Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Mkoa wa Mjini Magharibi, Borafya Silima.
---
CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) Zanzibar
kimeitaka serikali ya Mapinduzi kuifuta mara moja Jumuiya ya Uamsho na
Mihadhara ya Kiislamu Zanzibar (JUMIKI) kwa kuwa inafanya kazi kinyume
na malengo yake usajili.
Kauli hiyo imetolewa jana katika mkutano
wa hadhara uliofanyika katika viwanja vya Mabata huko Magomeni Mjini
Unguja na kuhudhuriwa na wanachama wa CCM na wafuasi wa CUF ambapo mgeni
rasmi wa mkutano huo alikuwa ni Mwenyekiti wa Mkoa wa Mjini Magharibi
Borafya Silima.
Akizungumza katika mkutano huo Katibu wa
Vijana wa Mkoa wa Mjini Magharibi, Mohammed Ali Khalifa alisema chama
cha CCM kinamuomba msajili wa taasisi za kiraia achukue uamuzi wa
kuifuta jumuiya hiyo ya Uamsho ili isiwepo kabisa katika kumbukumbu za
asasi za kiraia hapa Zanzibar.
Alisema
taasisi hiyo haiendeshi shughuli zake za kidini licha ya kuwa
imesajiliwa kwa misingi ya kuendesha mambo ya dini lakini imepoteza
muelekeo na imekuwa ikifanya kazi za kisiasa jambo ambalo linakwenda
kinyume na malengo ya jumuiya hiyo.Aidha alisema Uamsho ina mkono wa watu
wakubwa ndani ya serikali na ndio muda wote imekuwa ukinyamaziwa na
hivyo kuitaka serikali kuwa macho na watendaji wake na kuwachukulia
hatua wale wote ambao wamehusika katika kuwaunga mkono na kuwakamta kwa
kuwafikisha katika vyombo vya sheria.
Kwa upande wake Mgeni rasmi wa mkutano
huo, Borafya Silima alisema jeshi la polisi limefanya kazi nzuri sana ya
kuhakikisha linawakamata wahalifu wote na kuwafikisha katika vyombo vya
sheria na kuwataka waendelee na kazi hiyo.
Borafya alisema haiwezekani viongozi wa
dini ambao hawana elimu kuachiwa kutamba na kuiharibu nchi kwa
kisingizio cha kutangaza dini wakati wanachokitangaza ni siasa huku
akikishutumu chama cha wananchi CUF kuwa kinahusika moja kwa moja na
vurugu zilizotokea kwa kuwabariki viongozi hao wa Uamsho.
“Mtu hana dini yenyewe haijui leo hii
tumwite sheikh kwani kuvaa kanzu ndio sheikh? Alihoji huku akishangiriwa
na wafuasi wa chama hicho.
Mwenyekiti huyo ambaye amechaguliwa hivi
karibuni amesema kwamba nafasi aliyopata ni muhimu katika siasa za
Zanzibar na kwamba ataitumia vizuri na kuwataka wapinzani wake wajipange
vizuri ili kukabiliana nao kwani wameingizwa madarakani kwa maridhiano.
Borafya alisema Maalim Seif amekuwa
amepewa wizara zisizo na uzito wowote serikali na hivyo amekuwa
akimuonea choyo makamo wa pili wa rais, Balozi Seif Ali Idd kwa kuwa
yeye ndio mshughulikiaji wa wizara zote za serikali.
Mazungumzaji katika mkutano huo ambao
kwa kiasi kikubwa wote waliohutubia walimlenga na kumshutumu moja kwa
moja Makamo wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Maalim Seif Sharif Hamad na
kumtaka aachie ngazi kwa kuwa ameshindwa kutekeleza yale ambao aliapa
kuyasimamia wakati akiingia madarakani.
Mbali na matusi ya nguoni na kumshutumu
kwamba anahusika na kundi la Uamsho walisema Maalim Seif hafai kuwa
kiongozi kutokana na kuwa mbinafsi kwa kuwa ameisema serikali yake mbele
ya viongozi wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Maendeleo (UNDP) kwa
kuwaeleza kwamba jeshi la polisi na vikosi vya SMZ vinahitaji mafunzo ya
kukabiliana na vurugu ili waweze kupata mafunzo ya kukabiliana na
vurugu hizo bila ya kuvunja haki za binaadamu.
“Huyu Maalim Seif anawaambia UNDP kwamba
jeshi letu la polisi linahitaji mafunzo ya kuwakamata wahalifu sisi
tunamwambia polisi wetu na vikosi vyetu havihitaji mafunzo wewe ndio
unahitaji mafunzo kwa sababu kwani wewe unalindwa na nani? Si hawa hawa
polisi” alisema Khalifa.
Katika hatua nyengine viongozi hao wa
CCM walimtaka Maalim Seif kuachia ngazi kwa kwa kumsema rais wake Dk
Shein hadharani kitendo ambacho walisema ni kwenda kinyume na kiapo
chake cha kuheshimu, kulinda na kutotoa siri za serikali.
Hivi karibuni katika mkutano wake Maalim
Seif alimtaka Rais wa Zanzibar Dk Ali Mohammed Shein kutekeleza ahadi
yake ya kuwalinda wananchi wote bila ya ubaguzi na kuhakikisha vyombo
vya ulinzi vinasitisha ukiukwaji wa haki za binaadamu kwa kuwa wananchi
wamechoshwa na ukandamizaji wanaofanyiwa katika nchi yao.
No comments:
Post a Comment