Baadhi ya wananchi kwenye mkutano huo
Kundi la maigizo likifanya vitu vyake
Mkurugenzi Mtendaji wa Mtandao wa Jinsia Tanzania (TGNP), Bi. Usu Mallya akijumuika kucheza ngoma
Na Mwandishi wa Thehabari.com Morogoro
MKURUGENZI Mtendaji wa Mtandao wa Jinsia Tanzania
(TGNP), Usu Mallya amewataka wananchi kushiriki kikamilifu katika uundwaji wa
Katiba mpya ili itakapo kamilika sera na sheria za nchi ziendane na wananchi
wake, jambo ambalo litasaidia kutatua migogoro anuai.
Mkurugenzi huyo aliyasema hayo jana eneo la Mkambarani mje
kidogo ya Mji wa Morogoro ambapo linafanyika tamasha la Jinsia katika ngazi ya
wilaya lililoandaliwa na TGNP, kuchochea juhudi za wananchi hasa waliopo
pembezoni kushiriki katika mchakato wa maendeleo yao.
Akizungumza katika mkutano huo unaowashirikisha wanavijiji
kutoka baadhi ya vijiji vya Mkoa wa Morogoro na baadhi ya mikoa ambao ni
wanaharakati wa ngazi za jamii, alisema ushiriki wa wananchi ipasavyo katika
mchakato huo itasaidia mabadiliko ya mfumo wa uandaaji wa sera na sheria ili
zisiendelee kulalamikiwa na wananchi.
“Mfumo uliopo sasa yawezekana kabisa ukawa na upungufu, ndio
maana hata kwa sasa baadhi ya maeneo yanapata huduma za kijamii huku maeneo
mengine yakilegalega kihuduma,” alisema.
Alitolea mfano eneo la Mkambarani wananchi wanalalamikia
migogoro ya ardhi hali hiyo inachangiwa na mfumo katika mgawanyiko wa
rasilimali ikiwemo ardhi, ambapo baadhi ya makundi yamekuwa yakisahaulika huku
wajanja wakineemeka na mifumo hiyo.
Alisema wananchi wanapaswa kushirikishwa kwa karibu katika uandaaji
wa sera na sheria na pia kushirikishwa kwenye mipango ya maendeleo ili kuondoa
mkanganyiko ambao hujitokeza hapo baadaye. “Wananchi lazima tushirikishwe
katika mipango ya maendeleo…tukumbuke kwamba hakuna sera na sheria inayonihusu
mimi bila mimi kushirikishwa,” alisema Mallya.
Aidha aliwataka wanawake na wapenda mabadiliko kushiriki katika
vuguvugu la kupambana na mfumo dume na kandamizi ambao kwa kiasi kikubwa
unawaathiri akina mama. “Tukubali kuwa huu ni mchakato wa mabadiliko, tukatae
uonevu na kupambana na mifumo yote kandamizi kwa kutumia umoja wetu pamoja na
ushirikiano…umefika wakati wa kushirikiana katika masuala ya maendeleo,
tusiishie kwenye harusi na misiba tu,” aliongeza.
Tamasha la jinsia ngazi ya wilaya linalofanyika nje kidogo
ya mji wa morogoro linatarajiwa kumalizika leo jioni ambapo washiriki kwa
pamoja watatoka na maadhimio ambayo yatafanyiwa kazi kulingana na maitaji.
No comments:
Post a Comment