Beki wa pembeni kutoka nchini Brazil na klabu ya Barcelona,
Dani Alves ameushangaza ulimwengu wa soka, kufuatia shukrani alizozitoa
dhidi ya mashabiki wa klabu ya Villareal waliomtupia ndizi akiwa
uwanjani usiku wa kumkia hii leo huko El Madriga.
Katika hali isiyotarajiwa Daniel Alvesa alifanya hivyo mara baada ya
mchezo kati ya Barcelona na Villareal kumalizika huku Barca wakipata
ushindi wa mabao matatu kwa mawili.
Alves, amesema kurushiwa ndizi akiwa uwanjani kwake anakichukulia
kitendo hicho ni cha kawaida na anaamini wanaofanya hivyo ni mashabiki
wenye upeo mdogo wa kufikiria ambao bado wanahitaji usaidizi wa
kubadilishwa kimawazo.
Amesema ameishi nchini Hispania kwa miaka 11 na mara kadhaa wachezaji
wenye asili ya bara la Afrika wamekua wakikutana na vitimbi kama hivyo,
ambavyo vinaashiria ubaguzi wa rangi hali ambayo amesisitiza
ameshaizoea.
Hata hivyo beki huyo mwenye umri wa miaka 30, kwa kuonyesha hajali
masuala ya ubaguzi wa rangi, alidiriki kukata kipande cha ndizi
aliyorushiwa uwanjani na kukila huku sehemu iliyo baki akiitupa
pembezoni mwa uwanja wakati akijitayarisha kupiga mpira wa kona.
"Sikufahamu ni nani alitupa ndizi ile, lakini sijali kutokana na
kuichukulia tabia hiyo kama ya kawaida ambayo siku zote imekua ikifanywa
na mashabiki wenye upeo mdogo wa kimawazo.” Amesema Alves.
"Ni Ajabu kwa mtu ambae anapenda soka kuendeleza vitendo vya ubaguzi wa
rangi ambavyo kila siku vinapigwa vita duniani kote, hivyo sikujali ndio
maana nilidiriki kukata sehemu ya ndizi na kuila kwa kuwaonyesha
wahusika waliofanya kitendo kile ndizi ni sehemu ya matunda niyapendayo”
Ameongeza Alves.
Mashabiki wa soka nchini Hispania wamekua na tabia ya kurusha ndizi
uwanjani kwa kuwalenga wachezaji wenye asili ya bara la Afrika ambao
siku zote wamekua wakifananishwa na nyani.
No comments:
Post a Comment