Faustina Selali,akiwa katika maumivu makali baada ya
kushambuliwa na mumewe.
Inasikitisha sana jamani. Faustina Selali, 38, mkazi wa
Mgeta, Mvomero mkoani hapa, yupo kwenye mateso makali akijiuguza kutokana na
kipigo alichopata kutoka kwa mumewe wa ndoa aliyemtaja kwa jina la Lugasiani
John Miasiku, kisa kikiwa ni mumewe huyo kutaka kuoa mke wa pili.
Mwanamke huyo amelazwa katika wodi nambi 3 katika Hospitali
ya Rufaa ya Mkoa wa Morogoro, ambapo amesimulia kisa chote mbele ya kamera ya
Uwazi.
KISA CHENYEWE
Akizungumza kwa tabu, Faustina alisema tukio hilo
lililobadilisha historia ya maisha yake na kumwachia machungu moyoni mwake,
lilitokea Juni 25, mwaka huu majira ya saa nne usiku ndani ya nyumba yao.
“Mimi na mume wangu tumeishi kwenye ndoa kwa muda wa miaka
20 na kufanikiwa kupata watoto watano. Kwa kipindi kirefu nilihisi ana uhusiano
wa kimapenzi na mwanamke mwingine, wakati naendelea kumchunguza, mume wangu
akaniambia anataka kuoa mke wa pili,” alisema Faustina kwa uchungu na kuongeza:“Nikamhoji
mume wangu, dini yetu hairuhusu jambo hilo na zaidi ya yote anachotafuta kwa
huyo mke wa pili ni kitu gani wakati tayari mimi nimeshamzalia watoto watano na
bado naendelea kuzaa?
“Hakuwa na jibu la maana, akaendelea kushikilia msimamo wake.
Mwisho nikaona nisimlazimishe sana, nikamwambia kama hivyo ndivyo basi tugawane
mali ili mimi niondoke aje huyo mwenzangu kwani sitakuwa tayari kuishi maisha
ya uke wenza. Kwa kweli hakuwa na jibu la maana.”
Akionyesha sehemu ya jeraha.
HARUFU YA KIFO
“Ugomvi huo ulitokea Jumanne, kesho yake yaani Jumatano
(siku ya tukio) mume wangu alivyorudi shamba nilimtengea ugali kama kawaida.
Alikula vizuri tu... tukapanda kitandani kulala, kama unavyojua tena wanandoa
muda wao wa kuzungumza kwa utulivu ni usiku, nikaamua kuutumia muda huo
kumwuliza mwenzangu.
“Nikamwambia kama bado ana msimamo wake uleule, anipe sehemu
yangu niondoke zangu. Hapo nikawa nimechokoza moto. Ilikuwa ghafla tu, aliamka
kitandani na kuchukua nyundo kisha akaileta kichwani na kunipiga nayo, baadaye
akanipiga mdomoni na kuning’oa meno mawili ya mbele kwa kutumia ile nyundo.
“Hakuishia hapo, akanitoa panga kisha akanicharanga mikono
yote, palepale damu zikaruka kama kachinja ng’ombe. Nilihisi maumivu makali
sana, sikuwahi kupata maumivu makali kama yale. Kusema ukweli nilichanganyikiwa
kabisa na kile kipigo.”
ATUMIA UJANJA KUJIOKOA
“Wakati akiendelea kunipiga bila huruma, alikuwa akisema
dawa yangu mimi ni kufa ili aweze kumchukua huyo mwanamke wake bila usumbufu.
Nilivyosikia hivyo ikabidi nitumie akili; nikajiangusha chini na kujifanya
nimekata kauli ili nisiendelee kuumia.
“Alipoona hivyo kweli akaniacha. Akavaa nguo zake na
kukimbia. Mwanangu mdogo Nesto akanisaidia kunikongoja hadi kwa jirani yetu
Mzee Chota ambaye naye aliita majirani haraka, ilikuwa ni saa sita usiku,
wakanikimbiza hadi Zahanati ya Mlali lakini nikapewa rufaa ya kuletwa hapa
kutokana na hali yangu kuwa mbaya.”
Kwa mujibu wa Bi. Faustina, licha ya mume wake kumfanyia
ukatili huo, ndugu wanaofika hospitalini hapo kumjulia hali, wanasema mumewe
bado hajakamatwa na amekuwa akiendelea kutoa vitisho dhidi yake.
Uwazi lilifunga safari hadi kijijini Mgeta kwa lengo la
kuhojiana na mtuhumiwa huyo na kufanikiwa kumkuta lakini alipomuona mwandishi
wetu, Miasiku alitimua mbio akidhani alifuatwa na askari.chanzo Gpl
No comments:
Post a Comment