Mkurugenzi Mtendaji wa EWP na Mkurugenzi wa Kinukamori
Enterprises, Bw. Alpha Phares Moshi (wa pili kushoto) akimkaribisha
Mratibu Mkazi wa Umoja wa Mataifa na Mwakilishi wa Shirika la maendeleo
UNDP, Alvaro Rodriguez alipowasili kwenye Taasisi isiyo ya kiserikali
inayo shughulika na uhifadhi wa mazingira eneo la Kinukamori, Marangu
mkoani Kilimanjaro wakati wa ziara yake ya kukagua miradi mbalimbali
inayofadhiliwa na UNDP huku akiwa amembatana na Mratibu wa Kitaifa
miradi ya COMPACT mkoani Kilimanjaro, Victoria Nderumaki (wa tatu kulia)
pamoja na Mtaalam wa Mahusiano na Mawasiliano wa Umoja wa Mataifa (UN)
Tanzania Hoyce Temu (wa pili kushoto).
Na mwandishi wetu, Moshi
Taasisi isiyo ya kiserikali inayo
shughulika na uhifadhi wa mazingira eneo la Kinukamori, Marangu mkoani
Kilimanjaro Executive Wilderness Program (EWP) inatafuta dola za
marekani 30,000 kwa ajili ya kuendesha program tatu zenye kutengeneza
ajira, ujasirimali, utunzaji wa mazingira na mvuto kwa watalii
wanaokwenda kupanda mlima Kilimanjaro.
Kauli hiyo wameitoa kwa Mratibu
Mkazi wa Umoja wa Mataifa na Mwakilishi wa Shirika la maendeleo UNDP,
Alvaro Rodriguez wakati alipofanya ziara mkoani Kilimanjaro kuangalia
miradi inayofadhiliwa na Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa
(UNDP).
Uongozi wa EWP and Kinukamori
Enterprises katika taarifa yao kwa Mratibu huyo, iliyosomwa na Mshauri
wao wa fedha Grace Shayo wamesema pamoja na nia yao ya kuhakikisha
maporomoko ya Kinukamori yanaendelea, kwanza kama taasisi na pili kama
mradi wa kuhifadhi mazingira ya Mlima Kilimanjaro ambao ni sehemu ya
urithi wa dunia, wakishirikiana na KINAPA wamefikiria miradi kadhaa
ambayo ikienda kwa pamoja itaendeleza eneo hilo.
Wamesema fedha hizo zitatumika kutoa
elimu ya ujasirimali kwa vijana 300 wanaoishi katika jamii ya Marangu
ambao hutoa huduma mbalimbali kwa wenyeji na pia wageni wakiwemo
watalii.
Kundi hilo linalotakiwa kupewa mafunzo ni pamoja na wapagazi 50, waendesha pikipiki 100, wachuuzi 100 na walima mboga 50.
Mshauri wa fedha wa EWP na Kinukamori Enterprises, Grace Shayo
akisalimiana na Mratibu miradi ya UNDP Kitaifa, Nehemia Mususuri
aliyembata na Bw. Alvaro Rodriguez. Katikati ni Mkurugenzi Mtendaji wa
EWP na Mkurugenzi wa Kinukamori Enterprises, Bw. Alpha Phares Moshi.
Pia fedha hizo zitatumika kwa ajili
ya kuanzisha na kutoa huduma ya chakula kwa wanaopanda mlima Kilimanjaro
kwa lengo la kupunguza uchafu katika mlima huo na wakati huo huo
kuongeza ajira kwa vijana.
Aidha fedha hizo zitatumika
kuanzisha kituo cha mazoezi kwa ajili ya wageni wanaotaka kupanda mlima
Kilimanjaro kujizoesha na hali ya eneo hilo kabla ya kupanda mlima.
Grace alisema shughuli zote hizo zimelenga vijana kuwa na maeneo ya kudumu yenye ajira endelevu.
Pamoja na kutoa ombi la kusaidiwa
kupata fedha hizo, wameshukuru pia kwa misaada iliyotolewa na Shirika la
Umoja wa Mataifa la Maendeleo (UNDP) kwa kupitia COMPACT.Wamesema kama
si misaada hiyo eneo hilo ambalo lina historia ya kuharibiwa kwa
mazingira yake lisingekuwa linavutia na kutoa ajira kama ilivyo sasa.
Eneo hilo limeboreka mazingira baada
ya kuanzishwa kwa taasisi hiyo ya EWP kazi iliyofanywa na Bw. Alpha
Phares Moshi ambaye kwa sasa ndiye Mkurugenzi Mtendaji wa EWP na
Mkurugenzi wa Kinukamori Enterprises ambapo kwa kushirikiana na KINAPA
na COMPACT vijana walipewa elimu iliyowezesha kutengenezwa kwa mradi wa
kuhifadhi mazingira ya mto Una wenye maporomoko ya Kinukamori.
Bw. Alvaro Rodriguez akisaini kitabu cha wageni mara baada ya kuwasili kwenye mradi huo.
Vijana hao ambao ndio wanaoishi
katika mteremko wa mlima Kilimanjaro walianza shughuli hizo mwaka 1997
na kuanza kufikiria kuyatengeneza maporomoko ya Kinukamori kama chanzo
cha kivutio katika juhudi za kuhifadhi mto Una.
