Wakati Jeshi la Polisi nchini limesema limepata taarifa za
mwonekano wa mtu aliyetupa bomu katika mkutano wa kampeni wa Chama cha
Demokrasia na Maendeleo (Chadema) Arusha,Mwenyekiti wa chama hicho Freeman
Mbowe amesema wabunge wake leo hawataingia bungeni.
Akizungumza na waandishi wa habari jana,
Mbowe alisema wabunge hao watawasili Arusha kwa ajili ya kuungana na wananchi
pamoja na wanachama kwenye msiba huo.
Alisisitiza kwamba kuanzia leo mahema yatawekwa viwanja vya
Soweto kwa ajili ya kuomboleza msiba huo na mara polisi wakimaliza
uchunguzi wao na kutoa majibu juu ya vifo hivyo, marehemu hao watasafirishwa.
Wakati Mbowe anatoa kauli hiyo Waziri wa Mambo ya Ndani, Dk
Emmanuel Nchimbi akizungumza jana mjini Arusha na waandishi wa habari, alisema
taarifa za awali zinaonesha mlipuko huo ni bomu la kutupwa kwa mkono
(grumeti) na hivi sasa timu ya wataalamu ikiongozwa na Kamishna wa
Operesheni Maalumu wa Jeshi la Polisi, Paul Chagonja inaendelea na uchunguzi wa
tukio hilo.
Naye Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini, Inspekta
Jenerali wa Polisi (IGP), Said Mwema katika taarifa yake kwa vyombo vya
habari ameahidi kupambana na kuhakikisha wahusika wanapatikana.
Alitoa taarifa hiyo jana kwa waandishi wa habari Dar es
Salaam na kusema hadi jana, watu waliothibitika kufa katika tukio hilo ni
wawili na 68 ni majeruhi.
Waliokufa ni Katibu wa Baraza la Wanawake (Bawacha) wa
Chadema, Kata ya Sokoni 1, Judith Moshi (25) na mtoto aliyejulikana kwa jina
moja la Justin.
"Mpaka hivi sasa watu waliokufa ni wawili na
wengine 68 wamejeruhiwa na mlipuko huo, lakini naahidi kuwa tutapambana na
kuhakikisha tunawapata wahusika," alisema Mwema.
Sanjari na kupatikana taarifa juu ya mtu aliyetupa bomu,
Mwema alisema timu ya jeshi hilo imetumwa kutoka makao makuu kwenda
Arusha kuongeza nguvu katika upelelezi.
Hata hivyo, hakufafanua zaidi juu ya mtuhumiwa huyo kutokana
na kile alichosema taarifa husika zinafanyiwa uchunguzi kabla
ya kuwakamata watu sahihi waliohusika na tukio hilo.
Kwa mujibu wa IGP Mwema, timu ya polisi kutoka Makao Makuu
inayoongozwa na makamishna wawili, imeondoka kwenda mkoani Arusha
kuongeza nguvu katika operesheni na upelelezi.
Timu hiyo inaongozwa na Kamishna wa Operesheni na Mafunzo,
Paul Chagonja na Isaya Mngulu kutoka Idara ya Upelelezi wa Makosa ya Jinai,
wakishirikiana na vyombo vingine vya ulinzi.
Alisema polisi inafanya operesheni kali nchini kote
kuhakikisha inawatia mbaroni watu wote waliowezesha, waliofadhili na waliotenda
uhalifu huo.
"Kikubwa wananchi waendelee kuwa watulivu na waendelee
kutoa ushirikiano kwa wakati wote uchunguzi ukiendelea," alisema.
IGP ametaka mtu yeyote atakayekuwa na taarifa za wahalifu
hao, atoe taarifa kupitia namba yake ya simu ambayo ni 0754 785557 au kwenye kituo chochote cha polisi ili
wakamatwe.
