana wamewasilisha taarifa ya kusudio la kukata rufaa katika  Mahakama Kuu ya Tanzania.

Wakili wa askari hao, Mluge Karoli alisema wamewasilisha kusudio hilo la taarifa ya kukata rufaa kwa sababu hawajaridhishwa na uamuzi uliotolewa na Jaji Zainabu Muruke wa   kuwatia hatiani wanajeshi hao kwa kosa la kumuua kwa makusudi Fundikira, kinyume cha kifungu cha 196 cha Kanuni za Adhabu.

Karoli akitoa sababu za kuwasilisha kusudio hilo la kukata rufaa alidai kuwa kesi yoyote ya ugomvi  haiwezi  kuwa na kusudio la kutaka kuua na kwamba hakuna shahidi aliyefika mahakamani hapo na kueleza kuwa wateja wake ndio wamemuua Swetu Fundikira.

Pia alienda mbali zaidi na kudai kuwa wateja wake ambao ni MT 1900 Sajini Roda Robert (42), MT 85067 Koplo Mohamed Rashid  wa JKT Mbweni na MT 75854 Koplo Ally Ngumbe (37) wa kikosi cha JWTZ Kunduchi hawakuwa na wajibu wa kuthibitisha mauaji hayo.

“Waliomuua marehemu Swetu siyo wateja wangu na ninaamini  Mahakama ya Rufani itaangalia upya ushahidi na kutenda haki,” alidai Karoli.

Aliongeza kudai kuwa aliyepambana na wateja wake ni Swetu Fundikira na uchunguzi wa daktari unaonyesha jina la Swetu Ramadhani Fundikira hivyo ni watu wawili tofauti na kwamba hakuna hata shahidi mmoja  aliyesema aliwahi kuona mwili wa marehemu ama kuhudhuria kwenye msiba.

Askari hao kwa pamoja wanadaiwa kuwa walimpiga Fundikira, Januari 23 mwaka huu  saa 7:30 usiku wilayani Kinondoni jijini Dar es Salaam na baadaye kufariki dunia usiku huohuo wa kuamkia Januari 24, mwaka 2010, katika Hospitali ya Taifa Muhimbili.

Hukumu hiyo iliyotolewa juzi na Jaji Mruke, ilifufua upya msiba wa Swetu, baada ya ndugu zake kuangua vilio, huku chumba cha Mahakama kikigeuka kwa muda kuwa sehemu ya msiba.

Sambamba na vilio hivyo, ndugu wawili wa marehemu Swetu walianguka chini na kuzirai kwa muda, kabla ya kupewa huduma ya kwanza na kurejea katika hali ya kawaida.

Akisoma hukumu hiyo, Jaji Muruke alisema ingawa hakuna ushahidi wa moja kwa moja kuwa washtakiwa hao ndio waliomuua Fundikira, ushahidi uliotolewa na  upande wa mashtaka (Jamhuri) ulikuwa ni ushahidi wa mazingira, kwamba Jamhuri imeweza kuthibitisha mashtaka hayo.

Alisema kuwa anakubaliana na mtiririko wa ushahidi wa upande wa mashtaka kama ulivyoelezwa na mashahidi wake sita akiwamo daktari aliyeufanyia uchunguzi mwili wa marehemu, askari polisi wawili ambao washtakiwa katika utetezi wao walishindwa kuuvunja.

“Sheria iko wazi ukiondoka na mtu au ukionekana naye kwa mara ya mwisho na baadaye mtu huyo akapatikana na madhara, wewe ndio unawajibika kutoa maelezo ya kina kuhusu yaliyompata mtu huyo” alisema Jaji Muruke na kuongeza;

“Kisheria ukitoa maelezo ambayo hayajakidhi haja na yana utata ni faida kwa upande wa mashtaka ambao hutegemea ushahidi wa mazingira. Maelezo ya kina hayajatolewa na washtakiwa wote.”

Aliendelea,  “Ushahidi wa Jamhuri japokuwa ni wa mazingira, umejengwa thabiti na upande wa utetezi haukuweza kujenga matundu, ama kuuvunja mnyororo huo,  kidole kinawaelekea wao.”

Jaji Muruke alisisitiza kuwa katika kesi hiyo licha ya kuwa kuna ushahidi wa kimazingira, upande wa mashtaka umeweza kuthibitisha mashtaka bila kuacha shaka.

“Hivyo kosa wanaloshtakiwa nalo limethibitishwa na Mahakama imewaona washtakiwa kuwa wana hatia ya kumuua Swetu Abdallah Fundikira” alisema Jaji Muruke.

No comments:

Post a Comment

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...