CHAMA Cha
Mapinduzi(CCM), kimesema kuwa wananchi wa Mtwara wanayo hoja hivyo Serikali inatakiwa
kuwasikiliza na kutoa majibu sahihi.
Pamoja na
hayo chama hicho kimesema kuwa kinachoonekana hivi sasa nyuma ya sakata hilo
kuna watu wanafanya uhaini, uhalifu na kila aina ya hujumu jambo ambalo
wanaitaka Serikali kuchukua hatua kali za kuhakikisha wote wanojihusisha na
uhalifu huo wanachukuliwa hatua.
Kauli hiyo
ilitolewa jana mjini hapa na Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahaman Kinana ikiwa ni
msimamo wa chama chao katika sakata hilo.
Mjadala wa
gesi ya Mtwara kutoka mkoani humo kwenda Dar es Salaam umekuwa gumzo kubwa huku
wananchi wakiitaka Serikali kuwaeleza watanufaika vipi na gesi hiyo kabla ya
kunufaisha maeneo mengine.
Kinana
alisema kuwa kuna haja kwa Serikali kuhakikisha inatumia nafasi yake kuzungumza
na wananchi wa Mtwara katika kupata suluhu ya suala hilo kwani wana hoja za
msingi ambazo zinataka majibu.
“Msimamo
wetu kama chama, tunataka Serikali kukaa na wananchi hao na
kuwasikiliza.Tunahitaji kuona Serikali inatoa majibu ambayo yatakuwa sahihi na
kumaliza tofauti iliyopo sasa,”alisema Kinana.
Pamoja na
hayo alisema kuwa kinachoshangaza ni kuona hali ya uvunjifu wa amani
inayofanywa na baadhi ya watu ambao wameamua kuingia mtaani na kuiba, kupora
mali na kuharibu nyumba za watu kwa kuzichoma moto.
Alisema
kuwa CCM inaona ni wakati mzuri kwa Serikali kuwadhibiti wote ambao wanatumia
mwanya huo kufanya uhalifu huo ambao haukubaliki huku akisisitiza umuhimu wa
wananchi kusikilizwa.
Alisema
mtazamo wa chama chao ni kwamba kuna jambo ndani ya suala hilo maana gesi
inatakiwa kujadiliwa kwa njia ya amani kupata suluhu kuliko mali za watu
kuharibiwa na kufanywa kwa uhalifu ambao hauvumiliki.
No comments:
Post a Comment