Lwakatare na Ludovic |
SASA kuna kila dalili
zinazoonyesha kuwa faili la mtuhumiwa namba mbili katika kesi ya ugaidi
iliyofunguliwa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Ludovick Joseph, limeyeyuka
baada ya Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kinondoni, Charles Kenyella, kudai kuwa
hajaliona.
Dalili hizo zilianza
tangu wiki iliyopita, wakati MTANZANIA Jumapili lilipoanza kufuatilia taarifa za
kuwepo kwa utata wa tukio zima la kutekwa kwa Ludovick pamoja na utata wa
taarifa alizodai kuzitoa katika Kituo kidogo cha Polisi
Kigogo.
MTANZANIA
Jumapili lilianza uchunguzi wa taarifa hizo na wiki iliyopita likiripoti kwa
kina utata huo kwa kuweka wazi mkakati wa kumshitaki Ludovick kuwa ni mpango
mahususi unaodaiwa kuratibiwa na Serikali kufichua njama za kigaidi, ambazo
zinadaiwa kutekelezwa na baadhi ya viongozi wa kisiasa.
Hata hivyo, Polisi
wamekuwa wakishindwa kuthibitisha taarifa hizo za kutekwa kwa Ludovick, ikiwa ni
pamoja na kushindwa kutoa RB namba ambayo Ludovick alidai kuifungua katika kituo
cha polisi cha Kigogo.
Kamanda wa Polisi Mkoa
wa Kinondoni, Charles Kenyela, ambaye alitupiwa mpira huo kutoka kwa maofisa wa
chini yake kuwa ndiye anayeweza kutoa taarifa kamili kuhusiana na tukio hilo la
Ludovick, ikiwemo pia namba ya RB, mara kadhaa ameshindwa kufanya
hivyo.
Gazeti hili lilifika
ofisini kwake, lakini hakuweza kupatikana na kuambiwa kuwa yuko katika harakati
za sherehe za miaka 49 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar, lakini
alipotafutwa kwa namba yake ya simu alisema kuwa bado hajafanikiwa kupata RB
hiyo.
Kamanda Kenyela
alipoulizwa kuwa imekuwa ni muda mrefu tangu aseme kuwa anafuatilia taarifa hizo
na hakuna majibu ya kuridhisha, bado aliomba apewe
muda.
“Naomba muda bado
sijaipata, ni siku nyingi ...lakini ndiyo shughuli yenyewe maandalizi ya
Muungano … hivi sasa niko kwenye sherehe Ikulu,”
alisema.
Danadana hizo za polisi
zilianza wiki iliyopita, wakati MTANZANIA Jumapili lilipopata taarifa kuwa tukio
la kutekwa kwa Ludovick aliloliripoti katika kituo cha Kigogo ni
feki.
Gazeti hili lilikumbana
na vikwazo vya kutoelezwa ukweli kuhusu tukio hilo la Ludovick wakati
likifuatilia taarifa hizo tangu Kituo Kidogo cha Polisi
Kigogo.
Mwandishi wa gazeti hili
alipofika kituo cha Kigogo alielezwa na askari aliyemkuta hapo kuwa taarifa za
matukio mbalimbali hufunguliwa hapo, lakini huhamishiwa Kituo cha Polisi cha
Magomeni kutokana na udogo wa kituo hicho.
Hivyo kumtaka mwandishi
kufuatilia suala hilo katika Kituo cha Polisi Magomeni. Gazeti hili lilipofika
Kituo cha Polisi Magomeni, kwa askari mpelelezi liliyeelekezwa kuwa anahusika na
kesi ya Ludovick aliyetajwa kwa jina moja la Afande Chuki, hakupatikana kituoni
hapo, bali lilipewa namba yake ya simu, alipotafutwa alikana kuhusika na suala
hilo kwa kuelekeza atafutwe Askari Polisi aliyetajwa kwa jina la Lukwamba
Sanga.
Afande Sanga alipopigiwa
simu na kuulizwa kuhusu sakata hilo, kwanza alikiri kuwa yeye ndiye mpelelezi wa
kesi hiyo na kuwa ni kweli Ludovick alifungua RB katika kituo cha Polisi cha
Kigogo, lakini hakuwa tayari kuzungumza chochote juu ya tukio
hilo.
Alieleza kuwa mwenye
mamlaka ya kutoa namba hiyo ni Mkuu wa Upelelezi wa Kituo ambaye hata hivyo
hakupatikana.
Ofisa mwingine kituoni
hapo alisema namba hiyo inaweza kutolewa kwa idhini ya Kamanda wa Mkoa wa Polisi
Kinondoni, Charles Kenyela, ambaye hata hivyo alipotafutwa kwa namba yake ya
simu alisema anahitaji muda kuipata namba hiyo kwa sababu ana majukumu mengi
hivyo atafutwe baadaye.
Hata alipotafutwa tena
simu yake ya kiganjani ilikuwa haipatikani na ilipokuwa hewani iliita pasipo
majibu.
Baada ya wiki moja
kupita, gazeti hili lilipomtafuta tena Kenyella, alisema bado hajaliona faili la
Ludovick kutokana na kutingwa na mambo mengi ya
kikazi.
Kurushiana mpira kwa
askari hao pamoja na Kamanda Kenyela kushindwa kutoa taarifa sahihi za RB hiyo
ndiko kunakozidisha maswali kuhusu utata wa tukio la kutekwa kwa
Ludovick.
Wapasha habari wetu
walilidokeza gazeti hili wiki iliyopita kwamba taarifa za kutekwa kwa Ludovick
na kunyang’anywa vitu vyake vyote alivyokuwa navyo, zikiwemo nguo alizokuwa
amevaa siyo za kweli, bali zimetengezwa ili kufanikisha mkakati wa kuwatia
nguvuni watuhumiwa halisi wa sakata la ugaidi.
Ludovick alidai kutekwa
usiku wa Jumanne ya Machi 5, mwaka huu, akiwa eneo la Sinza, ambako alisema
alitoa taarifa zake katika Kituo cha Polisi cha Kigogo na kufunguliwa RB yenye
namba KIG/RB/318/2013.
Source:JF
No comments:
Post a Comment