Waziri wa Ujenzi Dkt. John Magufuli.
Wizara ya Ujenzi na Wakala wa Majengo Tanzania (TBA) imewafukuza kazi na kusitisha mikataba ya Wafanyakazi Waandamizi saba wa Wizara na Wakala wa Majengo Tanzania (TBA) kwa tuhuma za ubadhilifu na utendaji kazi mbovu. Hatua hiyo ni sehemu ya dhamira ya Wizara ya Ujenzi ya kusafisha Wakala zake na kuongeza ufanisi.
Katika nyakati tofauti Mheshimiwa Waziri wa Ujenzi amekuwa akipokea tuhuma za vitendo vya ubadhilifu miongoni mwa watendaji waandamizi katika Wakala zinazotoa huduma chini ya wizara hii. Kufuatia tuhuma hizo Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) alifanya ukaguzi maalum katika ofisi za TBA Mkoa wa Dar es salaam na Katibu Mkuu wa wizara Balozi Herbert E. Mrango na Mtendaji Mkuu wa TBA Arch. Elius Mwakalinga waliunda Kamati za kupitia taarifa za CAG na taarifa nyingine. Kamati hizo zimeweza kubaini kuwepo kwa ukiukwaji mkubwa wa taratibu za fedha, manunuzi na uendeshaji.
Maafisa waliofukuzwa kazi ni pamoja na Bw. Charles Gabriel Lyatuu ambaye alikuwa ni Meneja wa TBA mkoa wa Dar es Salaam; Bw. Ladislaus I. Kapongo aliyekuwa Mhasibu Msaidizi (TBA mkoa wa Dar es Salaam) na Bi. Agness F. Chambo aliyekuwa Mhasibu Msaidizi (TBA mkoa wa Dar es Salaam). Aidha, kwa Mkurugenzi wa Biashara na Fedha Bibi Yona Orida na Injinia Charles Makungu ambaye alikuwa ni Mkurugenzi wa Miliki wameondolewa katika nafasi za uongozi walizokuwa nazo TBA.
Hatua zaidi zilizochukukuliwa ni kuwashusha vyeo Meneja wa Mkoa wa Pwani Bibi Esteria M. Nyamhanga na Bw. Samwel C. Samike ambaye alikuwa ni Meneja wa TBA mkoa wa Mbeya.