ADV

ADV

ADVERTISEMENT CORNER

HUDUMA YA KUKATA TICKET ZA NDEGE ONLINE


SOMA HABARI

SOMA HABARI
Showing posts with label Bomu Arusha. Show all posts
Showing posts with label Bomu Arusha. Show all posts

Monday, June 17, 2013

WABUNGE WA CHADEMA WAGOMA KUINGIA BUNGENI KUFUATIA BOMU LA ARUSHA...IGP ATOA NAMBA YAKE KWA MTU YEYOTE MWENYE TAARIFA





Wakati Jeshi la Polisi nchini limesema limepata taarifa za mwonekano wa mtu aliyetupa bomu katika mkutano wa kampeni wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) Arusha,Mwenyekiti wa chama hicho Freeman Mbowe amesema wabunge wake leo hawataingia bungeni.

Akizungumza na waandishi wa habari jana, Mbowe alisema wabunge hao watawasili Arusha kwa ajili ya kuungana na wananchi pamoja na wanachama kwenye msiba huo.

Alisisitiza kwamba kuanzia leo mahema yatawekwa viwanja vya Soweto kwa ajili ya kuomboleza msiba huo na  mara polisi wakimaliza uchunguzi wao na kutoa majibu juu ya vifo hivyo, marehemu hao watasafirishwa.

Wakati Mbowe anatoa kauli hiyo Waziri wa Mambo ya Ndani, Dk Emmanuel Nchimbi akizungumza jana mjini Arusha na waandishi wa habari, alisema taarifa za awali zinaonesha mlipuko huo ni bomu la kutupwa kwa mkono (grumeti)  na hivi sasa timu ya wataalamu  ikiongozwa na Kamishna wa Operesheni Maalumu wa Jeshi la Polisi, Paul Chagonja inaendelea na uchunguzi wa tukio hilo.

Naye  Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini,  Inspekta Jenerali wa Polisi (IGP), Said Mwema  katika taarifa yake kwa vyombo vya habari ameahidi kupambana na kuhakikisha wahusika wanapatikana.

Alitoa taarifa hiyo jana kwa waandishi wa habari Dar es Salaam na kusema hadi jana, watu waliothibitika kufa katika tukio hilo ni wawili na 68 ni majeruhi.

Waliokufa ni Katibu wa Baraza la Wanawake (Bawacha) wa Chadema, Kata ya Sokoni 1, Judith Moshi (25) na mtoto aliyejulikana kwa jina moja la Justin. 

"Mpaka hivi sasa  watu waliokufa ni wawili  na wengine 68 wamejeruhiwa na mlipuko huo, lakini naahidi kuwa tutapambana na kuhakikisha tunawapata wahusika," alisema Mwema.

Sanjari na kupatikana taarifa juu ya mtu aliyetupa bomu, Mwema alisema  timu ya jeshi hilo imetumwa kutoka makao makuu kwenda Arusha kuongeza nguvu katika upelelezi.

Hata hivyo, hakufafanua zaidi juu ya mtuhumiwa huyo kutokana na kile alichosema taarifa husika  zinafanyiwa uchunguzi  kabla ya  kuwakamata watu sahihi waliohusika na tukio hilo.

Kwa mujibu wa IGP Mwema, timu ya polisi kutoka Makao Makuu inayoongozwa na makamishna wawili, imeondoka  kwenda mkoani Arusha kuongeza nguvu katika operesheni na upelelezi.

Timu hiyo inaongozwa na Kamishna wa Operesheni na Mafunzo, Paul Chagonja na Isaya Mngulu kutoka Idara ya Upelelezi wa Makosa ya Jinai, wakishirikiana na vyombo vingine vya ulinzi.

Alisema polisi inafanya operesheni kali nchini kote kuhakikisha inawatia mbaroni watu wote waliowezesha, waliofadhili na waliotenda uhalifu huo.

"Kikubwa wananchi waendelee kuwa watulivu na waendelee kutoa ushirikiano kwa wakati wote uchunguzi ukiendelea," alisema.

IGP ametaka mtu yeyote atakayekuwa na taarifa za wahalifu hao, atoe taarifa kupitia namba yake ya simu ambayo ni 0754 785557 au kwenye kituo chochote cha polisi ili wakamatwe. 

‘Kwa nini  iwe Arusha’ hii ni kauli ya Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Mulongo aliyoitoa baada ya kutembelea majeruhi katika Hospitali za Mount Meru, St Elizabeth pamoja na Hospitali ya Arusha Lutheran Medical Centre jijini.

