Baadhi ya wageni kutoka nchi mbalimbali za Bara la Afrika,
waliohudhuria mkutano huo leo, wakimsikiliza Makamu wa Rais, Dkt. Bilal.
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt.
Mohammed Gharib Bilal, akiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya
washiriki wa mkutano huo, baada ya ufunguzi.
Makamu wa Rais Dk. Mohammed Gharib Bilal amehimiza umuhimu wa
kujenga maelewano mazuri baina ya wafuasi wa dini mbalimbali,
vinginevyo, Bara la Afrika linaweza kushuhudia migogoro ya kidini kama
ilivyoanza kujitokeza huko Nigeria na hata hapa nchini.
Dk. Bilal ameyasema hayo leo katika ufunguzi wa mkutano wa pili wa
wanawazuoni wa Bara la Afrika uliofanyika katika ukumbi wa Karume, PTA
viwanja vya Sabasaba, Barabara ya Kilwa, jijini Dar es salaam.
Alielezea matumaini yake kuwa mkutano huo utayatafakari matukio
mbalimbali ya vurugu za kidini ambazo zimetokea hapa nchini hivi
karibuni kwa lengo la kuweka mustakabali mzuri wa kuishi kwa
kuheshimiana baina ya wafuasi wa dini kuu mbili za Kiislamu na Kikristo.
"Imani si ugomvi bali imani inapaswa itujenge kimaadili na moja
katika tunu za maadili ni kuishi vizuri na watu wengine hata kama si wa
imani yako," alibainisha
Makamu wa Rais alisisitiza umuhimu wa elimu ya mwongozo na ile ya
maarifa ya dunia kwa Waislamu na kusema itawawezesha kutatua matatizo
yanayowakabili wananchi yakiwemo ya uharibifu wa maadili, uasherati,
maambukizi ya virusi vya ukimwi, ukosefu wa ajira na unyanyasaji wa
kijinsia.
Alitoa changamoto kwa wanawazuoni wa Kiislamu na viongozi wengine
wa dini kuangalia ni jinsi gani utandawazi hautoathiri imani na maadili
ya waumini lakini pia ni jinsi gani waumini watanufaika na maendeleo
makubwa ya sayansi na teknolojia yaliyofikiwa na mwanadamu hivi sasa.
Malengo ya umoja huo wa wanawazuoni Barani Afrika ni pamoja na
kutilia nguvu masuala ya elimu, ushirikiano na kuheshimiana baina ya
jamii mbalimbali Barani Afrika.
Makamu wa Rais aliyaelezea malengo hayo ni mazuri na ya kujenga
ambayo kama yakiwekwa katika matendo, itaondoa ile picha hasi kuwa
waislamu ni watu wenye kufarakana, wasio na elimu, wasioheshimu dini za
wengine na wasiotambua nafasi na mchango wao katika maendeleo ya nchi
hizo.
Imetolewa na Ofisi ya Makamu wa Rais
Dar es salaam
No comments:
Post a Comment