Mkurugenzi wa Huduma za Sheria wa Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Rugonzibwa Mujunangoma.
Taasisi
ya Kuzuia na Kupamba na Rushwa (Takukuru) imembadilishia hati ya
mashtaka Mkurugenzi wa Huduma za Sheria wa Wizara ya Ardhi, Nyumba na
Maendeleo ya Makazi, Rugonzibwa Mujunangoma aliyekuwa akikabiliwa na
shtaka la kupokea rushwa ya Sh 323 milioni toka kwa James Rugemalira
fedha ambazo ni sehemu ya fedha za Akaunti ya Tegeta Esrow.
Katika
hati mpya iliyosomwa leo na Mwendesha Mashtaka wa Takukuru Leonard Swai
mbele ya Hakimu Mkazi wa Mahakama ya Kisutu, Emillius Mchauru aioneshi
tena kuwa fedha zilizopokelewa na Mujunangoma toka kwa Rugemalira ni
sehemu ya fedha za Akaunti ya Tegeta Escrow.
Swai
kupitia hati hiyo mpya alidai kuwa Februari 5, 2014 Mujunangoma akiwa
mtumishi wa serikali kama Mkurugenzi wa Huduma za Sheria wa Wizara ya
Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Rugonzibwa Mujunangoma alipokea
rushwa ya Sh Sh323 milioni kupitia akaunti yake namba 00120102602001
iliyopo kwenye benki ya Mkombozi .(P.T)
Alidai
kuwa mshtakiwa huyo alipokea kiasi hicho cha fedha kutoka kwa James
Burchard Rugemalira, ambaye ni mshauri huru wa kitaalamu, mkurugenzi wa
VIP na mkurugenzi wa zamani wa Kampuni ya Kufua Umeme ya IPTL kama tuzo
kwa kushughulikia mambo ya ufilisi wa muda wa kampuni hiyo.
Aliendelea
kudai kuwa baada ya kujipatia kiasi hicho cha fedha alishindwa kueleza
maslahi yake kwa Katibu Mkuu wa Wizara yake ya Ardhi, Nyumba na
Maendeleo ya Makazi na kwenye tume ya maadili ya Viongozi.
Baada ya
kusomewa mashtaka hayo, Mujunangoma ambaye anatetewa na mawakili Deo
Ringia na Jamuhuri Johnson alikana na upande wa mashtaka ulidai kuwa
upelelezi umekamilika na wapo tayari kwa ajili ya kumsomea mshtakiwa
huyo maelezo ya awali (PH) yanayohusiana na shtaka hilo linalomkabili.
Wakili
Deo Ringia alitoa taarifa mahakamani hapo kuwa kutokana na uchambuzi
walioufanya wameona katika kesi hiyo kuna masuala ya Kikatiba ambayo
wanapenda mahakama iyaangalie na kuyatolea maelekezo. Baada ya kutolewa
kwa taarifa hiyo Hakimu Mchauru ameiahirisha kesi hiyo hadi Februari
24,2015 kwa ajili ya kuisikiliza taarifa hiyo.
Awali
Shtaka la
awali, Mujunangoma alikuwa akidaiwa kuwa Februari 5, 2014 katika Benki
ya Mkombozi iliyopo wilayani Ilala, Dar es Salaam, akiwa Mkurugenzi wa
Huduma za Sheria wa Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi
alipokea rushwa ya kiasi hicho cha fedha kutoka kwa James Burchard
Rugemalira kama tuzo kwa kushughulikia mambo ya ufilisi wa muda wa
kampuni hiyo fedha ambazo ni sehemu ya fedha za Akaunti ya Tegeta
Escrow.
Mshtakiwa
huyo anayedaiwa kufanya kosa hilo, kinyume na kifungu cha 15 (1)cha
Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa, Namba 11 ya mwaka 2007 yupo nje
kwa dhamana na akaunti yake inayodaiwa kupokea rushwa toka kwa
Rugemalira imezuiwa.
Chanzo:Mwananchi
No comments:
Post a Comment