“Nawapa pole sana ndugu zangu wa Chadema, na wana Arusha kwa ujumla pamoja na watanzania. Lakini najiuliza kwa nini Arusha …tukio hili limenihuzunisha sana na nawaomba tusiingize masuala ya kisiasa, tuache polisi wachunguze tukio hili kwani timu ya wataalamu kutoka Jeshi la Ulinzi la Wananchi Tanzania (JWTZ) pamoja na wataalamu wengine wanachunguza tukio hili na wahusika watachukuliwa hatua.’’

Mulongo ambaye tukio hilo la juzi limekuja ikiwa ni  mwezi mmoja tangu kutokea kwa mlipuko katika Kanisa Katoliki la Joseph Mfanyakazi la Olasiti, alisema jana anayefanya ulipuaji wa mabomu na kumwaga damu za watu mbalimbali na wengine kufa, ipo siku Mungu atamhukumu.

Kati ya majeruhi  59  waliolazwa kwenye hospitali hizo, wawili wamehamishiwa Hospitali ya KCMC kutoka Hospitali ya  AICC kwa matibabu. Wagonjwa wengi wamelazwa hospitali ya Selian ambao ni 40. Hata hivyo, wanane waliruhusiwa baada ya matibabu. 

Mkuu wa Mkoa alisema  anajisikia mnyonge kutokana na matukio hayo mawili tofauti; mlipuko wa kanisani na la juzi wakati Chadema ilipokuwa ikihitimisha kampeni zake za udiwani kwenye kata nne za Themi, Kaloleni, Elerai na Kimandolu ambao hata hivyo uliahirishwa kutokana na tukio hilo.

Mulongo alitaka wananchi  wasihusishe na masuala ya kisiasa badala yake wawaachie polisi kuchunguza tukio hilo. Kwa mujibu wa Mulongo, watu kadhaa wamekamatwa.

Katika kipindi kisichozidi miezi miwili, mji wa Arusha umeshuhudia majeruhi wasiopungua 130, na vifo vya watu watano vilivyotokana na kurushwa mabomu na watu wasiojulikana katika mikusanyiko kanisani na kwenye mkutano huo wa siasa wa Chadema.

Katika tukio la mwezi uliopita katika Kanisa Katoliki la Mtakatifu Joseph Mfanyakazi,  watu watatu walifariki na wengine wapatao 59 kujeruhiwa. 

Mmoja wa watuhumiwa ambaye ni dereva wa pikipiki maarufu kama bodaboda, Victor Ambrose  alifikishwa mahakamani akidaiwa kuhusika katika shambulio hilo.

Akizungumza na waandishi wa habari, daktari wa hospitali ya Selian, Paul Kisanga alisema walipokea wagonjwa 48  kabla ya wanane kuruhusiwa. 

Alisema miongoni mwa wagonjwa hao, wamo watoto watano wanne wakiwa wa kiume na mmoja wa kike. Mtoto Fahad Jamal (7)  amelazwa kwenye wadi ya wagonjwa mahututi chini ya uangalizi wa madaktari.

Hospitali ya St Elizabeth wapo wagonjwa wanane na Mount Meru imepokea wagonjwa tisa. Mganga Mkuu wa Mkoa wa hospitali ya Mount Meru, Frida Mokiti alisema wamepokea miili ya marehemu wawili ambao ni Judith Moshi (25) ambaye ni Katibu wa Baraza la Wanawake (Bawacha)  kata ya Sokoni 1, Jijini Arusha pamoja na mtoto aliyejulikana kwa jina moja la Justin (13). 

Kwa mujibu wa majeruhi wa tukio hilo,  Abraham Samuel waliona kitu kikiwa kwenye mfuko wa rambo kikirushwa juu na baada ya muda mfupi walisikia vilio na wengine kuzimia.

Kitu hicho kilirushwa kabla ya  Mwenyekiti wa Taifa wa Chama hicho Taifa, Freeman Mbowe kuhitimisha kampeni za uchaguzi za udiwani wa kata nne za Jimbo la Arusha Mjini. 

Mlipuko huo unadaiwa kuwa ulitokea jirani na gari la matangazo la Chadema, aina ya Mitsubishi Fuso lililokuwa karibu na jukwaa alilokuwa akitumia Mbowe.

Mwenyekiti wa Chadema, Mbowe amedai tukio hilo si la bahati mbaya bali lilipangwa na kundi la watu. 

Akizungumza na waandishi wa habari jana, alisema wabunge wa chama hicho leo hawataingia bungeni bali watawasili jijini Arusha kwa ajili ya kuungana na wananchi pamoja na wanachama wa kwenye msiba huo.