Walisema kwa kuzingatia madhumuni ya
kuanzishwa kwa mradi huo vijana na wanawake walianza kurejesha hali ya
mazingira kwa kuyaweka bora na kudhibiti uharibifu wa ikolojia.
Kutokana na juhudi hizo miti zaidi
ya 5000 mingi ikiwa ya asili ilipandwa kandoni mwa mto na sasa miti hiyo
inatumika kutoa mafunzo na kurejesha hali ya upatikanaji wa maji ya
kutosha kwa ajili ya wananchi wa Marangu.
Aidha wanyama na ndege waliokuwa wametoweka kutokana na uharibifu wa mazingira uliokuwepo kwanza wameshaanza kurejea eneo hilo.
Pamoja na mafanikio hayo EWP
wanakabiliwa na changamoto kubwa hasa ukubwa wa eneo la shughuli zao
ambalo ni ndogo na sasa wanataka kusaidiwa kufika hadi maeneo ya
chemchem ya Soko iliyopo Kahe.
Mshauri wa fedha wa EWP na Kinukamori Enterprises, Grace Shayo
akisoma taarifa ya taasisi yao kwa Mratibu Mkazi wa Umoja wa Mataifa na
Mwakilishi wa Shirika la maendeleo UNDP, Alvaro Rodriguez.
Aidha wamesema wanakabiliwa na
tatizo la fedha na hasa kushawishi vijana kujikita zaidi katika masuala
ya uhifadhi wa mazingira na utalii wa kitamaduni.
Naye Mwakilishi wa Mashirika ya
Umoja wa Mataifa pamoja na kuwapongeza EWP kwa kufanikisha kurejesha
mazingira katika hali ya kawaida katika eneo hilo amesema kwamba
wataendelea kushirikiana nao kuhakikisha kwamba shughuli za hapo
zinahifadhi mazingira na kutoa ajira kwa vijana.
Alisema duniani nzima kwa sasa
inakabiliwa na tatizo la ajira kwa vijana ambao kutokana na kukosekana
kwa ajira wanatopea katika ulevi na hivyo kuhatarisha nguvu kazi hiyo
muhimu.
Alisema hata Tanzania pamoja na
kuanza kufikiria kuwa na uchumi wa gesi, hatua hiyo itachukua muda
lakini kuna haja ya vijana wanaomaliza shule wakawajibika katika miradi
mbalimbali ya uhifadhi na maendeleo ya kiuchumi.
Mshauri wa fedha wa EWP na Kinukamori Enterprises, Grace Shayo
akikabidhi taarifa ya taasisi hiyo kwa Mratibu Mkazi wa Umoja wa
Mataifa na Mwakilishi wa Shirika la maendeleo UNDP, Alvaro Rodriguez
aliyetembelea mradi wao na kujionea maendeleo yao.
Mwakilishi huyo pamoja na kutotoa
ahadi katika ombi la taasisi hiyo amesema kwamba wataangalia nini cha
kufanya kwani alifika eneo hilo kujifunza na kuona maendeleo kwani ana
miezi miwili tu toka ameingia nchini kuwakilisha mashirika ya Umoja wa
Mataifa.
Alisema amefurahishwa na maendeleo yaliyopo na hasa kwa kuzingatia kwamba kulikuwa na tatizo la raslimali kufanya shughuli hiyo.
Alisema anatambua changamoto
zilizopo cha ongezeko la watu, tatizo la ajira kwa vijana na mabadiliko
ya tabia nchi na kwamba wataendelea kushirikiana na taasisi hiyo kuona
kwamba changamoto hizo zinakabiliwa na kufutwa.
Bango linaloonyesha tarehe ya kuzinduliwa kwa mradio huo wa COMPACT unaofadhiliwa na UNDP.
Baadhi ya sheria zilizowekwa kwenye maporomoko ya maji ya Kinukamori yaliyopo Marangu mkoani Kilimanjaro.
Mtaalam wa Mahusiano na Mawasiliano wa Umoja wa Mataifa (UN)
Tanzania Hoyce Temu akiwa amefuatana na Mratibu Mkazi wa Umoja wa
Mataifa na Mwakilishi wa Shirika la maendeleo UNDP, Alvaro Rodriguez
kutembelea mazingira ya taasisi hiyo pamoja na vivutio vya kitalii
vilivyomo kwenye Maporomoko ya maji ya Kinukamori yaliyopo Marangu
mkoani Kilimanjaro.
Pichani juu na chini ni mtoa maelezo kwa watalii (Guide) wa EWP
na Kinukamori Enterprises, Pascal Cosma akitoa maelezo ya sehemu ya
utamaduni wa Kabila la Kichaga kwa Mratibu Mkazi wa Umoja wa Mataifa na
Mwakilishi wa Shirika la maendeleo UNDP, Alvaro Rodriguez aliyembatana
na ujumbe wake kutembelea miradi mbalimbali inayofadhiliwa na UNDP.
Sanamu la aliyekuwa Chifu wa kabila la Wachaga Chifu Thomas Marealle lilipo kwenye taasisi hiyo.
Pichani juu na chini ni mtoa maelezo kwa watalii (Guide) wa EWP
na Kinukamori Enterprises, Pascal Cosma akiendelea kutoa maelezo ya
tamaduni mbalimbali za kabila la wachaga ikiwemo na sanamu mbalimbali
zilizowekwa kwenye taasisi hiyo.
No comments:
Post a Comment