* MILLIONI 50 KUTOLEWA KWA ATAKAYE SAIDIA UPELELEZI
Kwa ufupi
“Baada
ya kutua, nilisikia kishindo kikubwa nikashtuka ikabidi niangalie.
Baada ya kuona ni kitu kama chuma nilipata hofu nikafikiria kuondoka,”
Mwalimu
Dar es Salaam/Arusha. Bomu
lililorushwa na kuua watu watatu na kujeruhi wengine zaidi ya 60 kwenye
Kanisa Katoliki la Mtakatifu Joseph Mfanyakazi huko Arusha, inadaiwa
lilitengenezwa kienyeji.
Wakati
kukiwa na madai hayo, mazishi ya marehemu hao Regina Kurusei, (45),
James Gabriel (16) na Patricia Joachim (9) yanatazamiwa kufanyika leo
Olasiti, Arusha na Waziri Mkuu, Mizengo Pinda anatarajiwa kuhudhuria.
Ofisa mstaafu wa Jeshi la Wananchi wa
Tanzania (JWTZ), ambaye hakutaka jina lake liandikwe gazetini,
alimdokeza mwandishi wetu jana kuwa kwa ujuzi na uzoefu wake wa masuala
hayo, bomu hilo si la kiwandani akisema msingi wa imani yake ni jinsi
vyuma vilivyotawanyika na kuumiza watu zaidi ya 20.
Watu saba wamefikishwa kwenye Hospitali ya Taifa ya Muhimbili kwa ajili ya kuondolewa vyuma na kupata matibabu zaidi.
Mstaafu huyo alieleza kuwa mabomu mengi
zaidi ya kienyeji hutengenezwa kwa kutumia bakuli za chuma, zikiwekewa
baruti ndani na kufungwa kwa waya.
“Hawa jamaa huweka vipande kama 36 vya
baruti na hufungiwa ndani ya bakuli kwa kubanwa sana ili kuvipa joto na
bomu likitua, husababisha madhara makubwa,” alisema ofisa huyo ambaye
alishiriki Vita ya Uganda mwaka 1978 hadi 1979.
Mstaafu huyo alisema mabomu ya aina hiyo
yametumika kwenye mashambulizi ya kigaidi katika nchi mbalimbali
duniani kama Lebanon, Vietnam, Libya, Ireland Kaskazini, Syria,
Afghanistan, Iraq, Chechnya na India.
Mmoja wa majeruhi, Mwalimu Fatuma Tarimo amesimulia alivyoshuhudia bomu likitua mbele yake na kulipuka.
Tarimo, ambaye amelazwa katika Hospitali
ya Taifa ya Muhimbili, alisema jana kuwa aliliona bomu hilo likiwa na
rangi ya shaba. Pia alisema lilikuwa na waya kwa juu.
“Baada ya kutua, nilisikia kishindo
kikubwa nikashtuka ikabidi niangalie. Baada ya kuona ni kitu kama chuma
nilipata hofu nikafikiria kuondoka,” alisema mwalimu huyo wa Shule ya
Msingi ya Burka Estate, nje kidogo ya Jiji la Arusha. Hata hivyo,
alisema kabla ya kuondoka, alishtukia amenyanyuliwa juu na hakujua
kilichoendelea kwani aliposhtuka alijikuta akiwa katika Hospitali ya
Mount Meru.
Tarimo ametolewa kipande cha chuma katika mguu wake wa kulia.
“Nina maumivu bado lakini nina matumaini
nimechukuliwa kipimo cha ‘T-Scan’ kwa matibabu zaidi,” alisema Mwalimu
Tarimo ambaye anaaminika kuwa na kipande kingine kwenye mapafu.
Majeruhi mwingine, Jenipher Joackim
ambaye amefiwa na mwanaye Patricia Joackim (9) hana taarifa za kifo
hicho kilichotokea katika Hospitali ya KCMC.
“Nimeambiwa kwamba yupo ICU sijui anaendeleaje,” alisema.
Jeshi la Polisi mkoani Arusha
limetangaza donge nono la Sh50 milioni kwa watu watakaosaidia upelelezi
wa ulipuaji bomu huku likiwashikilia na kuwahoji watuhumiwa 12 hadi
sasa.
mwananchi
No comments:
Post a Comment