Mh. John Mnyika
IKULU imetakiwa kutoa ufafanuzi kwa umma kuhusu mkutano uliokuwa ufanyike kati ya Rais Jakaya Kikwete, mbunge wa Ubungo John Mnyika (CHADEMA) na watendaji wa mamlaka zinazosimamia masuala ya maji.
Hatua hiyo imekuja kutokana na mkutano huo kutofanyika na hivyo mbunge huyo kutaka ufafanuzi endapo mkutano huo utafanyika kabla ya kusomwa au kuhitimishwa kwa bajeti ya Wizara ya Maji.
Taarifa kwa vyombo vya habari iliyotolewa jijini Dar es Salaam jana na Ofisi ya Mbunge wa Ubungo, ilieleza kwa sasa inasubiri barua rasmi kutoka Ofisi ya Rais, ili kuwezesha hatua za haraka za kuboresha upatikanaji wa majisafi na ushughulikiaji wa majitaka jijini Dar es Salaam.
Taarifa hiyo ilieleza kwa mujibu wa ratiba ya Bunge, hotuba ya bajeti ya Wizara ya Maji kuhusu makadirio ya mapato na matumizi na miradi ya maendeleo katika sekta ya maji itawasilishwa bungeni Aprili 24, mwaka huu.
Rais alitoa ahadi ya kukutana na viongozi hao kutokana na madai ya wananchi kutaka majibu kutoka serikali juu ya hatua za haraka za kuboresha upatikanaji wa majisafi.
Mnyika alieleza katika majumuisho ya mjadala wa hotuba ya bajeti ya ofisi ya Rais, Waziri Steven Wassira, alimhakikishia kwamba mkutano huo utafanyika bila kueleza lini.
No comments:
Post a Comment