Na: Albert Sanga
Ninafahamu
kuwa linapokuja suala la matumizi ya lugha ya Kiswahili katika mambo ya
biashara na ujasiriamali-akili zetu zinapwaya. Sio kwa sababu Kiswahili
hakina maneno yote ya kibiashara, la hasha! Lakini ni kwa sababu
hatujazoea biashara kwa hiyo misamiati haijatukaa sana kama ilivyotukaa
ile ya kisiasa. Moja ya neno hilo ambalo nimeamua kulikopa kama lilivyo
ni “Risks”; na ndio dhana nitakayoijadili leo
Kiukweli
ujasiriamali unahitaji mtu kuwa na roho ya paka (roho ngumu na ya
uvumilivu mkubwa). Leo kupata faida na kesho hasara ama....
kufilisika kabisa ni mambo ya kawaida sana. Wajasiriamali wengi tuna tatizo katika utunzaji na ukuzaji wa mitaji.
Yaani,
mitaji inapanda na kushuka. Mtu unaweza kufanya biashara na kufikisha
pengine mtaji wa milioni ishirini lakini baada ya muda fulani unashangaa
mtaji unasoma milioni kumi. Inakuwa kama mchezo wa kubahatisha (kupata
ama kukosa). Wakati mwingine wajasiriamali tunaishi maisha ya misongo
mikubwa kimawazo kutokana na mambo kwenda npyo sivyo. Unaweza kuchukua
mkopo benki halafu biashara ulizotegemea zikakataa.
Ikiwa
uliwekea dhamana ya nyumba ama rasilimali nyingine lazima jasho lianze
kukutoka. Ama wakati mwingine unaweza kufanikisha kulipa mkopo lakini
ukajikuta mtaji haujaongezeka na pengine umeshuka; inakuwa kama ulikuwa
unawafanyia kazi benki!
Uzoefu
unaonesha kuwa usipokuwa makini katika ufanyaji wa ujasiriamali,
unaweza kushindwa hata kumudu ndoa yako (kwa wale waliooa ama kuolewa).
Kufanikiwa kibiashara inatakiwa kuendane na furaha katika familia na
ustawi wa afya ya mwili wako. Unatakiwa kuwa na fedha ya kutosha pamoja
na muda wa kutosha kupumzika ama kukaa na familia yako.
Kinachosikitisha
ni kuwa wajasiriamali wengi wanakuwa na fedha (hata kama si nyingi za
kutosha), lakini hawana muda wa kufurahi na familia wala ndoa zao. Hata
wanapokuwa katika nyumba zao akili zao haziwi na wake zao, haziwi na
watoto wao, zipo kwenye ujasiriamali ama zinawaza marejesho ya mikopo!
Wajasiriamali wengi hawajui ni lini hasa watakuwa na furaha za kudumu.
Kuwa na furaha katika maisha yao ni kama bahati nasibu!
Kupanda
na kushuka kimafanikio, kuishi na vidonda vya tumbo ama presha
kunakotokana na mawazo; pamoja na migogoro ya kifamilia sio stahili ya
mjasiriamali na katu haifai kuwa hivyo. Pamoja na hayo, mazingira ya
ujasiriamali tuliouzoea Tanzania yanatupelekea kuwa katika hali hizi,
Je, tunajikwamuaje hapa?
Ili
kuepuakana na hali kama hizi za ujasiriamali kuwa kama mchezo wa
kubahatisha kuna mtindo wa ufanyaji wa biashara ambao wajasiriamali
tunatakiwa kuuzoelea. Mtindo huu ni kuwekeza katika aina tofauti za
biashara kwa wakati mmoja.
Kwa
kitaalamu mtindo huu tunauita ‘persification’ ambapo zile biashara
mbalimbali unakowekeza zinaitwa ‘portofolio’. Kufanya ‘persification’
kunaondoa kubahatisha katika kupata faida kunapunguza msongo wa mawazo
na kunakupa furaha ya ujasiriamali muda wote.
Kwa
mfano, badala ya kuhangaika na biashara ya mbao pekee, ambayo ina
mtindo wa kupanda na kushuka (kutegemea na msimu), ni vema mjasiriamali
ukawekeza katika biashara zingine kama, majengo, usafirishaji na
nyingine unazoweza kuzimudu. Kanuni itakayokusaidia katika
‘persification’ ni kuhakikisha biashara unazowekeza zisiwe na kufanana
ama kutegemeana.
Ipo
hivi, ukiwa ni mfanyabiashara wa mazao, ‘persification’ haitakuwa na
tija kubwa kama utawekeza katika usafirishaji kwa kununua lori. Shida
itakuwa ni moja, biashara zako zote mbili (ya mazao na usafirishaji)
zitakuwa ni za msimu; msimu wa mazao ukiisha na biashara ya usafirishaji
itasimama. (ikiwa lori hilo hukodishwa kusafirisha mazao)
Ndio
maana ninasema katika kufanya hiki ninachokiita, ‘persification’
mjasiriamali unatakiwa kutafuta biashara ambazo angalau moja inapoenda
vibaya basi nyingine iwe inazalisha faida. Ukianza na kujizoesha
kufanya, ‘persification’ haimaanishi kuwa hautapita katika changamoto za
kuyumba, lakini nakuthibitishia kuwa hautakuwa mtu wa kuyumba kiasi cha
kufika sifuri.
Najua
kuwa kuna watu watawaza mioyoni mwao mambo mengi kuhusu hii
‘persification’. Unaweza kuniuliza, “Nitafanyaje biashara zaidi ya moja
na mtaji unanikaba?” ama pengine unaweza kujisemea, “Biashara zaidi ya
moja nitasimamiaje?” Kuhusu la usimamizi nitalieleza katika makala
zijazo, lakini hili la mtaji ni rahisi.
Usisubiri
kuwa na mtaji mkubwa ili ufanye ‘persification’. Pale ulipo angalia ni
biashara aina gani tofauti unaweza kuzifanya kwa wakati mmoja? Kwa
mfano, unaweza kuwa na mgahawa wenye mtaji wa laki tatu halafu ukawa na
saluni yenye mtaji wa laki tano, tayari hii ni ‘persification’.
Hata
katika mambo ya mikopo, huwa inakuwa rahisi kwa mjasiriamali kurejesha
mkopo kwa wakati ikiwa una biashara zaidi ya moja (za aina tofauti).
Kuna wakati itatokea, biashara uliyochukulia mkopo ikagoma, lakini
ukaweza kurejesha mkopo kupitia biashara nyingine. Lakini ukiacha hilo,
mjasiriamali unakuwa na maisha yasiyo na mawazo ya kuumiza na unakuwa na
uhakika kwa yale unayoyafanya.
Tatizo
la wajasiriamali wengi ni ubishi wa kung’ang’ania biashara moja miaka
nenda rudi pamoja na kuigana. Biashara iliyokufaidisha jana sio lazima
ikupe faida leo. Biashara inayompa faida mwenzio haimaanishi ukianzisha
na wewe utapata faida.
Mazingira
yanabadilika, ushindani unaongezeka, hivyo ni lazima kukabili
changamoto mpya na kuwa tayari kujaribu biashara mpya. Hili litasaidia
sana mjasiriamali kuwa na uhakika kwa biashara zako na kuepuka maisha ya
kubahatisha kiujasiriamali! Tuonane wakati ujao.
Wajasiriamali wote tunahitaji ushindi!
No comments:
Post a Comment