Na Jennifer Chamila,MAELEZO
Msajili wa vyama vya Siasa nchini
amewaasa wanachama na viongozi wa Chama Cha Democrasia na Maendeleo
(CHADEMA) kutumia muda wao kufanya shughuli za siasa ili kuchangia
maendeleo ya nchi badala ya kutumia uwezo na muda wao kubuni mambo
yanayoleta mtafaruku na kuhatarisha amani ya nchi.
Pia amepinga tamko la chama hicho la kuanzisha mafunzo ya kujilinda kwa vijana wake nchi nzima.
Kwa mujibu wa taarifa kwa vyombo vya
habari iliyotolewa leo jijini Dar es Salaam na kusainiwa kwa niaba ya
Msajili wa vyama vya siasa Sisty Nyahoza alisema kuwa hajawahi kuruhusu
CHADEMA au chama chochote cha siasa kufanya mafunzo ya ukakamavu au
mafunzo ya kutumia nguvu ya aina yoyote kwa wanachama wake au mtu
yeyote yule.
Anaongeza kuwa CHADEMA wanaruhusiwa
kuanzisha vikundi vya kujilinda lakini hawaruhusiwi kuanzisha mafunzo ya
kutumia nguvu kwaajili ya kujilinda kama walivyo tangaza katika
mikutano yao ya hadhara kwani ni kinyume na Demokrasia na Katiba ya
Jamuhuri ya Muungano.
Nyahozo ametoa ufafanuzi kuhusu
vikundi vya ulinzi na usalama vilivyopo katika Katiba ya Vyama vya Siasa
kwamba vikundi hivyo haviruhusiwi kufanya mafunzo ya kutumia nguvu ya
aina yoyote katika kutekeleza majukumu yao.
Bali wajibu wao ni kutoa taarifa wa
vyombo vya Dola pale wanapo sikia au kuona uhalifu ukitokea na wala sio
kupambana na wahalifu au watu wanaotaka kuwadhuru kama tamko la
CHADEMA la tarehe 9 mwezi huu linavyo sema.
“Hakuna maelezo yoyote katika Katiba
ya CHADEMA yanayoruhusu kutumia nguvu kufanikisha shughuli za kulinda
mali na Viongozi wa Chama.Ni vyema wananchi wote waelewe kuwa Sheria za
Nchi zimeweka masharti maalumu kwa Vyama Vya Siasa kutokana na umuhimu
wa vyama hivi katika kudumisha aman utulivu na umoja wa Kitaifa”,
alisema Nyahoza.
Alisema kuwa kutokana na Ibara
ya20(2)C ya Katiba ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1997
inasema kuwa “Bila kujali masharti ya ibara ya (1) na (4),haitakuwa
halali kwa chama chochote cha siasa kuandikishwa ambapo kutokana na
katiba au sera yake:-kinakubali au kunapigani matumizi ya nguvu au
mapambano kama njia za kufikia malengo yake ya kisiasa.
Nyahoza alimaliza kwa kuwataka
CHADEMA kuacha kutekeleza mpango walio tangaza wa kuanzisha makambi ya
kufanya mafunzo ya kujilinda kwa vijana wao nchi nzima,kwani kufanya
hivyo ni kukiuka sheria za nchi na endapo watashindwa kutii agizo
hilo hatua za Kisheria zitachukuliwa dhidi yao.
No comments:
Post a Comment