Polisi
mkoani Arusha imemuua kinara namba mbili wa ujambazi wa kuua na kupora
wanawake, Wecensilaus Matei(32), maarufu Mandela, Jacob au Star.
Jambazi huyo anadaiwa kushirikiana na jambazi aliyeuawa hivi karibuni, Ramadhan Abdallah (37), maarufu ‘Ramandonga’.
Akithibitisha kuuawa kwa jambazi huyo, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha,
Liberatus Sabas, alisema Mandela alikuwa anasakwa kwa muda mrefu na
aliuawa jana saa 10 alfajiri akiwa ndani ya nyumba ya bibi kizee eneo la
Nduruma, Arumeru.
Alisema aliuawa katika majibizano ya risasi na polisi waliomtaka
kujisalimisha na kukataa ndipo walipolazimika kuvunja mlango wa nyumba
na alipotoka alianza kuwarushia risasi polisi.
Alisema wakiwa njiani kumpeleka hospitali ya Mkoa ya Mt Meru walimuhoji
na kukiri kufanya matukio mbalimbali ya ujambazi akiwa dereva wa
pikipiki ambapo pia aliwataja watu waliokuwa wakimsaidia kufanya uhalifu
huo ikiwemo aliyemnunulia pikipiki, James Lyatuu (36), ambaye ni
mfanyabiashara wa vyuma chakavu.
Jambazi huyo amekuwa tishio kubwa jijini Arusha na ameshafanya matukio
mengi ya ujambazi ikiwemo la Agosti 6, mwaka huu saa 3.00 usiku eneo la
kwa Iddi, alimuua kwa risasi Shamimu Rashid na Agosti 21, 2014 saa1.00
usiku katika eneo la Olasiti, alimuua kwa kumpiga risasi mtoto Christene
Nelson.
Wakati huo huo, polisi inamshikilia mkazi mmoja wa Murieti jijini hapa,
Amon Losioku (32), kwa tuhuma za kufanya mauaji ya mdogo wake Francis
Losioku kwa kumchoma kisu shingoni.
Kwa
mujibu wa Kamanda Sabas, katika tukio hilo baba mzazi wa marehemu,
Losioku Veneti (70), alifariki dunia baada ya shuka alilokuwa amevaa
kunasa kwenye mlango.
No comments:
Post a Comment