JESHI la
Kujenga Taifa (JKT) limewataka vijana waliomaliza katika jeshi hilo,
kutambua kuwa walikula kiapo cha utii wakati wa kuhitimu mafunzo, hivyo
suala la kuandamana ni kinyume na kiapo chao.
Vijana
hao waliotumikia Jeshi la Kujenga Taifa Operesheni za nyuma na kumaliza
mkataba wa miaka miwili, wameambiwa shinikizo lao la kulazimisha ajira
kwa kuandamana ni kinyume cha sheria za nchi.
Taarifa
kwa vyombo vya habari iliyotolewa na Makao Makuu ya jeshi hilo, jijini
Dar es Salaam mwishoni mwa wiki, ilisema kipengele kimoja cha masharti
ya kujiunga na JKT kinasema baada ya mkataba, wanapaswa kurejea nyumbani
na hawapaswi kudai jeshi liwatafutie ajira. Ilieleza kwamba masharti ya
jeshi hilo, huwekwa bayana kwa vijana wanapojiunga na JKT.
Vijana
hao wanatakiwa kujua masharti hayo na taratibu za JKT na kuelewa kuwa
JKT halitoi ajira. Taarifa hiyo ilinukuu kipengele kimojawapo cha
masharti, kinachosema “Kwa kipindi chote nitakachokuwa ndani ya Jeshi la
Kujenga Taifa nitakuwa nafanya mafunzo ya kijeshi na ya stadi za kazi
na maisha, na baada ya mkataba nitarejea nyumbani. Hivyo sitalidai Jeshi
la Kujenga Taifa ajira, wala kulitaka linitafutie ajira/ kazi”.
Ufafanuzi
huo ulitolewa, kutokana na vijana zaidi ya 200 waliohitimu mafunzo ya
JKT kuanzia mwaka 2000 hadi mwaka 2013, kutangaza wiki iliyopita kuwa
wataandamana siku yoyote wiki hii kwenda kwa Rais Jakaya Kikwete,
kumweleza shida zao, ikiwemo kutokuwa na ajira tangu wamalize mafunzo.
Jeshi
hilo lilisema ni vema vijana hao, wakatambua kuwa tatizo la ajira siyo
kwao peke yao, ni tatizo la ulimwengu mzima Tanzania, ikiwemo hivyo
wanashauriwa kutumia stadi za kazi kujiajiri wenyewe.
“Kutokana
na dhumuni la kuundwa JKT Taifa, halina dhamana ya kuajiri bali kufunza
vijana wa taifa hili umoja, stadi za kazi na uzalendo baada ya hapo
wawe wenye sifa za kuajiriwa hupata ajira katika taasisi mbalimbali za
serikali na binafsi,” ilisema taarifa hiyo.
Hata
hivyo, jeshi hilo limesema tangu mwaka 2003 hadi 2014, vijana 24,708
wameajiriwa katika vyombo vya ulinzi na usalama. Kati ya hao, vijana
21,977 wakiwemo wavulana 17,307 na wasichana 4,670, wameajiriwa na Jeshi
la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ).
Kwa
upande wa Polisi, vijana 3,965 wameajiriwa ambao kati yao, wavulana ni
2,943, Magereza wameajiriwa 2,139 kati yao wavulana ni 2,044, Zimamoto
vijana 100 wavulana wakiwa 78 na taasisi zingine wameajiriwa vijana 592.
Aidha,
vijana 1,622 wameajiriwa katika taasisi mbalimbali kama vile migodi ya
dhahabu ya Geita, Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA) na Shirika la
Hifadhi za Taifa (Tanapa).
Taarifa
hiyo ilisema JKT ilianzishwa Julai 10, 1963 kwa lengo la kuwaweka pamoja
vijana na kuwapa malezi, kuhusu uzalendo na umoja ili kuondoa dalili za
matabaka, zilizoanza kujitokeza katika jamii baada ya uhuru.
Serikali ilirejesha mafunzo ya jeshi hilo kwa vijana wa kujitolea mwaka 2001 baada ya kusitishwa mwaka 1994.CHANZO:HABARI LEO
No comments:
Post a Comment