CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), kimeendelea kukipa wakati mgumu Chama cha Mapinduzi (CCM) katika siasa, ambapo kwenye matokeo ya udiwani katika uchaguzi uliofanyika leo, chama hicho kimefanikiwa kutetea kata zake na kunyakua nyingine za CCM.
Hata hivyo uchaguzi huo ambao ulifanyika kwenye kata 29 katika halmashauri mbalimbali nchini, umemalizika huku vurugu kubwa zikitawala na kusababisha wafuasi wa vyama hivyo kuumizana.
Hadi sasa matokeo ya kata 14 yanaonyesha kuwa CCM ilikuwa imefanikiwa kurejesha kata zake saba, huku CHADEMA ikinyakua kata sita,
ambapo mbili zilikuwa za kwao na nne imewanyang’anya CCM na CUF ikiwa na kata moja.
matokeo ya udiwani katika baadhi ya kata yalikuwa yakiendelea kutolewa huku CHADEMA ikiendelea kuikaba CCM kwa kuzitwaa baadhi ya zilizokuwa kata zake.
Jijini Arusha katika Kata ya Daraja Mbili, CCM ilipoteza kata hiyo kwa CHADEMA iliyozoa kura 2192 dhidi ya 1315 za chama tawala.
CHADEMA wameweza kuzirejesha kata zao mbili za Nangerea jimboni Rombo, ambapo mgombea wao Frank Sarakana alijizolea kura 2370 dhidi ya 1134 za Dysmas Silayo wa CCM pamoja na ile ya Mtibwa, mkoani Morogoro.
Wilayani Sikonge katika kata ya Ipole, CCM walipoteza kata hiyo kwa CHADEMA iliyopata kura 577 dhidi ya 372 za washindani wao, na vilevile kuitwaa kata nyingine ya Lengali wilayani Ludewa iliyokuwa ya CCM.
CHADEMA pia ilikuwa ikiongoza katika kata ya Mpwapwa, mkoani Dodoma, hadi tunakwenda mitamboni usiku.
Nayo CCM ilifurukuta kwa kuzirejesha kata zake za Msalato ya mkoani Dodoma, Bang’ata ya Arumeru Magharibi kwa kuwa 1177 dhidi ya 881 za CHADEMA, Mletele ya Songea CCM ilishinda kwa kura 950 na CHADEMA ilipata 295.
Pia CCM iliweza kutetea kata zake za Mwawaza mjini Shinyanga, Lwenzela mkoani Geita, Bungala wialayni Kahama na Bagamoyo mkoani Pwani kwa kuibwaga CHADEMA wakati Chama cha Wananchi (CUF) kilishinda kata ya Newala.
No comments:
Post a Comment