- Mbunge huyo alipanga kuliaga bunge na alisema amekwishapata ruksa ya Spika kuwa angesimama bungeni kuwaaga wabunge na wanachama wa Chadema baada ya chama hicho kumtimua uanachama wake hivi karibuni, lakini ghafla mpango huo uliyeyuka kwa kile kilichoelezwa kuwa Spika amemkatalia.
Dar es Salaam. Pamoja na mpango
wa Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe kuliaga Bunge kukwama jana,
Chama cha ACT- Tanzania kimetangaza kukamilisha maandalizi ya kumpokea
mwanasiasa huyo kuanzia leo.
Mbunge huyo alipanga kuliaga bunge na alisema
amekwishapata ruksa ya Spika kuwa angesimama bungeni kuwaaga wabunge na
wanachama wa Chadema baada ya chama hicho kumtimua uanachama wake hivi
karibuni, lakini ghafla mpango huo uliyeyuka kwa kile kilichoelezwa kuwa
Spika amemkatalia.
Tangu kuanzishwa kwa chama hicho mwaka mmoja
uliopita, Zitto amekuwa akihusishwa kukianzisha, hivyo kitendo chake cha
kujiunga nacho kitahitimisha mjadala wa muda mrefu wa mashabiki wake
waliokuwa wakihoji wapi ataelekea baada ya kung’olewa Chadema.
Akizungumza na gazeti hili jana, Katibu Mkuu wa
ACT, Samsom Mgamba aliangua kicheko na bila kuuma maneno alisema:
“Hahahaa... tutampokea kuanzia kesho (leo) na maandalizi yamekamilika.”
Alipotakiwa kueleza wapi mapokezi hayo yatafanyika
alisema: “Hilo mbona liko wazi, yatafanyikia makoa makuu yetu (yapo
Makumbusho, Dar es Salaam) lakini kwa taarifa zaidi tutawajuza.”
Zitto anaingia ACT ikiwa ni siku tisa kabla ya
chama hicho kufanya uchaguzi wake mkuu, huku akitajwa kuwa ameandaliwa
kushika wadhifa wa mwenyekiti kuendeleza harakati zake za siasa.
Hivi karibuni, chama hicho kilimvua uongozi
aliyekuwa mwenyekiti mwanzilishi, Lucas Limbu kutokana na mgogoro
uliokuwapo baina ya viongozi na kufanya nafasi hiyo kubaki wazi.
Tayari washirika wa Zitto waliohusishwa naye
kuandika waraka wa mapinduzi ndani ya Chadema na baadaye kufukuzwa
uanachama, Mwigamba na Profesa Kitila Mkumbo wametua ndani ya chama
hicho kipya.
Chama hicho ambacho kinaendelea na uchaguzi katika
ngazi ya mikoa kikibakiza Mkoa wa Geita unaofanya uchaguzi wake kesho.
Kitaanza vikao vyake vya kitaifa Machi 27 na kuhitimisha kwa mkutano
mkuu Machi 29.
Akizungumzia uchaguzi huo, Mwigamba alisema:
“Maandalizi yanakwenda vizuri na hakuna shaka utafanikiwa kwa kiasi
kikubwa na tunawaomba Watanzania watuunge mkono.”
Tangu juzi, Zitto alitarajiwa kuliaga Bunge lakini
hakufanya hivyo kwa kilichoelezwa kuwa aliitwa na Spika wa Bunge, Anne
Makinda na kupewa ushauri kuwa afanye hivyo jana jioni.
Jana asubuhi mbunge huyo hakuingika katika kikao
cha Bunge lakini alionekana katika viwanja vya Bunge akiwa amevaa shati
la drafti na suruali ya kaki akizungumza na rafiki yake wa karibu, Deo
Filikunjombe ambaye ni mbunge wa Ludewa kupitia CCM.
Mwananchi
Mwananchi
No comments:
Post a Comment