ADV

ADV

ADVERTISEMENT CORNER

HUDUMA YA KUKATA TICKET ZA NDEGE ONLINE


SOMA HABARI

SOMA HABARI

Friday, May 10, 2013

Mazishi ya Wakristo waliouwawa kwa bomu Arusha yafanyika


Mapadri wa kanisa katoliki wakiwa wamebeba jeneza lenyenye mwili wa mmoja wa waliokufa katika tukio la kutupwa kwa bomu la mkonokatika kanisa la Olasiti Arusha may 5, 2013.
Mapadri wakiwa wamebeba mislaba yenye majina ya marehemu wawili kati ya watatu waliofariki kwenye tukio la bomu la kurushwa kwa mkono kwenye kanaisa la Olasiti jijini Arusha May 5, 2013, katika ibada ya mazishi iliyofanyika kwenye kanisa hilo may 10,2013.
Askofu wa Jimbo Kuu la Arusha, Mhashmu Josephat Lebulu akinyunyuzia maji miili ya waumini wa kanisa hilo waliofariki katika tukio la kurushwa kwa bomu la mkono kwenye kanisa la Olasiti jijini Arusha may 10,2013.
Kiongozi wa kanisa Katoliki nchini, Mhashamu Polycarp kaldinari Pengo akiongoza ibada ya mazishi ya waumini wa kanisa hilo waliouwawa katika bomu lililotupwa kwenye kanisa la Olasiti Arusha May 5,2-13. Kuhoto ni Askofu wa Jimbo Kuu la Arusha, Mhashamu Josephat Lebulu.



Arusha. Watu watatu, waliofariki katika shambulio la bomu katika Kanisa Katoliki la Mtakatifu Joseph Mfanyakazi, Parokia ya Olasiti, mkoani Arusha wamezikwa jana na mamia ya watu, huku ulinzi ukiwa umeimarishwa kuliko kawaida na viongozi wa dini na Serikali kutoa kauli nzito.
Marehemu hao, ni  Regina Loning’o Laizer (45), James Gabriel(16) na  Patricia Joachim Assey(9) walizikwa katika eneo la kanisa hilo Katoliki, mazishi yaliyohudhuriwa na maaskofu wanane wa majimbo tofauti ya Kanisa Katoliki, Mkuu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania(KKKT), Askofu Alex Malasusa, Waziri Mkuu Mizengo Pinda na viongozi mbalimbali wa dini, Serikali na kisiasa.

Kauli za viongozi
Katika ibada hiyo ya viongozi mbalimbali wa kidini, walitoa salama zao akiwamo Rais wa Baraza la Maaskofu wa Kanisa Katoliki Tanzania (TEC), Askofu Tarcisius Ngalalekumtwa aliyeitaka Serikali kutumia msamiati wa mwenye macho haambiwi tazama na kukomesha mpasuko wa kidini aliosema unalitafuna taifa.
Askofu huyo alisema kuwa miongo mitatu sasa, Serikali imekaa kimya, ikishuhudia mafundisho na mihadhara ya kidini inayochochea na kuhamasisha uhasama kati ya Ukristo na Uislamu, bila kuchukua hatua kukomesha hali hiyo.
“Matukio mbalimbali yanayoashiria uhasama wa kidini yanayotokea nchini. Kuna mihadhara, CD, DVD, machapisho na mafundisho yanayotishia maisha na usalama wa viongozi wa kanisa na waumini wao, ambayo yamefuatiwa na uchomomaji wa makanisa,” alisema Askofu Ngalalekumtwa.
Alitaja mfano wa kongamano la Januari 15, mwaka juzi iliyofanyika Ukumbi wa Diamond Jubillee jijini Dar es Salaam kuwa moja ya mikutano iliyojaribu kuchochea chuki ya kidini kati ya Waislamu na Wakristo kwa kudai kuwa Serikali ya Tanzania inaongozwa kwa mfumo Kikristo ulioasisiwa na Hayati Mwalimu Julius Nyerere.
Askofu huyo alisema kwamba katika kongamano hilo, washiriki waliaminishwa kuwa Serikali inatoa fedha za ruzuku kujenga shule na taasisi za kanisa kutokana na kuwapo mkataba maalumu kati ya kanisa na Serikali, jambo ambalo siyo kweli.
“Kinachosikitisha zaidi ni kwamba Serikali haikukanusha madai na uchochezi huo, licha ya mambo hayo kufanyika na kusemwa hadharani kwa wahusika kuzunguka nchi nzima kueneza chuki na uchochezi huo,” alisema Askofu Ngalalekumtwa.
Mkuu wa Kanisa la KKKT, Askofu Dk Alex Malasusa alisema kuwa tukio la Arusha ni la kikatili na aibu kwa taifa akiwataka wenye dhamana ya ulinzi na usalama kuchukua hatua kudhibiti hali hiyo akionya kuwa wasipofanya hivyo watahukumiwa kwa kosa la kukaa kimya mambo yakiharibika mikononi mwao.
“Wote wenye jukumu la kulinda na kuitunza amani waifanye kazi hiyo bila uoga. Wasipofanya hivyo iko siku watahukumiwa,” alisema Dk Malasusa
Mwakilishi wa Muungano wa Madhehebu ya Kikristo mkoani Arusha, Askofu Stanley Hotay aliwataka viongozi wa kisiasa kuepuka kutumia jukwaa la dini kutimiza malengo ya kisiasa, akionya kuwa makanisa hayana itikadi, bali waumini ndiyo wenye itikadi mbalimbali.

