Na: Albert Sanga
Miaka
ya hivi karibuni dhana inayohusu ujasiriamali imeenea kwa kasi kubwa
sana miongoni mwa wana jamii. Kwa sasa kila kona tunasikia
ujasiriamali, makanisani , mitaani, vyuoni na katika mikutano ya kisiasa
kunahubiriwa ujasiriamali. Hata hivyo kuna kibwagizo kinajirudia kila
zinapotajwa changamoto za ujasiriamali; ukosefu wa mitaji!. Dhana ya
ujasiriamali imepata kushika kasi kutokana na nchi yetu kujikuta
inajisalimisha katika mfumo wa kibepari pasipo kupenda wala kutoa
taarifa. Utandawazi umeyasababishia mataifa masikini kama Tanzania
kurukia ubepari bila kuagana na...
nyonga zao. Nyonga ninazomaanisha hapa ni mifumo ya kiuchumi
iliyokuwepo nap engine iliyobuniwa na wazalendo wa mataifa husika;
Tanzania tukiwa na ujamaa wetu ulioasisiwa na mwalimu Julius Nyerere.
Inafaa
sana watanzania wote kufahamu kuwa maisha ni magumu. Na ugumu wa
maisha haujaanza jana wala miaka ya karibuni, bali tangu uwepo wa dunia
hii maisha ni magumu. Wengi huwa hawataki kuukubali ukweli huu ‘kama
ulivyo’.
Ndio
maana utawasikia wakihuzuniaka, kung’ung’unika na kulalamika, kana
kwamba waliambiwa maisha ni rahisi. Saa unapoukubali ukweli ya kuwa
maisha ni magumu, ndio wakati ambao maisha hayawi magumu tena! Ndio! Kwa
sababu ukijua maisha ni magumu ni lazima utaishi kwa nidhamu kubwa, na
nidhamu ndio msingi namba moja wa kutatua matatizo yote katika maisha.
Ukiwa
na nidhamu kidogo utatatua matatizo machache, na ukiwa na nidhamu
nyingi utatatua matatizo mengi! Nidhamu inahusisha kufanya kazi kwa
bidii, kuwapenda na kuwafikiria wengine, kuheshimu sheria za nchi na
kila namna ya jema unalolijua.
Ukiona
unalalamika kuwa maisha ni magumu, rejea katika fikra zako, huenda bado
hakujafanyika mapinduzi! Ukiona unaukubali ukweli ya kuwa maisha ni
magumu na wakati huo huo huna nidhamu ama una nidhamu chache, basi ujue
kuwa hujaukubali ukweli wote wa maisha kuwa ni magumu, !
Ujasiriamali
unawagusa watu wa kada na umri mbalimbali, vijana wazee na hata watoto.
Kwa kuwa kundi la vijana [wasomi na wasio wasomi] ndio linaloongoza
sana kwa kutegemewa kwa uzalishaji nitaongelea hilo. Ujasiriamali kwa
ujumla ni dhana ambayo ili kukubalika kikamilifu kunahitajika mapinduzi
makubwa sana ya fikra kwa vijana kuliko elimu ya kawaida. Fikra za
kuwatazama wajasiriamali waliofanikiwa na kutoa visingizio kuhusu
mafanikio yao ni fikra zenye matege na ukilema na hizo kamwe haziwezi
kutufanya tukafanikisha kujikwamua kiuchumi.
Vijana
ambao hawana elimu wanalalamika kuwa hawana elimu ndio maana maisha yao
ni magumu ama yanasumbua, nao vijana ambao wanaelimu katika fani na
viwango mbalimbali wanalalamika kuwa ajira hamna. Unapogusia suala la
ujasiriamali katika kundi hili la vijana wenye elimu, utakisikia kilio
ambacho kimekuwa kama wimbo sasa nacho ni “ukosefu wa mitaji”. Kwa ufupi
ni kuwa vijana wenye elimu wanalia kutokana na ugumu wa maisha na vile
vile vijana wasio na elimu wanalia. Wasio na elimu wanawatamani wenye
elimu, na wenye elimu wanaitamani mitaji.
Kutokana
na hali hii utagundua kuwa tatizo linaliwakabili vijana wengi wa
Tanzania katika kujikwamua kiuchumi sio mitaji wala ukosefu wa elimu
bali kuna tatizo la kifikra hapa. Ili kijana aweze kufanikiwa kubuni na
kuanzisha mradi anatakiwa aamini kuwa kujiajiri kuna tija kubwa sawa
sawa na kuajiriwa. Kwa sababu ni mara chache sana mtu anaweza kuwa
tajiri kwa kutegemea mshahara wake!
Kwa
bahati mbaya katika jamii kuna utamaduni uliojengeka sana katika jamii
zetu wa kuamini sana kuajiriwa. Hata familia nyingi zinaposomesha watoto
wao zinawasisitiza wasome kwa bidii ili wafaulu na kupata kazi zenye
mishahara mikubwa. Utamaduni huu umefifisha hamasa na moyo wa kupenda
kujiajiri miongoni mwa vijana wetu hasa waliopo katika mifumo ya
kielimu..
Hebu
tumtafakari kijana anayesema kuwa amekosa mtaji ndio maana ni masikini.