‘Kwa nini iwe Arusha’ hii ni kauli ya Mkuu wa Mkoa wa
Arusha, Mulongo aliyoitoa baada ya kutembelea majeruhi katika Hospitali za
Mount Meru, St Elizabeth pamoja na Hospitali ya Arusha Lutheran Medical Centre
jijini.
“Nawapa pole sana ndugu zangu wa Chadema, na wana Arusha kwa
ujumla pamoja na watanzania. Lakini najiuliza kwa nini Arusha …tukio hili
limenihuzunisha sana na nawaomba tusiingize masuala ya kisiasa, tuache polisi
wachunguze tukio hili kwani timu ya wataalamu kutoka Jeshi la Ulinzi la
Wananchi Tanzania (JWTZ) pamoja na wataalamu wengine wanachunguza tukio hili na
wahusika watachukuliwa hatua.’’
Mulongo ambaye tukio hilo la juzi limekuja ikiwa ni
mwezi mmoja tangu kutokea kwa mlipuko katika Kanisa Katoliki la Joseph
Mfanyakazi la Olasiti, alisema jana anayefanya ulipuaji wa mabomu na kumwaga
damu za watu mbalimbali na wengine kufa, ipo siku Mungu atamhukumu.
Kati ya majeruhi 59 waliolazwa kwenye hospitali
hizo, wawili wamehamishiwa Hospitali ya KCMC kutoka Hospitali ya AICC kwa
matibabu. Wagonjwa wengi wamelazwa hospitali ya Selian ambao ni 40. Hata hivyo,
wanane waliruhusiwa baada ya matibabu.
Mkuu wa Mkoa alisema anajisikia mnyonge kutokana na
matukio hayo mawili tofauti; mlipuko wa kanisani na la juzi wakati Chadema
ilipokuwa ikihitimisha kampeni zake za udiwani kwenye kata nne za Themi,
Kaloleni, Elerai na Kimandolu ambao hata hivyo uliahirishwa kutokana na tukio
hilo.
Mulongo alitaka wananchi wasihusishe na masuala ya
kisiasa badala yake wawaachie polisi kuchunguza tukio hilo. Kwa mujibu wa
Mulongo, watu kadhaa wamekamatwa.
Katika kipindi kisichozidi miezi miwili, mji wa Arusha
umeshuhudia majeruhi wasiopungua 130, na vifo vya watu watano vilivyotokana na
kurushwa mabomu na watu wasiojulikana katika mikusanyiko kanisani na kwenye
mkutano huo wa siasa wa Chadema.
Katika tukio la mwezi uliopita katika Kanisa Katoliki la
Mtakatifu Joseph Mfanyakazi, watu watatu walifariki na wengine wapatao 59
kujeruhiwa.
Mmoja wa watuhumiwa ambaye ni dereva wa pikipiki maarufu kama
bodaboda, Victor Ambrose alifikishwa mahakamani akidaiwa kuhusika katika
shambulio hilo.
Akizungumza na waandishi wa habari, daktari wa hospitali ya
Selian, Paul Kisanga alisema walipokea wagonjwa 48 kabla ya wanane
kuruhusiwa.
Alisema miongoni mwa wagonjwa hao, wamo watoto watano wanne
wakiwa wa kiume na mmoja wa kike. Mtoto Fahad Jamal (7) amelazwa kwenye
wadi ya wagonjwa mahututi chini ya uangalizi wa madaktari.
Hospitali ya St Elizabeth wapo wagonjwa wanane na Mount Meru
imepokea wagonjwa tisa. Mganga Mkuu wa Mkoa wa hospitali ya Mount Meru, Frida
Mokiti alisema wamepokea miili ya marehemu wawili ambao ni Judith Moshi (25)
ambaye ni Katibu wa Baraza la Wanawake (Bawacha) kata ya Sokoni 1, Jijini
Arusha pamoja na mtoto aliyejulikana kwa jina moja la Justin (13).
