Mheshimiwa Edward Lowassa Photo swahili TV |
Na Swahili TV
Aliyekuwa Waziri Mkuu wa Tanzania Mheshimiwa
Edward Lowassa, amemsifia Rais Jakaya Kikwete kuwa ameweza kuifanya Tanzania
kupata heshima katika ulingo wa kimataifa, aliyasema hayo wakati akihojiwa na
Swahili TV jijini Washington DC.
Alisema kitendo cha Rais wa Marekani Bwana
Barack Obama kuja nchini na viongozi mbalimbali wa mataifa makubwa kumeonyesha
Rais Kikwete anakubalika.
“Ni hivi karibuni tu Rais Xi Jinping wa China,
Rais Obama na Rais mstaafu wa Marekani George W. Bush walikuwa nchini Tanzania,
hii inaonyesha kuwa Tanzania iko juu katika medani za kimataifa” alisema
Mheshimiwa Lowassa.
Mheshimiwa Lowassa ambaye yuko nchini Marekani
kwa ziara ya kikazi, aliongeza kwa kusema, Rais Kikwete anastahili pongezi sana
kwa hilo kwani sio rahisi kwa viongozi wa mataifa makubwa kutembelea nchi
zingine labda kama mko juu sana katika medani za kimataifa.
Pia alisema Rais Kikwete amekuwa akihusishwa na
utatuzi au ushauri wa kutatua matatizo mbalimbali ya nchi zingine na pia ameanza
kuishirikisha Tanzania katika usimamizi wa amani katika nchi mbalimbali.
Tanzania iliweka historia hivi karibuni kwa
maraisi wawili wa Marekani kukutana katika nchi moja kwa wakati mmoja, Rais
Barack Obama na George W.Bush walikutana jijini Dar es Salaam mwezi huu.
No comments:
Post a Comment