ADV

ADV

ADVERTISEMENT CORNER

HUDUMA YA KUKATA TICKET ZA NDEGE ONLINE


SOMA HABARI

SOMA HABARI

Thursday, February 21, 2013

Vigogo watema cheche



 MWANANCHI
Akizungumza na waandishi wa habari jana, Lowassa alisema matokeo hayo ni aibu kwa taifa na kuilaumu Serikali kwa kuzitelekeza shule za sekondari za kata.Alisema taifa kwa sasa linazalisha wabeba kuni na maji na siyo wasomi ambao wanaweza kushindana kwenye soko la ajira.

WAKATI Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa akiinyooshea kidole Serikali kwa kuzitelekeza shule za sekondari za kata, Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Dk Shukuru Kawambwa amesema hatajiuzulu ng’o kutokana na matokeo mabaya ya kidato cha nne. Baraza la Vijana la Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Bavicha), nalo limetishia kuitisha maandamano ya nchi nzima kwa kushirikisha wanafunzi wote waliopata sifuri ikiwa waziri huyo hatajiuzulu. Taifa limeshikwa na mshtuko kutokana na matokeo hayo ambayo yanaonyesha kuwa asilimia 60 ya wanafunzi waliofanya mtihani huo mwaka jana, walipata sifuri.
Dk Kawambwa
Akizungumza jana katika uzinduzi wa Mpango Maalumu wa Mafunzo ya Kompyuta katika Shule ya Msingi ya Majengo wilayani Bagamoyo, Dk Kawambwa alisema hawezi kuachia ngazi kwa shinikizo la
wanasiasa.

Alisema yeye si wa kulaumiwa kutokana na wanafunzi hao kufanya vibaya kwenye mtihani wa kidato cha nne na kwamba wanaosema waziri anapaswa kujiuzulu hawana hoja za msingi zaidi ya kutaka kujipatia umaarufu kwa kudandia hoja zinazokuwapo kwa wakati husika.
“Unajua katika mfumo wa vyama vingi, kila linapotokea jambo baya basi wanaona dawa ni kiongozi mhusika kung’oka. Unapozungumza waziri kujiuzulu hiyo ni lugha ya kisiasa lakini hata akijiuzulu inakuwa bado tatizo halijaweza kupatiwa ufumbuzi,” alisema.

Dk Kawambwa alisema hata Serikali haijafurahishwa na matokeo hayo mabaya na kushauri njia nzuri ni kutafuta dawa ya kukabiliana na tatizo la wanafunzi kufeli huku akiahidi kuwa wizara yake inaangalia tatizo hilo kwa karibu zaidi ili kujua chanzo chake.

Alisema amesikitika kuona hata shule ambazo zilikuwa zinategemewa kufanya vizuri zikiwamo za seminari, watu binafsi na kongwe za Serikali, nazo zimefanya vibaya.
Aliunga mkono maoni ya kutaka mfumo mzima wa elimu nchini uangaliwe upya kwa kushirikisha wadau mbalimbali wa elimu.
Lowassa
Akizungumza na waandishi wa habari jana, Lowassa alisema matokeo hayo ni aibu kwa taifa na kuilaumu Serikali kwa kuzitelekeza shule za sekondari za kata.
Alisema taifa kwa sasa linazalisha wabeba kuni na maji na siyo wasomi ambao wanaweza kushindana kwenye soko la ajira.

Alisema sekondari za kata ambazo zilianzishwa chini ya usimamizi wake akiwa Waziri Mkuu, zilikuwa ukombozi kwa Watanzania wengi wa kipato cha kawaida na ndiyo sababu waliitikia wito kwa kuchangia ujenzi, hatua ambayo alisema ilimpa faraja kubwa.

“Serikali tuliahidi kuzikamilisha shule hizo kwa kuzijengea maabara na kuhakikisha zina walimu. Ni wajibu wake kutimiza. Mimi ndiyo maana hata kwenye Katiba Mpya nilipendekeza uwezekano wa elimu ya sekondari kuwa bure, elimu ni kama mapigo ya moyo ya taifa ukiona hayaendi vyema lazima ujiulize,” alisema.

Lowassa, ambaye alijiuzulu uwaziri mkuu mwaka 2008, alisema tangu aondoke madarakani, shule hizo nazo zimetelekezwa.

Alimwomba Rais Jakaya Kikwete kuchukua hatua za makusudi, ikiwa ni pamoja na kuunda tume ili ichunguze kwa makini kiini cha matokeo hayo mabaya.

“Matokeo hayo ni aibu kwa taifa, walimu, wazazi na wanafunzi wenyewe. Namwomba kwa dhati Rais afanye kitu cha ziada, natambua mchango wa juhudi zake katika sekta nyingine ikiwamo ujenzi wa barabara nchini lakini elimu ndiyo iwe ya kwanza,” alisema.

Alitaka ufike wakati nchi iamue kuwekeza katika elimu tofauti na ilivyo sasa kwa Tanzania kuwa nchi inayotenga fedha kidogo zaidi katika sekta hiyo katika Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC).

No comments:

Post a Comment

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...