KONDOMU zinazodaiwa kuwa ni bandia ambazo
zilipigwa marufuku nchini Uingereza kutokana na kubainika kuwa hazina
ubora unaotakiwa, zimetapakaa katika maduka mbalimbali ya dawa nchini,
Mwananchi limebaini.
Kondomu hizo ni Durex na Trojan ambazo zina vipele
na uchunguzi uliofanywa na gazeti hili umebaini kuwa zinauzwa katika
maduka mbalimbali ya dawa kwa bei ya Sh5,000.
Mwishoni mwa mwaka jana, Serikali ya Uingereza
ilifanya msako mkali kwa lengo la kukamata mamilioni ya kondomu hizo,
wakati ambao ilikuwa imepita takriban miezi 18 tangu zilipokuwa
zimeingizwa nchini humo.
Mdhibiti wa Dawa na Bidhaa za Afya wa Uingereza
alinukuliwa akisema kuwa mamilioni ya kondomu hizo feki ziliingizwa
kutokea Mashariki ya Mbali na kwamba tayari zilikuwa zimetumiwa na idadi
kubwa ya watu.
Kondomu hizo zinadaiwa kutokuwa na ubora hali
inayoweza kuongeza hatari kwa watumiaji kwa kusambaza kwa kasi magonjwa
ya zinaa, virusi vya Ukimwi au kusababisha mimba zisizohitajika, hivyo
kuharibu mikakati ya uzazi wa mpango.
Ofisa Habari wa Mamlaka ya Chakula na Dawa
Tanzania (TFDA), Gaudensia Simwanza akizungumza na gazeti hili jana,
alithibitisha kuwapo kwa taarifa za kondomu hizo za Durex na Trojan na
kuongeza kuwa mamlaka hiyo imewaagiza wakaguzi wake kuzichunguza ili
kubaini kama zina ubora ama la.
“Wakaguzi walichukua sampuli ya kondomu hizo kwa
lengo la kuzichunguza, nipe muda kidogo ili nizungumze na mkurugenzi ili
kujua uchunguzi ule umefikia wapi,” alisema Simwanza.
Alipotafutwa baadaye alibainisha kwamba uchunguzi
wa sampuli hiyo bado upo maabara na kwamba majibu yake hayajatoka. Hata
hivyo hakusema ni lini yatatolewa.
Kwa upande wake, Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Shirika
la Viwango Tanzania (TBS), Leandri Kinabo aliomba apewe muda ili
afuatilie kujua ni kondomu za aina gani zilizowahi kukamatwa na kupigwa
marufuku zisitumike.
“Nipe muda kidogo nifuatilie ili kujua zilizopigwa
marufuku na ambazo tulizizuia kuingizwa nchini, nitafute mchana,”
alisema Kinabo ambaye alipotafutwa baadaye alisema yuko kwenye kikao na
kwamba alikuwa hajaweza kuwasiliana na watu wa maabara.
Hii siyo mara ya kwanza kuibuliwa kwa taarifa za
kuwapo kwa kondomu feki nchini, kwani Desemba 20, mwaka jana kontena
lililosheheni kondomu za kiume aina ya Melt Me kutoka nchini India
lilikamatwa na kuzuiwa katika Bandari ya Dar es Salaam, baada ya
kubainika kuwa hazifai kwa matumizi.
Maofisa wa TBS walilazimika kufanya msako katika
baadhi ya maduka ya dawa jijini Dar es Salaam ikiwa ni hatua ya
kuziondoa kondomu hizo katika soko.
No comments:
Post a Comment