ADV

ADV

ADVERTISEMENT CORNER

HUDUMA YA KUKATA TICKET ZA NDEGE ONLINE


SOMA HABARI

SOMA HABARI

Thursday, May 8, 2014

DAVID KAFULILA AWAFYATUA VIGOGO WA SERIKALI YA CCM KUHUSIKA NA WIZI MKUBWA BOT.


MBUNGE wa Kigoma Kusini, David Kafulila (NCCR-Mageuzi), amefichua ufisadi mkubwa wa dola za Marekani milioni 122, sawa na shilingi bilioni 200 akidai umefanywa na vigogo sita wa serikali. Aliwataja vigogo hao kuwa ni Waziri wa Nishati na Madini, Prof. Sospiter Muhongo na Katibu Mkuu wake, Eliakim Maswi, Waziri wa Fedha Saada Mkuya, Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania, Prof. Beno Ndullu, Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Frederick Werema na Mkurugenzi Mkuu wa Tanesco, Mhandisi Felchesmi Mramba
Mbunge wa Kigoma Kusini, David Kafulila (NCCR-Mageuzi),akichangia hoja katika Bunge la Bajeti mjini Dodoma 

Akichangia hotuba ya makadirio ya mapato na matumizi ya bajeti ya ofisi ya Waziri Mkuu kwa mwaka wa fedha 2014/15, Kafulila alidai kuwa vigogo hao wamehusika na ufisadi wa fedha hizo zilizokuwa zimewekwa katika akaunti ya Baraza la Usuluhishi la Migogoro ya Kibiashara (ESCROW) katika Benki Kuu ya Tanzania (BoT).
Akaunti hiyo ilifunguliwa kutokana na mgogoro wa kibiashara kati ya IPTL na Tanesco ambapo Tanesco ilipeleka shauri hilo kulalamikia gharama kubwa wanazotozwa na IPTL. 
Akizungumza kwa kujiamini, Kafulila alisema kuwa hivi karibuni baraza hilo lilitoa uamuzi wa awali wa kutaka Tanesco kukaa pamoja na IPTL kupitia upya malipo hayo, lakini Tanesco imekataa kufanya hivyo.
“Hadi tunavyozungumza leo, Tanesco imeandika barua kukataa kukaa pamoja na IPTL. Hii ni ajabu sana, Tanesco ndiyo waliolalamika, wanaambiwa wakae wapitie upya hesabu zao, hawataki, kwanini?” alihoji Kafulila. Kwa mujibu wa Kafulila, uchunguzi alioufanya na ushahidi anao, amebaini kuwa fedha hizo zimeshachotwa katika akaunti hiyo kwa ushirika wa vigogo hao.
Mbunge huyo aliapa kuwa hatakubali fedha hizo zipotee wakati wahusika wapo na wanatamba kwa kutoa kauli za kejeli. Alisisitiza kuwa lazima sakata hilo liondoke na mtu. Akifafanua hoja hiyo mbele ya waandishi wa habari, Kafulila alisema akaunti hiyo ilifunguliwa mwaka 2004 kutokana na mgogoro kati ya Tanesco na IPTL.
Alisema kuwa fedha hizo zilihifadhiwa katika akaunti hiyo kusubiri hatma ya mgogoro huo ambao kwa sasa alisema umekuwa mkubwa zaidi baada ya Kampuni ya PAP kudai imeinunua IPTL.
PAP inadai kuinunua IPTL kutoka kwa MERCMA iliyokuwa ikimiliki asilimia 70 ya hisa na VIP iliyokuwa na umiliki wa asilimia 30. Kwa mujibu wa Kafulila, ushahidi wa cheti unaonyesha kuwa PAP imenunua asilimia 30 ya hisa za VIP, lakini haina ushahidi wa ununuzi wa hisa asilimia 70 za MERCMA.
Baraza la Usuluhishi wa Migogoro ya Wawekezaji (ISCID), lilitoa hukumu ya awali Februari 2014 na kutoa siku 90 kwamba Tanesco ikae na IPTL wapige upya mahesabu ya bei ya umeme kwani inatoza zaidi.
“Muda huo umeisha na Tanesco wamekataa kufanya mahesabu upya na IPTL kwa kuwa tangu Novemba 2013 fedha imeshaliwa kwa kupewa raia mmoja wa kigeni mwenye asili ya Singasinga wa Kampuni ya PAP kwa ushirika wa vigogo wa juu, kila mmoja kwa namna yake,” alisema. Kafulila alisisitiza kuwa suala hilo liko wazi kwa vile limethibitishwa na Gavana Ndullu alipoitwa kwenye Kamati ya Bunge. Alisema kuwa alipewa maelekezo ya kushinikizwa kutoa fedha hizo.



Kafulila alisema anakusudia kuwasilisha hoja binafsi kuhoji ufisadi huo na kusisitiza kuwa utaondoka na vigogo aliowataja bungeni jana. Nao, wabunge wawili wa Chadema, Godbless Lema (Arusha Mjini) na Ezekiel Wenje (Nyamagana) walimtaka Naibu Spika wa Bunge, Job Ndugai amwagize Kafulila atoe ushahidi huo na iundwe kamati teule ya Bunge kuchunguza.
Hata hivyo, Kafulila alipotakiwa kufuta kauli hiyo, alisisitiza kuwa amerejea maelezo ya gavana wa BoT kwenye kamati yaliyoonyesha kwamba alishinikizwa kutoa fedha hizo toka Septemba mwaka jana, lakini katika kulinda heshima ya benki, suala hilo alilisogeza hadi Novemba zilipotolewa.
Hivyo, Kafulila alipendekeza iundwe Kamati Teule ya Bunge ili iweze kuchunguza na kuleta ukweli wote, huku akisisitiza kuwa kile alichokisema ni asilimia 10 tu ya ukweli wote anaoujua kuhusu suala hilo.
Hizi ni tuhuma za pili za kashfa kubwa ya ufisadi kuihusisha Benki Kuu ya Tanzania. Ufisadi wa kwanza ulikuwa wa tuhuma za ukwapuaji wa sh bilioni 133 katika Akaunti ya Malipo ya Nje (EPA) uliowahusisha vigogo kadhaa wa serikali kwa kushirikiana na wafanyabiashara mwaka 2005. 

 Chazo Tanzania Daima

No comments:

Post a Comment

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...