Kwa mujibu wa Mbowe, marehemu Judith atapelekwa mkoani Kilimanjaro na Justin atapelekwa mkoani Tabora kwa ajili ya maziko mara baada ya polisi kukamilisha uchunguzi juu ya tukio hilo.

Alisisitiza kwamba kuanzia leo mahema yatawekwa viwanja vya Soweto kwa ajili ya kuomboleza msiba huo na  mara polisi wakimaliza uchunguzi wao na kutoa majibu juu ya vifo hivyo marehemu hao watasafirishwa.

‘’Nimetembelea majeruhi jana hospitalini lakini kwa Hospitali ya Selian, Arusha Lutheran Medical Centre majeruhi ni wengi lakini walioumia sana ni watoto kuna mtoto mmoja amekatika mkono na mguu ambaye ni Sharifa Jumanne na Amiri Ally ana vyuma vitatu mwilini mwake,’’alisema Mbowe.

Ingawa polisi imesema inaendelea na uchunguzi wa tukio hilo kabla ya kutoa taarifa kamili, Mbowe aliwaambia waandishi wa habari kwamba zipo taarifa kwamba shambulio hilo liliambatana na risasi za moto.
Chama cha Wananchi (CUF) kupitia kwa Mwenyekiti wake, Profesa Ibrahim Lipumba, kimelaani tukio hilo na kutaka Serikali ichukue hatua za haraka na kukamata waliohusika na matukio hayo iwe fundisho.

“Hatuna sababu na tusijenge utamaduni wa nchi yetu kugeuka eneo ambalo palipo na mkusanyiko mabomu yanalipuka, Tanzania ni nchi ya amani, kwa matukio haya CUF tunalaani kwa nguvu zote na kutoa pole kwa familia zilizoathirika,” alisema Lipumba.

Lipumba alisema kitendo kilichofanyika katika mkutano huo wa Chadema ni unyama wa kutisha wenye makusudi ya kundi fulani kutekeleza azma yao dhidi ya chama, watu, kundi na viongozi.

Alisisitiza kuwa utamaduni huo wa kufanya unyama katika mkusanyiko wa watu  unapaswa kudhibitiwa mapema ili kuepusha madhara mengine ndani ya jamii kwa kusababisha vifo, ulemavu wa kudumu na familia tegemezi.

“Tumefikia hatua mbaya sana ya kufanya siasa za mabomu huu ni utamaduni unaopaswa kukemewa na kupingwa, matukio haya yanajirudia kutokana na Serikali  yenyewe kuyakaribisha kwa kushindwa kuwachukulia hatua kali wahusika, tunaomba dola ifanye ifanyalo katika uchunguzi wake na kuwakamata na kuwafikisha wahusika kwenye vyombo vya sheria,” alisisitiza.

Saturday, June 15, 2013

MWENYEKITI WA CHADEMA FREEMAN MBOWE, GODBLELSS LEMA WANUSURIKA KUUAWA NA BOMU ARUSHA.


Majeruhi. Mungu urehemu tz 





 

MWENYEKITI wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Freeman Mbowe, amenusurika kuuawa kwa kitu kinachodhaniwa kuwa ni bomu, lililolipuka katika mkutano wa hadhara wa kampeni za udiwani mkoani Arusha.

Mbali ya Mbowe, viongozi wengine mbalimbali waandamizi wa chama hicho, akiwamo Mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema, walinusurika katika mlipuko huo wa bomu hilo lililorushwa katika Uwanja wa Soweto muda mfupi baada ya mwenyekiti huyo kumaliza kumnadi mgombea udiwani wa Kata ya Kaloleni, Emanuel Kessy, jijini hapa.
Habari kutoka eneo la tukio zilisema kuwa watu kadhaa wanasadikiwa kufariki dunia na wengine zaidi 15 wamejeruhiwa sehemu mbalimbali za miil
i yao ikiwamo miguuni na kichwani  wakiwamo watoto wawili wanaodaiwa kuvunjika miguu.

Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Arusha, Liberatus Sabath, alithibitisha kuwa watu wawili waliuawa katika mlipuko huo na kulielezea tukio hilo kuwa ni kubwa na baya kuendelea kutoka mjini hapa.

Mwezi mmoja uliopita, mlipuko wa bomu kama hilo ulitokea katika Kanisa Katoliki Olasiti la Joseph Mfanyakazi na kusababisha vifo vya watu watatu na wengine kadhaa kujeruhiwa.

