MAMLAKA
ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) kwa kutumia mtambo maalumu uitwao
Telecommunication Traffic Monitoring System (TTMS) wamefanikiwa
kuwakamata baadhi ya watu wanaofanya udanganyifu katika mitandao ya simu
za kimataifa.Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam
jana, Meneja Mawasiliano wa TCRA, Innocent Mungy, alisema ufungaji wa
mtambo huo umeweza kutambua mawasiliano ya udanganyifu katika mitandao
ikiwa ni pamoja na namba za ulaghai za nchini zinazotumika kuruhusu au
kupitisha mawasiliano ya kimataifa kinyume na matakwa ya sheria.
Alisema
kumekuwa na makampuni na watu binafsi wanaowezesha simu zinazopigwa
kutoka nje kufika nchini bila kupitia kwenye njia rasmi, hivyo
kuikosesha serikali na makampuni ya simu mapato halisi.
"Watu
hawa hutumia internet kuruhusu simu zinazopigwa kutoka nje ya nchi na
kuzifanya zionekane kama zimetoka hapa nchini kwa kifaa kinachojulikana
kama Sim box," alisema.
Alisema
kifaa hicho kina uwezo wa kutumia laini za simu nyingi ambazo
zinatumika kuidanganya mitambo ya kampuni za ndani kutokutambua kuwa
simu zilizopigwa ni za kimataifa.
"
Mwananchi anapopigiwa simu na mtu aliyeko nje ya nchi na akaona kwenye
simu yake namba ya mtandao ya hapa nchini ajue kuwa simu hiyo
aliyopigiwa inapita kwenye mitandao isiyo rasmi, mara nyingi mitandao
hii huwa na huduma mbovu na zisizo na viwango vinavyokubalika," alisema.
Alisema
kwa kutumia mitambo hii na kwa kushirikiana na watoa huduma za simu na
vyombo vya usalama inafanya uchunguzi wa kitaalamu kila wakati ili
kubaini uwepo wa udanganyifu katika mitandao ya simu.
"
Zoezi hili ni endelevu na linahusisha ukaguzi na utambuzi wa mitambo
inayojihusisha na udanganyifu katika mitandao ya simu na endapo mtu
yeyote au kampuni itabainika kuhusika na udanganyifu huu, hatua kali za
kisheria zitachukuliwa dhidi yao," alisema.
No comments:
Post a Comment