Uchunguzi
huo ulibaini kuwa vinasaba vya pembe hizo vilifanana, hivyo kujenga
dhana kwamba baadhi ya watu wamekuwa wakiwinda katika hifadhi hiyo mara
kwa mara katika utaratibu maalumu unaotambuliwa na
Serikali.PICHA|MAKTABA
Ongezeko la kasi ya ujangili nchini
limedaiwa kusababishwa na vitendo vya rushwa, matumizi mabaya ya
madaraka na mfumo dhaifu wa usimamizi wa sheria katika Wizara ya
Maliasili na Utalii.
Kwa mujibu wa
ripoti iliyopewa jina la Urasimishaji wa Ujangili wa Kitaalamu Afrika,
tangu mwaka 2000 wizara hiyo imejikuta katika kashfa za rushwa na
kusababisha mawaziri na watendaji wakuu kuvuliwa nyadhifa zao.
Katika ripoti hiyo, Taasisi ya Kimarekani ya Utunzaji Wanyamapori ya
Born Free USA kwa ushirikiano na Shirika la Ripoti za Kichambuzi na
Takwimu la C4ADS, imeeleza pia jinsi vikundi vya waasi barani Afrika
wanavyoendesha shughuli za ujangili.
Ripoti hiyo iliyozinduliwa mwezi huu nchini Kenya, inaitaja Tanzania
kama kitovu cha kusafirisha pembe za ndovu katika ukanda wa Afrika
Mashariki na Bandari ya Dar es Salaam imekuwa ikishindana na ile ya
Mombasa katika kutumia bandari kibiashara.
Kutoka mwaka
2008 mpaka 2013, inaelezwa zaidi ya tani 20 za pembe za ndovu ama
zilikamatwa zikisafirishwa kuingia au kutolewa katika Jiji la Dar es
Salaam, hii ni kwa mujibu wa taarifa ya Taasisi ya C4ADS.
Ripoti hiyo inafafanua kuwa uchunguzi wa vinasaba (DNA), katika tani 11
za pembe za ndovu zilizokamatwa Taiwan, Japan na Hong Kong mwaka 2006,
ilibainika kuwa pembe 1,500 zilitoka Tanzania (Selous).
Uchunguzi huo ulibaini kuwa vinasaba vya pembe hizo vilifanana, hivyo
kujenga dhana kwamba baadhi ya watu wamekuwa wakiwinda katika hifadhi
hiyo mara kwa mara katika utaratibu maalumu unaotambuliwa na Serikali.
“Kuna udhaifu mkubwa katika usimamizi wa uwindaji halali na wawindaji
wenye vibali hawasimamiwi ipasavyo kufanya uwindaji kwa taratibu
zilizowekwa kisheria. Hivyo hutumia nafasi hiyo kufanya vitendo vya
ujangili,” inasema sehemu ya ripoti hiyo.
Serikali yakanusha
Hata hivyo, Mkurugenzi wa Wanyamapori, Paul Sarakikya alikanusha madai
hayo akisema siyo kweli kwamba wawindaji halali huachwa bila usimamizi,
bali wana mifumo ya kusimamia shughuli hiyo.
“Sikubaliani na ripoti hiyo, tumeshaongea sana juu ya suala hili, Rais
alishalizungumzia na waziri pia. Ufafanuzi ndio huo, hamna ukweli wowote
katika ripoti hiyo,” alisisitiza Sarakikya.
Salakikya alisema idadi ya tembo nchini inazidi kuongezeka katika hifadhi tofauti na upungufu unaoelezwa katika ripoti hiyo.
Mkurugenzi huyo alihoji kuwa kama hakuna usimamizi madhubuti katika
uwindaji halali, wamewezaje kusimamia uwindaji miaka yote mpaka idadi ya
tembo inaongezeka, baada ya upungufu uliokuwepo miaka ya nyuma.
Wakati Sarakikya akisema tembo wanaongezeka, ripoti hiyo inaeleza kuwa
idadi ya tembo katika hifadhi za Selous na Mikumi kwa mwaka 1976,
ilikuwa ni 109,419 lakini kufikia mwaka 2009, idadi hiyo ilishuka hadi
kufikia tembo 38,975.
Nchi zilizoathirika zaidi na ujangili barani Afrika, zinatajwa kuwa ni
Jamhuri ya Afrika ya Kati, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC),
Cameroon, Msumbiji, Kenya, Zimbabwe na Tanzania ambayo pia inatajwa kuwa
kitovu cha usafirishaji wa pembe za ndovu.
Idadi ya tembo waliosalia
Na kwa utafiti uliofanywa na Taasisi ya Frankfurt Zoological Society
mwishoni mwa mwaka 2013, ripoti hiyo inaeleza kuwa ni tembo 13,084
wanaokadiriwa kusalia katika hifadhi, sawa na upungufu wa asilimia 66
katika kipindi cha miaka minne tangu 2009.
Hii imefafanuliwa kuwa zaidi ya tembo 25,000 waliuawa katika Hifadhi ya
Selous ndani ya miaka minne pekee. Pia, ripoti hiyo inabainisha upungufu
wa tembo katika hifadhi ya Ruaha-Rungwa kutoka tembo 35,461 mpaka tembo
20,090 sawa na upungufu wa asilimia 36.5 kuanzia mwaka 1990 mpaka sasa.
No comments:
Post a Comment