MWENYEKITI wa Chama
cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Freeman Mbowe, amenusurika kuuawa kwa
kitu kinachodhaniwa kuwa ni bomu, lililolipuka katika mkutano wa hadhara wa
kampeni za udiwani mkoani Arusha.
Mbali ya Mbowe,
viongozi wengine mbalimbali waandamizi wa chama hicho, akiwamo Mbunge wa Arusha
Mjini, Godbless Lema, walinusurika katika mlipuko huo wa bomu hilo lililorushwa
katika Uwanja wa Soweto muda mfupi baada ya mwenyekiti huyo kumaliza kumnadi
mgombea udiwani wa Kata ya Kaloleni, Emanuel Kessy, jijini hapa.
Habari
kutoka eneo la tukio zilisema kuwa watu kadhaa wanasadikiwa kufariki dunia na
wengine zaidi 15 wamejeruhiwa sehemu mbalimbali za miil
i
yao ikiwamo miguuni na kichwani wakiwamo watoto wawili wanaodaiwa
kuvunjika miguu.
Kamanda wa Polisi wa
Mkoa wa Arusha, Liberatus Sabath, alithibitisha kuwa watu wawili waliuawa
katika mlipuko huo na kulielezea tukio hilo kuwa ni kubwa na baya kuendelea
kutoka mjini hapa.
Mwezi mmoja uliopita,
mlipuko wa bomu kama hilo ulitokea katika Kanisa Katoliki Olasiti la Joseph
Mfanyakazi na kusababisha vifo vya watu watatu na wengine kadhaa kujeruhiwa.
Mmoja wa mashuhuda
aliyezungumza na Tanzania Daima Jumapili muda mfupi baada ya mlipuko wa jana,
alisema alijitokeza mtu ambaye hakujulikana anapotokea na kurusha bomu la mkono
katikati ya umati na bomu hilo kutoa kishindo kikubwa.
Alisema baada ya mtu
huyo kurusha bomu hilo baadhi ya wananchi na wafuasi wa CHADEMA walimuona,
walianza kumkimbiza na kabla hawajamfikia polisi waliokuwa wameweka ulinzi
katika eneo hilo waliingilia kati na kuzuia mtu huyo asifikiwe.
Bomu lililorushwa
linadaiwa kuwa lilielekezwa katika jukwaa walilokuwa Freeman Mbowe na viongozi
wengine ambao muda mfupi kabla ya tukio hilo walikuwa wameshuka jukwaani kwa
ajili ya kuondoka katika eneo hilo.
Hali katika eneo la
tukio ilikuwa mbaya baada ya damu kutapakaa sehemu mbalimbali ya uwanja wa
Soweto na majeruhi zaidi ya 20 wakikimbizwa katika hospitali za jijini humo.
Wafuasi wa CHADEMA
waliendelea kukakaa katika uwanja huo huku wakihanikiza kwa wimbo wa
kukishutumu Chama Cha Mapinduzi (CCM) kuwa kinawaua.
Chanzo kingine
kilieleza kuwa katika majeruhi waliopelekwa katika Hospitali ya Mount Meru,
mtoto mdogo ambaye jina lake halijajulikana amefariki dunia.
Mwenyekiti wa CHADEMA
Mkoa wa Arusha, Samson Mwigamba, alisema bomu hilo ni mbinu ya watu wanaohofia
kushindwa katika uchaguzi huo na kuwataka wafuasi wao kutoka maeneo yasiyo na
uchaguzi kujitokeza kwa wingi kulinda kura zitakazopigwa leo.
Hali katika Hospitali
ya Mount Meru
Tanzania Daima
Jumapili lilishuhudia majeruhi hao wakiingizwa na kutolewa katika Hospitali ya
Mount Meru mara baada ya kutokea kwa tukio hilo lililotokea saa 11:40 muda
mfupi baada ya Mbowe kumaliza kuhutubia wananchi wa kata hiyo na kumuombea kura
mgombea huyo.
Katika Hospitali ya
Mount Meru, umati mkubwa wa wafuasi wa CHADEMA ulifurika muda mfupi baada ya
kutokea kwa tukio hilo, ambao wengi wao walionekana kushinikiza wauguzi
wachache waliokuwepo hospitalini hapo kuwapatia majeruhi huduma ya kwanza.
Zoezi zima la
kushinikiza wauguzi hao kuwapatia huduma majeruhi hao liligeuka baada ya baadhi
ya wauguzi kujificha wakiogopa umati huo wa wafuasi wa CHADEMA, hivyo majeruhi
kukosa huduma ya kwanza.
Hali hiyo iliwalazimu
wafuasi wa CHADEMA kubeba majeruhi hao waliokuwa wakivuja damu katika miili yao
kwa kutumia magari binafsi na kuwahamishia hospitali mbalimbali ikiwamo
Hospitali ya Rufaa ya Kanisa la Kiinjili la Kilutheri ya Seliani ya jijini
hapa.
Mmoja wa wafuasi wa
CHADEMA aliyejitambulisha kwa jina la Martin Lucas, alidai wakiwa katika Uwanja
wa Soweto huku mkutano ukiendelea kwa amani na utulivu na Mwenyekiti wa CHADEMA
alipomaliza kuhutubia na kushuka jukwaani akielekea kupanda gari lake tayari
kuondoka, ghafla mlipuko mkubwa ulitokea katika jukwaa alilokuwa akihutubia.
“Ndugu mwandishi hii
ni hujuma kabisa, mkutano ulifanyika kwa amani na utulivu wa kutosha, ghafla
tukashangaa watu wanaanguka chini huku moshi mkubwa ukipaa juu, sisi
tulikuwa pembeni ya mti tukafikiri mwenyekiti wetu amepigwa bomu lakini haikuwa
hivyo, yeye alishapanda gari na kuanza safari, watu wengi wameumia sana ndugu
yangu,” alisema mfuasi huyo, Robert Kinabo.
Hadi tunakwenda
mitamboni eneo lilipotokea mlipuko huo lilikuwa limezingirwa kwa alama ya tahadhari
ya Jeshi la Polisi kwa ajili ya kuwasubiri wataalamu wa milipuko kutoka Jeshi
la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) kwa ajili ya kubaini aina ya mlipuko.
CHANZO TANZANIA
DAIMA.
No comments:
Post a Comment