RAIS KIKWETE AKIMPONGEZA BI KIDUDE, IKULU |
Rais
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Jakaya Mrisho
Kikwete amemtumia Salamu za Rambirambi Waziri wa Habari, Utamaduni na
Michezo, Mheshimiwa Dkt. Fenella Mukangara kufuatia taarifa za kifo cha
Msanii Mkongwe hapa nchini, Marehemu Fatma Binti Baraka Hamisi ambaye
alijulikana sana kwa jina la kisanii la Bi. Kidude aliyefariki dunia
tarehe 17 Aprili, 2013 akiwa nyumbani kwake katika eneo la Bububu,
Zanzibar kutokana na kusumbuliwa na maradhi ya Kisukari kwa muda mrefu.
“Nimepokea
kwa masikitiko makubwa taarifa za kifo cha Msanii Mkongwe na Mwimbaji
Mashuhuri wa Nyimbo za Mwambao hapa nchini, Marehemu Fatma Binti Baraka
Hamisi maarufu kwa jina la Bi Kidude aliyefariki tarehe 17 Aprili, 2013
akiwa nyumbani kwake eneo la Bububu, Zanzibar kutokana na ugonjwa wa
Kisukari”, amesema Rais Kikwete katika Salamu zake za Rambirambi.
Katika
salamu hizo, Rais Kikwete amesema alimfahamu Bibi Fatma Binti Baraka
enzi za uhai wake kutokana na mchango wake mkubwa ndani na nje ya nchi
yetu katika nyanja za Sanaa na Utamaduni ambapo alimudu kuitangaza vyema
nchi yetu kupitia kipaji chake cha uimbaji kwenye matamasha mbalimbali
aliyowahi kuhudhuria na uimbaji wake kuwa kivutio kikubwa kwa watu wengi
waliowahi kuhudhuria matamasha hayo, kuyasikiliza kwenye Radio na
kuyatazama kupitia matangazo ya Televisheni.
“Kwa
hakika Fani ya Sanaa na Utamaduni imempoteza mtu muhimu ambaye mchango
wake ulikuwa bado unahitajika sana katika kuinua zaidi kiwango cha
uimbaji wa Muziki wa Mwambao ambao umejizolea sifa nyingi”, amesema Rais Kikwete katika Salamu zake na kuongeza,
“Kufuatia
taarifa hizo za kusikitisha, ninakutumia wewe Waziri wa Habari,
Utamaduni na Michezo, Mheshimiwa Dkt. Fenella Mukangara Salamu zangu za
Rambirambi kwa kumpoteza mmoja wa Wasanii nguli wa Muziki wa Mwambao
hapa nchini”.
“Vilevile
naomba unifikishie Salamu zangu za Rambirambi na pole nyingi kwa
Wanafamilia, ndugu na jamaa wa Marehemu Bibi Fatma Baraka Hamisi kwa
kupotelewa na mhimili madhubuti wa familia. Namuomba Mwenyezi Mungu,
Mwingi wa Rehema aipokee na kuilaza mahala pema peponi Roho ya Marehemu.
Amina”, amesema Rais Kikwete.
Aidha
Rais Kikwete amewapa pole Wasanii wote hapa nchini ambao kwa hakika
watakuwa wameguswa sana na kifo cha Bibi Fatma Baraka ambaye alichangia
vilivyo katika kuitangaza sanaa kupitia uimbaji wa Muziki wa Mwambao.
Amesema “kwa wao, njia bora ya kumuenzi Bi. Kidude ni
kuendeleza zaidi sanaa ya uimbaji wa Muziki wa Mwambao na kuyaenzi yote
mema na mazuri aliyolifanyia Taifa letu.”
Rais
Kikwete amewahakikishia wanafamilia, ndugu na jamaa wa Marehemu Fatma
Baraka kuwa yuko pamoja nao katika kuomboleza msiba huu mkubwa.
Imetolewa na:
Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,
Ikulu.
Dar es Salaam.
17 Aprili, 2013
No comments:
Post a Comment