Mmoja wa mashuhuda aliyezungumza na Tanzania Daima Jumapili muda mfupi baada ya mlipuko wa jana, alisema alijitokeza mtu ambaye hakujulikana anapotokea na kurusha bomu la mkono katikati ya umati na bomu hilo kutoa kishindo kikubwa.

Alisema baada ya mtu huyo kurusha bomu hilo baadhi ya wananchi na wafuasi wa CHADEMA walimuona, walianza kumkimbiza na kabla hawajamfikia polisi waliokuwa wameweka ulinzi katika eneo hilo waliingilia kati na kuzuia mtu huyo asifikiwe.

Bomu lililorushwa linadaiwa kuwa lilielekezwa katika jukwaa walilokuwa Freeman Mbowe na viongozi wengine ambao muda mfupi kabla ya tukio hilo walikuwa wameshuka jukwaani kwa ajili ya kuondoka katika eneo hilo.

Hali katika eneo la tukio ilikuwa mbaya baada ya damu kutapakaa sehemu mbalimbali ya uwanja wa Soweto na majeruhi zaidi ya 20 wakikimbizwa katika hospitali za jijini humo.

Wafuasi wa CHADEMA waliendelea kukakaa katika uwanja huo huku wakihanikiza kwa wimbo wa kukishutumu Chama Cha Mapinduzi (CCM) kuwa kinawaua.

Chanzo kingine kilieleza kuwa katika majeruhi waliopelekwa katika Hospitali ya Mount Meru, mtoto mdogo ambaye jina lake halijajulikana amefariki dunia.

Mwenyekiti wa CHADEMA Mkoa wa Arusha, Samson Mwigamba, alisema bomu hilo ni mbinu ya watu wanaohofia kushindwa katika uchaguzi huo na kuwataka wafuasi wao kutoka maeneo yasiyo na uchaguzi kujitokeza kwa wingi kulinda kura zitakazopigwa leo.

Hali katika Hospitali ya Mount Meru
Tanzania Daima Jumapili lilishuhudia majeruhi hao wakiingizwa na kutolewa katika Hospitali ya Mount Meru mara baada ya kutokea kwa tukio hilo lililotokea saa 11:40 muda mfupi baada ya Mbowe kumaliza kuhutubia wananchi wa kata hiyo na kumuombea kura mgombea huyo.

Katika Hospitali ya Mount Meru, umati mkubwa wa wafuasi wa CHADEMA ulifurika muda mfupi baada ya kutokea kwa tukio hilo, ambao wengi wao walionekana kushinikiza wauguzi wachache waliokuwepo hospitalini hapo kuwapatia majeruhi huduma ya kwanza.

Zoezi zima la kushinikiza wauguzi hao kuwapatia huduma majeruhi hao liligeuka baada ya baadhi ya wauguzi kujificha wakiogopa umati huo wa wafuasi wa CHADEMA, hivyo majeruhi kukosa huduma ya kwanza.

Hali hiyo iliwalazimu wafuasi wa CHADEMA kubeba majeruhi hao waliokuwa wakivuja damu katika miili yao kwa kutumia magari binafsi na kuwahamishia hospitali mbalimbali ikiwamo Hospitali ya Rufaa ya Kanisa la Kiinjili la Kilutheri ya Seliani ya jijini hapa.

Mmoja wa wafuasi wa CHADEMA aliyejitambulisha kwa jina la Martin Lucas, alidai wakiwa katika Uwanja wa Soweto huku mkutano ukiendelea kwa amani na utulivu na Mwenyekiti wa CHADEMA alipomaliza kuhutubia na kushuka jukwaani akielekea kupanda gari lake tayari kuondoka, ghafla mlipuko mkubwa ulitokea katika jukwaa alilokuwa akihutubia.

“Ndugu mwandishi hii ni hujuma kabisa, mkutano ulifanyika kwa amani na utulivu wa kutosha, ghafla tukashangaa watu wanaanguka chini huku moshi mkubwa ukipaa juu,  sisi tulikuwa pembeni ya mti tukafikiri mwenyekiti wetu amepigwa bomu lakini haikuwa hivyo, yeye alishapanda gari na kuanza safari, watu wengi wameumia sana ndugu yangu,” alisema mfuasi huyo, Robert Kinabo.

Hadi tunakwenda mitamboni eneo lilipotokea mlipuko huo lilikuwa limezingirwa kwa alama ya tahadhari ya Jeshi la Polisi kwa ajili ya kuwasubiri wataalamu wa milipuko kutoka Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) kwa ajili ya kubaini aina ya mlipuko.
CHANZO TANZANIA DAIMA.


Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...