SERIKALI
imeamua kupunguza kwa kiasi kikubwa bei ya kuunganisha umeme majumbani
na kufikia sh. 27,000/ kwa wanavijiji wanaoishi kwenye maeneo ambayo
bomba la gesi linapita.
Hatua
hiyo imetangazwa jana (Jumapili, Januari 26, 2014), na Waziri wa Nishati
na Madini, Prof. Sospeter Muhongo wakati akizungumza na wanakijiji wa
Mangaka wilayani Nanyumbu, mkoani Mtwara kabla ya kumkaribisha Waziri
Mkuu, Mizengo Pinda azindue mradi wa umeme kwenye wilaya hiyo.
“Jana
Waziri Mkuu aliagiza tutafute namna ya kuwasaidia wananchi wanaoishi
jirani na njia ya bomba la gesi. Nami nilikaa na wasaidizi wangu jana
usiku na kufanya hesabu na tukaamua tuweke kiwango hicho kwa ajili ya
wakazi hao,” alisema.
Alisema
katika mikoa mikoa mingine gharama za kuunganisha umeme ni sh. 177,000/-
lakini kwa mikoa ya Lindi na Mtwara gharama hizo zilishushwa na kufikia
sh.99,000/-. “Lakini sasa hawa wenzetu tumewapa upendeleo zaidi na
tumewapunguzia gharama hizo hadi sh. 27,000/-,” alisema huku
akishangiliwa.
Gharama
hizo ni maalum kwa ajili ya wakazi waishio jirani na bomba hilo
linaloanzia Mtwara hadi Dar es Salaam kupitia mikoa ya Lindi na Pwani.
Akizungumza
na mamia ya wakazi wa Mangaka waliofika kushuhudia uzinduzi huo, Waziri
Mkuu alisema uzinduzi wa mradi huo wa umeme ni utekelezaji wa azma ya
Serikali ya kuhakikisha kila wilaya inapata umeme.
“Mpango
wa kupeleka umeme nchi nzima ni wa miaka mitatu na katika sekta ya
Nishati chini ya Mpango wa Matokeo Makubwa ya Haraka (BRN), tumeazimia
kwenda kwa awamu ili tuwafikie wananchi wengi zaidi kutoka asilimia 24
ya sasa hadi kufikia asilimia 30 ya watumiaji wa umeme,” alisema Waziri
Mkuu.
Akitoa
taarifa juu ya mradi huo wa umeme wilayani Nanyumbu, Meneja Mwandamizi
wa TANESCO, Kanda ya Dar es Salaam na Pwani inayojumuisha mikoa ya Lindi
na Mtwara, Eng. Mahende Mugaya alisema mradi huo umegharimu sh. bilioni
5.6/- na unatarajiwa kukamilika Aprili, mwaka huu.
Alisema
kuzinduliwa kwa mradi huo kunafanya wilaya zote za mkoa wa Mtwara ziwe
zimepata umeme wa kuanzia na kwamba kazi itaendelea kupitia Wakala wa
Umeme Vijijini (REA) ili kuongeza idadi ya watumiaji wa umeme kwenye
mkoa huo.
“Chini ya
mfuko wa REA tumetenga sh. bilioni 7.6 ili zitumike kusambaza umeme
katika wilaya zote za mkoa wa Mtwara ambao sasa hivi watumiaji wa umeme
wamefikia 15,675 sawa na asilimia nne ya wakazi wote wa mkoa huu.”
Alisema
katika mwaka 2012-2013 walipata wateja 2,609 tofauti na idadi ya zamani
ya wateja 1,300 ambayo ilikuwa imezoeleka. Alisema hivi sasa wamepokea
maombi kutoka kwa wateja 2,588 ambao tayari wamekwishalipia gharama za
kuunganishiwa umeme.
Chini ya
mradi wa umeme kupitia REA, jumla ya vijiji 54 katika wilaya za
Tandahimba, Masasi na Newala vitanufaika na mradi huo ulioanza
kutekelezwa Desemba 2013 na unatarajiwa kukamilika ifikapo Desemba
2015.Na Issa michuzi matukio
No comments:
Post a Comment