KWA UFUPI
Alikuwa akijaribu kumsaidia mwenzake aliyekuwa amevamiwa na majambazi eneo la hoteli.
Zanzibar.Askari wa Kikosi cha FFU, Mohamed Mjombo (Namba E 5607) ameuawa kwa kupigwa risas, huku mwingine akijeruhiwa baada ya majambazi kuvamia hoteli ya kitalii ya Pongwe Bay iliyo Pongwe mkoani Kusini Unguja.
Akizungumza na gazeti hili jana, Kamishna wa Polisi Zanzibar, Hamdan Omar Makame alisema tukio hilo lilitokea juzi saa 3:00 usiku wakati wageni wakiwa wamepumzika na askari hao wa FFU kutoka Kituo cha Polisi Machui wakiwa katika lindo kwenye hoteli hiyo.
Kamishna Hamdan alisema muda huo lilifika gari moja na baada ya kuegeshwa watu watatu waliteremka na kumvamia askari mweye Namba F 6198, Ibrahim Juma Mohamed na kujaribu kumnyang’anya silaha aina ya SMG na katika purukushani hiyo walimpiga risasi ya begani.
Alisema askari huyo anaendelea na matibabu katika Hospitali ya Mnazi Mmoja.
“Majambazi walifanikiwa kumpora bunduki aina ya SMG na kisha kumpiga risasi na kumjeruhi begani. Tuko katika msako mkubwa hivi sasa,” alisema Kamishna huyo wa Polisi Zanzibar.
Hata hivyo, alisema wakati Mjombo akisonga mbele kujaribu kumsaidia mwenzake, alifyatua risasi lakini ikakwama katika chemba na majambazi hao kufanikiwa kumpiga risasi sehemu ya ubavu na kutoroka.
Alisema askari huyo wa FFU alifariki majira ya saa 7:00 usiku katika Hospitali ya Mnazi Mmoja na kuzikwa jana huko Bambi Mkoa wa Kaskaszini Unguja. Watu wawili wanashikiliwa na polisi kuhusiana na tukio hilo na wengine wanaendelea kusakwa.
“Tayari tumepeleka kikosi cha askari maalumu kutoka Mkoa wa Mjini Magharibi na Mkoa wa Kusini Unguja, ili kuhakikisha usalama unaimarishwa katika maeneo ya ukanda wa utalii,” alieleza Kamishna Hamdan.
Daktari bingwa wa Hospitali ya Mnazi Mmoja, Msafiri Marijani ambaye ndiye aliyemfanyia uchunguzi Mjombo, alisema askari huyo alipoteza damu nyingi baada ya kupigwa risasi ubavu wa kushoto na kutokea paja la kulia na ndio maana alipoteza maisha.
“Uti wa mgongo pia ulivunjika,” alisema Dk. Marijani. “Amepoteza damu nyingi iliyokuwa ikivuja ndani ya tumbo na nje. Risasi bado haijapatikana mahali ilipo mwilini.”
Akizungumzia tukio hilo, mwenyekiti wa Jumuiya ya Uwekezaji Katika Sekta ya Utalii Zanzibar (ZAT), Abdulswamad Said alisema wakati umefika kwa SMZ kuimarisha ulinzi katika Ukanda wa Utalii kwa vikosi vya SMZ na Polisi kufanya kazi pamoja ili kulinda wawekezaji, watalii na wananchi.
Abdulswamad alisema uongozi wa ZAT uliwahi kukutana na Rais wa Zanzibar, Dk. Ali Mohamed Shein na kuomba vikosi vya SMZ viongezewe nguvu za ulinzi ili kukabiliana na matukio ya uhalifu na kusema jambo la kushangaza pamoja na Rais kutoa agizo hilo, hakujawa na utekelezaji wa wazi.
“Matukio ya watu kumwagiwa tindikali, milipuko ya mabomu na uhalifu wa kutumia silaha hayatoi sura nzuri kwa maendeleo ya utalii Zanzibar. Juhudi zaidi zinahitajika kukabiliana na vitendo hivyo hatari,” alisema mwenyekiti huyo wa ZAT.
Taarifa kutoka eneo la tukio zinaeleza kuwa majambazi hao walikuwa wamebeba silaha za kivita na kuaminika huenda walikuwa na silaha aina ya AK 47, lakini hawakufanikiwa kupora mali hotelini hapo.
CHANZO:MWANANCHI
No comments:
Post a Comment