Kwa mujibu wa majeruhi wa tukio hilo, Abraham Samuel
waliona kitu kikiwa kwenye mfuko wa rambo kikirushwa juu na baada ya muda mfupi
walisikia vilio na wengine kuzimia.
Kitu hicho kilirushwa kabla ya Mwenyekiti wa Taifa wa
Chama hicho Taifa, Freeman Mbowe kuhitimisha kampeni za uchaguzi za udiwani wa
kata nne za Jimbo la Arusha Mjini.
Mlipuko huo unadaiwa kuwa ulitokea jirani na gari la
matangazo la Chadema, aina ya Mitsubishi Fuso lililokuwa karibu na jukwaa
alilokuwa akitumia Mbowe.
Mwenyekiti wa Chadema, Mbowe amedai tukio hilo si la bahati
mbaya bali lilipangwa na kundi la watu.
Akizungumza na waandishi wa habari jana, alisema wabunge wa chama
hicho leo hawataingia bungeni bali watawasili jijini Arusha kwa ajili ya
kuungana na wananchi pamoja na wanachama wa kwenye msiba huo.
Kwa mujibu wa Mbowe, marehemu Judith atapelekwa mkoani
Kilimanjaro na Justin atapelekwa mkoani Tabora kwa ajili ya maziko mara baada
ya polisi kukamilisha uchunguzi juu ya tukio hilo.
Alisisitiza kwamba kuanzia leo mahema yatawekwa viwanja vya
Soweto kwa ajili ya kuomboleza msiba huo na mara polisi wakimaliza
uchunguzi wao na kutoa majibu juu ya vifo hivyo marehemu hao watasafirishwa.
‘’Nimetembelea
majeruhi jana hospitalini lakini kwa Hospitali ya Selian, Arusha Lutheran
Medical Centre majeruhi ni wengi lakini walioumia sana ni watoto kuna mtoto
mmoja amekatika mkono na mguu ambaye ni Sharifa Jumanne na Amiri Ally ana vyuma
vitatu mwilini mwake,’’alisema
Mbowe.
Ingawa polisi imesema inaendelea na uchunguzi wa tukio hilo
kabla ya kutoa taarifa kamili, Mbowe aliwaambia waandishi wa habari kwamba zipo
taarifa kwamba shambulio hilo liliambatana na risasi za moto.
Chama cha Wananchi (CUF) kupitia kwa Mwenyekiti wake, Profesa
Ibrahim Lipumba, kimelaani tukio hilo na kutaka Serikali ichukue hatua za
haraka na kukamata waliohusika na matukio hayo iwe fundisho.
“Hatuna sababu na tusijenge utamaduni wa nchi yetu kugeuka eneo
ambalo palipo na mkusanyiko mabomu yanalipuka, Tanzania ni nchi ya amani, kwa
matukio haya CUF tunalaani kwa nguvu zote na kutoa pole kwa familia
zilizoathirika,” alisema
Lipumba.
Lipumba alisema kitendo kilichofanyika katika mkutano huo wa
Chadema ni unyama wa kutisha wenye makusudi ya kundi fulani kutekeleza azma yao
dhidi ya chama, watu, kundi na viongozi.
Alisisitiza kuwa utamaduni huo wa kufanya unyama katika
mkusanyiko wa watu unapaswa kudhibitiwa mapema ili kuepusha madhara
mengine ndani ya jamii kwa kusababisha vifo, ulemavu wa kudumu na familia
tegemezi.
“Tumefikia hatua
mbaya sana ya kufanya siasa za mabomu huu ni utamaduni unaopaswa kukemewa na
kupingwa, matukio haya yanajirudia kutokana na Serikali yenyewe
kuyakaribisha kwa kushindwa kuwachukulia hatua kali wahusika, tunaomba dola
ifanye ifanyalo katika uchunguzi wake na kuwakamata na kuwafikisha wahusika
kwenye vyombo vya sheria,” alisisitiza.
No comments:
Post a Comment