LICHA ya
kuwapo kwa shutuma mbalimbali zinazopinga mpango wa Chama cha Demokrasia
na Maendeleo (CHADEMA) kuanzisha kikundi cha kujihami cha Red Brigade
kitakachotoa ulinzi kwa viongozi wao, imebainika kuwa msajili wa vyama
vya siasa nchini, John Tendwa alitoa baraka za kuanzishwa kwake.
Tanzania
Daima imeona nakala ya barua ya mwaka 2005 kutoka katika ofisi ya
Tendwa, ikionyesha kubariki jambo hilo ambalo katika siku za hivi
karibuni limezua gumzo kubwa na kusababisha Mwenyekiti wa CHADEMA,
Freeman Mbowe, kuhojiwa na polisi kuhusiana na kauli zake.
Uchunguzi wa
kina uliofanywa na Tanzania Daima umebaini kuwa Desemba 30, 2004 ofisi
ya msajili wa vyama siasa ilimwandikia Katibu Mkuu wa CHADEMA barua
yenye kumbukumbu Na. RPP/CHADEMA/72/29 ikitaka ufafanuzi baada ya
kusikia kupitia vyombo vya habari kuwa chama hicho kinataka kuanzisha
kikundi cha kujihami (Red Brigade).
“Kulingana
na Ibara ya 9 (2) (c) ya Sheria Na. 5 ya Vyama vya Siasa 1992, ibara ya
147 na 148 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Sheria ya
Jeshi la Polisi, kuanzishwa kwa kikundi hicho ni kinyume cha sheria
hizo,” imeeleza sehemu ya barua hiyo.
Barua hiyo
ambayo Tanzania Daima inayo iliyosainiwa na Hilda Lugembe kwa niaba ya
msajili wa vyama vya siasa, inaeleza kuwa kuvunjwa kwa sheria hizo
kutasababisha CHADEMA kufutwa.
CHADEMA
baada ya kupata barua hiyo, Januari 6 mwaka 2005 iliijibu kuwa kikundi
kinachozungumziwa ni walinzi wa ndani ya chama, vijana wa kike na wa
kiume, wanachama wa CHADEMA, watu wasio na silaha, chini ya usimamizi wa
kurugenzi ya ulinzi na usalama ya chama hicho.
“Kikundi
kinachokusudiwa kuundwa ni kutokana na Katiba ya CHADEMA ambayo
inaruhusu uundwaji wa Kurugenzi ya Ulinzi na Usalama chini ya Katiba ya
CHADEMA, kifungu cha 7.6.4 (h),” inaeleza barua ya CHADEMA yenye
kumbukumbu Na. C/HQ/ADM/64 iliyosainiwa na Suzan Kiwanga kwa niaba ya
Katibu Mkuu wa CHADEMA.
Chama hicho
kiliilaumu serikali kwa vitisho ilivyotoa vya kutaka kukifuta endapo
kingeendelea na kusudio la kuanzisha kikundi hicho.
Hata hivyo,
baada ya ufafanuzi huo, Januari 11 mwaka 2005, ofisi ya msajili wa vyama
vya siasa, ilipopata majibu hayo ya CHADEMA, ilieleza kuwa kwa
madhumuni yaliyoelezwa na chama hicho inakubaliana na malengo ya
kuanzisha kikundi cha ulinzi kwa ajili ya usalama wa ndani ya chama.
“Ofisi ya
msajili wa vyama vya siasa, kwa madhumuni mliyoyatoa kwenye barua yenu
C/HQ/ADM/62 inakubaliana na maelezo yenu ya kuanzishwa kwa kikundi cha
ulinzi kwa ajili ya usalama wa ndani ya chama ingawa Katiba ya CHADEMA
haijatoa ufafanuzi huo, vinginevyo tunawatakia kila la heri kwenye
matayarisho ya uundwaji wa kikundi hicho,” ilisema barua ya msajili wa
vyama vya siasa nchini.
Barua hiyo
yenye kumbukumbu Na. RPP/CHADEMA/72/32 iliyosainiwa na Hilda Lugembe kwa
niaba ya msajili wa vyama vya siasa nchini, pia iliwatakia kila la heri
CHADEMA kwenye matayarisho ya uundwaji wa kikundi hicho.
Nakala za
majibu ya Ofisi ya Tendwa kwa CHADEMA zilipelekwa kwa Waziri wa Mambo ya
Ndani wakati huo, Omar Mapuri, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu,
aliyekuwa anashughulikia Habari na Siasa, Muhammed Seif Khatib; Katibu
Mkuu, Ofisi ya Waziri Mkuu; Inspekta Jenerali wa Polisi na Mkurugenzi wa
Makosa ya Jinai.