“Sote tuliomo ndani ya jahazi lazima tuwakemee na kuwadhibiti vichaa wanaojaribu kutoboa jahazi letu kwani tusipofanya hivyo maji yatajaa ndani, chombo kitazama na sote tutaangamia,” alisema Askofu Hotay.

Viongozi wa kisiasa waliohudhuria ni pamoja na Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe na Mwenyekiti wa NCCR- Mageuzi, James Mbatia  na wabunge kadhaa.

Salamu za Serikali
Akitoa salamu za Serikali katika ibada hiyo ya mazishi, Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, alitoa pole kwa tukio hilo akaeleza kuwa yoyote anayedhani kuua muumini mmoja, Askofu au Mufti ataua Ukristo au Uislamu,  hajui kuwa hiyo haitawezekana.
Pinda alisema Serikali imetoa Sh100 milioni ikiwa ni rambirambi zake akiongeza kuwa dini za Kikristo na Kiislamu  zina historia ndefu duniani.
“Itakuwa ni kujidanganya kuwa ukiua kiongozi wa dini leo utaifuta dini hiyo, kwani kwa kuamini hivyo hiyo ni ndoto,” alisema Pinda.
Waziri Mkuu, alisema kwamba Serikali imeagiza vyombo vyote vya usalama nchini, vifanye kazi usiku na mchana kuhakikisha amani na utulivu unaendelezwa nchini.
Aliwataka Watanzania kuwa watulivu, hasa watakaposikia kamatakamata inaendelea na kueleza kuwa lengo la hatua hiyo ni kulinda amani ya nchi.

Ulinzi waimarishwa
Ulinzi uliimarishwa eneo lote kuzunguka kanisa hilo, barabara za kuingia Parokia hiyo na katikati ya Jiji la Arusha. Maofisa wa Polisi na Usalama kutoka makao makuu jijini Dar es Salaam na Maofisa Usalama wa Taifa kutoka maeneo mbalimbali waliimarisha ulinzi.
Askari wenye silaha za moto na mabomu, waliranda juu ya kanisa hilo kwa kupeana zamu, huku baadhi wakiwa na miwani na kuona mbali. Maeneo mengine askari wanafunzi wa Chuo cha Polisi Moshi, walikuwa wameimarisha ulinzi na kuwapekua waliowatilia shaka




Mahubiri ya Kardinali Pengo
Ndugu zangu,
Nafasi hii inaunganisha mawazo ya furaha na uchungu kutokana na kilichotukutanisha leo.

Mazingira haya yanaweka ugumu wa kupata cha kusema. Ila sisi ni watu wa imani. napenda kueleza imani yetu kama tunavyopaswa kuwa kwenye mazingira haya.

Tumejumuika ili kuwaweka kwenye nyumba ya milele hawa marehemu, lakini pia tunatumia nafasi hii kubariki Kanisa.

Kila mbatizwa ni kiungo cha mwili wa Kanisa. Kila kiungo cha mwili kinapaswa kuungana na kichwa cha Mwili ambae ni Yesu Mwenyewe

Kristo akipitia kwa mdomo wa mtume Paulo anatufundisha kuwa “Msijaribu kushindana na uovu kwa uovu, lakini shindeni uovu kwa wema”.

Katika viongozi waanzilishi wa dini, ni Yesu peke yake aliyetolea uhai wake kujenga imani ya wafuasi wake. Viongozi wengine hawajikutoa sadaka wenyewe, na baadhi wametoa sadaka ya maisha ya watu wengine kwa ajili ya kueneza imani yao.

Sisi Wakristu Imani yetu inajengwa juu ya mwanzilishi wetu ambaye alitoa uhai wake ili kujenga imani yetu, na hakutoa uhai wa mtu yeyote kwa ajili ya kujenga imani yetu.

Katika masomo tuliyosikia leo, Somo la plili limetupa neno la Mtume Paulo Rum:12:17 linasisitiza hilo: usishinde uovu kwa uovu, bali shinda uovu kwa wema.

Soma la Kwanza limeeleza kuwa Paulo na Sila wanateswa kwa ubaya mkubwa sana na kuwekwa gerezani kwa ubaya. Na baada ya kufunguliwa kwa muujiza, askari wa magereza alitaka kujiua, lakini Paulo na Sila wakatenda lililo jema kuokoa maisha yake. Ni baada ya wema huo wokovu ulifika kwa askari huyo na jamaa yake yote wakaweza kumwamini Mungu.

Nawauliza waumini: “Wale waliotekeleza ubaya huu, akija mbele yetu akasema ni mimi ndiye, tungefanya nini kama waumini kwa kufuata mfano wa Yesu?”

Mimi nawaambia “Tujifunze kutoka kwa Bwana wetu Yesu Kristo: ‘Tusidiriki kulipia uovu kwa uovu, lakini tutende mema ili kushinda uovu’.”

Lakini haya hayaondoi majukumu ya serikali, ambayo yanabaki, na si mimi ninayepaswa kuyasema, wenye mamlaka wanayajua majukumu yao. Mimi nawaambia ninyi waumini.

Uovu si kitu kinachopendeza. Warumi waliwatesa wakristo kwa karne tatu, na haikusaidia chochote Himaya ya Warumi, ambayo baadaye ilisambaratika. Lakini imani yetu imebaki.

Amemalizia kwa kusema: Tukio hili na tukio la mauaji ya Padre Mushi, isiwe sababu ya kuacha amani ya nchi yetu isambaratike.

Lakini ni jukumu la wananchi wotte kuhakikisha nchi yetu haisambaratiki.

Wenye mamlaka watimize wajibu wao. Sisi wakristo tusamehe, tusijibu uovu, tudumishe amani na upendo katika taifa letu.

Tumsifu Yesu Kristu.

No comments:

Post a Comment

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...