Ni dhahiri kuwa wengi wa vijana mara kwa mara huwa wanabahatika kupata,
shilingi elfu ishirini mifukoni mwao. Kijana akitumia ubunifu, kwa
mfano anaweza kununua kuku wawili wa kienyejji wa kufugwa, kila mmoja
shilingi elfu saba, jumla wawili ni elfu kumi na nne.
Hawa
wakifugwa kwa miezi mine wanaweza kutotoa kuku kumi. Baada ya mwaka
mmoja kuku wanaweza kufikia sitini! Kuku sitini ukiwauza kwa shilingi
elfu saba kila mmoja anakuwa na zaidi ya laki nne. Tayari huyu anakuwa
ameanza safari ya kujikwamua na umasikini!
Vijana
wa Tanzania ambao wanapambana na ugumu wa maisha wanahitaji sana
kupokea semina, shuhuda na uzoefu kutoka kwa wajasiriamali wa kitanzania
ambao wamefanikiwa. Kama semina, warsha na makongamano yatakuwa
yakitumia dhana pekee za vitabuni tutarudi kule kule katika mfumo
tegemezi, ambao unaonekana sio halisi bali ni wa kujibia mitihani.
Tunawahitaji wajasiriamali vijana kuandika vitabu vinavyoeleza namna
walivyofanikiwa ili kutia hamasa na kubadilisha fikra za vijana wengine
ambao wanasua sua kujikita katika ujasiriamali kwa visingizio vya kukosa
elimu na kukosa mitaji.
Ujasiriamali
unahusisha kujenga fikra madhubuti za kujitegemea na kutegemewa. Kwanza
ni kuwa akili ya mtu inapanuka na kuwaza zaidi na zaidi kutegemea na
mahitaji yaliyopo katika fikra. Ukiwaza kupata fedha kidogo ya kujikimu
ubunifu wa akili yako utajikita katika upatikanaji wa fedha hiyo kidogo!
Ukiwaza kuwa na fedha nyingi akili yako inapanuka kuwaza namna ya
kupata fedha nyingi. Lengo langu hapa si kusisitiza vijana kuwa na fedha
nyingi, isipokuwa ni kuweka hamasa kwa vijana kuhusu ujasiriamali na
namna ya kujikwamua kiuchumi.
Ni
vema vijana wote wafahamu ya kuwa “fedha ni mawazo”. Kama fedha ni
mawazo basi kujikwamua kiuchumi ni mawazo pia. Kama ni suala la kuwaza,
kwa nini asiye na elimu asiwaze? Kama ujasiriamali unaanza na mawazo,
kwa nini wenye elimu walilie mitaji? Sikatai kuwa mitaji ni suala la
msingi katika ujasiriamali, lakini ifahamike kuwa uthubutu wa kuanza na
kujaribu wazo hata kwa sehemu ndogo ndio msingi wa mafanikio ya
mjasiriamali yeyote.
Nchi
ya Tanzania ina ajira na fursa nyingi sana za kiuchumi za kumtosha hata
mtoto atakayezaliwa kesho! Sioni sababu ya muhitimu wa darasa la saba
kukosa ajira, kwa nini muhitimu wa kidato cha nne na sita wakose kitu
cha kufanya chenye kuwakwamua kiuchumi katika nchi tajiri kama Tanzania?
Kwa wale ambao ni wahitimu wa vyuo vya kati na vya elimu ya juu sioni
haja ya kuwaandikia kwa sababu inatosha sana kwao kutengeneza ajira kwa
wengine.
Tatizo
jingine linalowasibu vijana wengi wa Tanzania hata wanashindwa kupoka
(Seizing) fursa za kijasiriamali na fikra potofu za kutaka kuanza na
mafanikio. Kama ni kijana msomi anawaza kuanza na kampuni lenye mtaji wa
mamilioni. Yatatoka wapi mamilioni bila kuanza na kudogo? Kwa wale
ambao hawana elimu kubwa wengi wamevia kimawazo kwa kuota kuokota fedha
ama kuokota elimu.
Kama
ulikosa elimu haupaswi kulalamika wala kung’ung’unika kwa sababu huko
ni kupoteza muda bado unayo nafasi kubwa sana ya kufanikiwa. Fikra za
kupata vya bure bila kuhangaika ndio zinapelekea watanzania wengi
kujiingiza katika michezo mingi ya ‘kibahati nasibu’ kwa matarajio kuwa
watatoka! Cha ajabu ni kuwa michezo mingi inayohusu bahati nasibu ama
mingineyo inawapotezea fedha badala ya kuwasaidia, hapa yanahitajika
mapinduzi ya kifikra.
Maisha
bora na ya uhakika kwa vijana yanawezekana sana ikiwa kutafanyika
mageuzi makubwa katika sekta binafsi, ujasiriamali. Na ili ujasiriamali
ufanikiwe na kufanywa na vijana kwa uhakika ni lazima vijana wote
wakubali kufanya mapinduzi ya fikra zao za kitegemezi. Tukisema
ujasiriamali hatumaanishi ujasiriamali wa kujikwamua wewe kijana peke
yako, bali tunagusa pia katika utanuzi wa fikra za kuanzisha makampuni,
huduma na bidhaa mbalimbali zenye ubunifu mpya kwa kuvitumia vipaji
kikamilifu
Watanzania tunahitaji ushindi wa kiujasiriamali!
http://make-it-simply-easy-life.com/
ReplyDelete