CHADEMA waibua mjadala
Julai 9
mwaka huu akisoma maazimio ya Kamati Kuu ya CHADEMA mbele ya vyombo vya
habari, Mwenyekiti wa chama hicho, Mbowe alitangaza mpango wa kuboresha
vikundi vya mafunzo ya kujilinda.
Baada ya
kauli hiyo watu mbalimbali akiwemo Rais Jakaya Kikwete, walijitokeza
kuupinga mpango huo kwa madai kuwa utasababisha uvunjivu wa amani na
utulivu vilivyodumu kwa muda mrefu hivi sasa.
Ofisi ya
msajili wa vyama vya siasa pia alimwandikia barua Katibu Mkuu wa CHADEMA
yenye kumbukumbu Na. 112/123/16A/3 kukitaka chama hicho kuacha
kutekeleza mpango huo kwani kufanya hivyo ni kukiuka sheria za nchi
ikiwamo sheria ya vyama vya siasa ya mwaka 1992 hali inayoonyesha
kujikanganya kwa ofisi hiyo kwani awali ilisharuhusu kitu hicho.
Barua hiyo
kutoka ofisi ya msajili inaongeza kuwa; “Kifungu cha 9(2) (c) cha sheria
ya vyama vya siasa kinakataza chama cha siasa kuruhusu kutumika,
kushabikia au kutumia nguvu na vurugu ili kufikia malengo yake ya
kisiasa.”
Kwa mujibu
wa barua hiyo iliyosainiwa na Sisty L. Nyahoza kwa niaba ya Msajili wa
Vyama vya Siasa, madai ya CHADEMA kusema kuwa “Chama Cha Mapinduzi (CCM)
wana kambi za mafunzo ya kupambana isiwe kisingizio cha vyama vingine
vya siasa kuvunja sheria ya vyama vya siasa.”
Msajili pia
kupitia barua hiyo amesema “kama CCM wanakiuka sheria, ni jukumu la
CHADEMA, kila chama na kila Mtanzania kutoa taarifa na ikiwezekana na
ushahidi katika taasisi husika ikiwamo ofisi ya msajili wa vyama vya
siasa ili suala hili lishughulikiwe kisheria.”
Hata hivyo,
Katibu Mkuu wa CHADEMA, Dk. Willibrod Slaa katika majibu yake
aliifahamisha Ofisi ya Msajili kuwa matumizi ya nguvu ikiwamo silaha kwa
ajili ya ulinzi wa maisha au mali yameruhusiwa na sheria ya jinai
kanuni ya adhabu sura ya 16 ya sheria ya Tanzania.
“Nimeshangazwa
sana na kauli yako kwamba vikundi vya ulinzi vya vyama vya siasa
vinapaswa kuwa na wanachama wasiokuwa na mafunzo ya kijeshi au ukakamavu
kama ilivyo kwa walinzi wa majumbani, kauli hii inadhihirisha ufahamu
wako mdogo wa mambo haya. Kwanza walinzi wa majumbani na maofisini
wanaoajiriwa na utitiri wa kampuni binafsi za ulinzi zilizosajiliwa
nchini kwetu hupatiwa mafunzo ya ulinzi na ukakamavu na wengine hupatiwa
silaha za moto,” alisema Slaa.
Alisema
kauli hiyo ya msajili wa vyama vya siasa kwamba jukumu la vikundi vya
ulinzi si kupambana na wahalifu au watu wanaotaka kuwadhuru, ni hatari
sana kwani inawapotosha wananchi wasitumie haki yao ya kujilinda
wanaposhambuliwa au kudhuriwa na wahalifu wa kisiasa.
“Barua yako
inatutishia kwamba endapo tutatekeleza mpango wetu wa mafunzo kwa
kikundi chetu cha ulinzi utakuwa si uamuzi wa busara kwa uhai wa chama
chetu.
“Kwa maneno
mengine endapo tutatekeleza haki yetu ya kujilinda kama tunavyoruhusiwa
na sheria za nchi yetu, kama tulivyoeleza katika barua hii, utatumia
mamlaka yako kumaliza uhai wetu kama chama cha siasa kwa kufuta usajili.
Hatutaki kuamini kwamba na wewe pia unatumiwa na CCM kukandamiza na
kutoa vitisho kwa chama kingine kwa manufaa yake,” alisema Dk. Slaa.
Chanzo:Tanzania Daima
No comments:
Post a Comment