Na Boniface Meena
(email the author)
WABUNGE vijana katika Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,
wameanza kujiandikisha tayari kwa kujiunga na Jeshi la Kujenga Taifa
(JKT) kwa Mujibu wa Sheria kwa ajili ya mafunzo yatakayoanza Machi mwaka
huu.
Taarifa ambazo Mwananchi Jumamosi ilizipata juzi,
zimeeleza kuwa, idadi ya wabunge ambao tayari wamejiandikisha kujiunga
na JKT hadi sasa ni zaidi ya 31, huku wengine wakiendelea.
Kujiandikisha kwa wabunge hao ili wajiunge na JKT
kunafuatia wito uliotolewa na Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga
Taifa, Shamsi Vuai Nahodha, Julai mwaka uliopita, alipowasilisha hotuba
ya bajeti ya wizara yake katika Bunge la Bajeti mjini Dodoma.
Kwa nyakati tofauti wabunge vijana kutoka CCM,
Chadema na NCCR- Mageuzi walilithibitishia gazeti hili kuwa tayari
wamejiandikisha katika Ofisi ya Katibu wa Bunge kwa ajili ya mafunzo
hayo.
Imebainishwa kuwa, miongoni mwa wabunge
waliojiandikisha, wamo pia ambao waliwahi kupitia mafunzo hayo,
ikielezwa kuwa wamefanya hivyo wakitaka kwenda kujikumbushia.
Hata hivyo, Kaimu Katibu wa Bunge, Eliakimu Mrema
hakuwa tayari kuzungumzia suala hilo akieleza kuwa linaweza kuzungumziwa
na Spika wa Bunge kwa kuwa ndiye anayezungumzia masuala ya wabunge.
“Sisi kazi yetu ni utendaji tu na masuala ya wabunge, Spika ndiye anayezungumzia,”alisema Mrema.
Alipotakiwa kuzungumzia taarifa hizo, Naibu Spika
wa Bunge, Job Ndugai, alisema kwamba ni mapema mno kuzungumzia suala
hilo kwa kuwa hawajapata idadi kamili.
“Tukiwa Dodoma (bungeni), ukituuliza tutakuwa
tayari kutoa taarifa kamili, lakini kwa sasa ni mapema kuzungumzia suala
hilo,”alisema Ndugai na kuongeza:
“Watu ni rahisi kusema, lakini wakati mwingine
utekelezaji ni mgumu kama unavyosema kwani, ukisikia moja ya uamuzi
mgumu, hili ni mojawapo.”
Ndugai alisema kuwa mafunzo hayo hayatawahusu
wabunge ambao waliwahi kupitia JKT siku za nyuma na kwamba ni maalumu
kwa wabunge vijana.
“Naomba usubiri Dodoma, tutakuambia hali ilivyo,” alisema Ndugai.
No comments:
Post a Comment