Wageni waalikwa wakibadilishana mawazo kabla ya kupata chakula cha jioni nyumbani kwa Balozi wetu Uingereza.
Mheshimiwa Balozi Peter Kallaghe akiinua kinywaji (“cheers”) na wageni kabla ya kumkaribisha mgeni kuongea.
Mheshimiwa Balozi Dianna Melrose akiongelea machache. Kushoto kwake ni Balozi wetu Uingereza, Mheshimiwa Peter Kallaghe.
Balozi Dianna Melrose akitia saini kitabu cha wageni. Kushoto ni Mama Balozi Joyce Kallaghe.
Mheshimiwa Balozi Dianna Melrose akifanya mahojiano na wanahabari Freddy Macha na Urban Pulse.
Mheshimiwa Balozi Dianna Melrose (katikati) na Balozi Peter Kallaghe na Mama Balozi Joyce Kallaghe.
-Imeandikwa na Freddy Macha
-Picha za Urban Pulse
Balozi
mpya wa Uingereza nchini Tanzania, Mheshimiwa Dianna Melrose ameeleza
furaha yake kuteuliwa kufanya kazi nchini kwetu na kukiri kwamba
anauchangamkia wadhifa huo atakaouanza karibuni.
Balozi
Melrose alikuwa akiongea katika sherehe ya chakula cha jioni
iliyofanywa kwa heshima yake nyumbani kwa Balozi wetu wa Uingereza
mheshimiwa Peter Kallaghe na mkewe Joyce Kallaghe jijini London Alhamisi
iliyopita.
“Nimebahatika
sana.” Alikiri Mama Melrose. “ Watanzania ambao nimekutana nao wana
hulka ya kirafiki na uungwana sana. Ni watu wenye tabia njema na
ninahisi nitafurahia sana maisha yangu kwenu. Nitafurahia kwa sababu
wenzangu walioshaishi Tanzania muda mrefu wamebakia na mapenzi makubwa
ambayo sijayaona kwa Waingereza walioishi nchi nyingine. Wamebakia na
kumbukumbu nzuri na mahusiano ya muda mrefu na Tanzania.”
Balozi aliendelea kufafanua kwamba Tanzania inasonga mbele na ni taifa muhimu kwa Uingereza ambaye ni mwekezaji wake mkuu.
“Wakati
Balozi Diane Corner aliyenitangulia, alipokutana na Rais Kikwete ,
Rais alihimiza kwamba mahusiano ya serikali zetu mbili yamefikia
mapatano ya juu sana. Hivyo jukumu langu litakua kuimarisha muungano
huu.”
Balozi Diane Corner aliyeshika kiti hicho toka 2009 hadi 2013 amehamishiwa Jamhuri ya Kidemokrasia Kongo.
Hafla
hii ndogo pia ilihudhuriwa na Afisa Ubalozi wa daraja la pili, Allen
Kuzilwa( anayehusika na mahusiano ya kimataifa ya ufadhili wa
kimaendeleo na elimu ).
Balozi
Melrose mwenye uzoefu mkubwa katika shughuli za ujenzi jamii na
mahusiano ya kimataifa alikuwa balozi wa Uingereza nchini Cuba toka 2008
hadi 2012.
Mwanadiplomasia
huyu ambaye ni mtaalamu wa lugha za Kifaransa na Kispanyola keshaanza
kujifunza Kiswahili na alijaribu kuthibitisha maneno machache
aliyoshayanyasua.
Akiwa
kijana alifanya kazi shirika linalopambana na umaskini na kupigania
haki duniani, Oxfam, mwaka 1980. Oxfam linalohudumia nchi 90 duniani
lilianzishwa Uingereza mwaka 1942 mjini Oxford.Melrose alizaliwa
Zimbabwe mwaka 1952 akamaliza masomo ya shahada ya kwanza ya lugha- kwa
alama za juu (“Honours”) chuo kikuu cha Kings College, London.
Akimkaribisha, Mheshimiwa Balozi Kallaghe alikumbusha kwamba kwenda
Tanzania itakuwa changamoto kubwa maana taifa letu linapitia
mabadiliko makubwa hasa kutoka kwa vijana, majadiliano ya katiba mpya
na hali ya Afrika yenye matukio muhimu sasa hivi.
Mabalozi
wengine waliohudhuria ni waheshimiwa Ernest Rwamucyo (Rwanda), Nkwelle
Ekaney (Cameroon), na balozi wa zamani Canada (aliyeshastaafu), Antony
Carey na mkewe Claire. Vile vile mwakilishi wa Tanzania Standard
Chartered Bank, Uingereza, Rweyunga Kazaura, wanachama wa Jumuiya ya
Watanzania na Waingereza (BTS) Ron Fennel , mkewe Liz, mhariri wa jarida
la Tanzanian Affairs, David Brewin na mfanya biashara wa Kitanzania
London (Swift Freight) Bwana Abubakar Faraji.
No comments:
Post a Comment