
WASOMI
na baadhi ya wanasiasa wazalendo nchini wameunga mkono
msimamo wa Tanzania uliotolewa na Rais Jakaya Kikwete kuhusiana na chokochoko
zinazoanzishwa na Rwanda na wamemtaka Rais wa nchi hiyo, Paul
Kagame, kukaa meza ya mazungumzo na waasi wa nchi hiyo walioko Jamhuri ya
Kidemokrasia ya Kongo (DRC), kwani amani haiwezi kutafutwa kwa njia ya mtutu wa
bunduki.
Akizungumza na
MAJIRA kwa njia ya simu jana Mhadhiri wa Chuo cha St. Agustino, katika
kitivo cha sayansi ya siasa, Prof. Mwesiga Baregu, alisema ushauri alioutoa
Rais Kikwete kwa Rais Kagame ni mzuri, hauwezi kuleta athari zozote tofauti na
kutumia mtutu wa bunduki kukabili waasi.
"Mimi nikiwa kama mtaalam wa
kutatua migogoro suala la mazungumzo ni njia moja ambayo huwa inatumika mara
kwa mara na inasaidia kuleta amani," alisema na kuongeza;
"Kutumia mtutu wa bunduki haileti
tija kwa mataifa yote mawawili, hivyo ni busara itumike njia ya
mazungumzo."
Alitoa mwito kwa nchi jirani
kushirikiana kutatua mgogoro uliopo kwa njia ya mazungumzo baina ya Rwanda na
DRC.
Kwa upande wake Mkuu wa Kitivo cha
Elimu Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Dkt. Kitila Mkumbo, alisema
anakubaliana na kauli ya Rais Kikwete na anashangazwa na Rais Kagame ni kwa
nini anachukizwa kuambiwa azungumze na waasi
"Maana yake inaonekana hataki
kushauriwa...ushauri huo ni kitu kizuri kinaweza kuleta
maelewano," alisema Dkt. Mkumbo. Alisema Rais Kagame, anaonekana kama
dikteta kutokana na kukataa kuambiwa ukweli na viongozi wenzake.
Alisema kauli ya Rais Kikwete,
aliyoitoa kwenye hotuba yake ya mwisho wa mwezi wa saba hakugusia masuala ya
vita na anaamini kwamba kwa karne hii sio mwafaka nchi kuingia kwenye vita
kwani nchi zina matatizo mengi ambayo yanahitajika kupatiwa ufumbuzi.
"Alichoongea Rais Kikwete, ni
msimamo unaotakiwa kuungwa mkono na Watanzania kwani yeye ndiye Amiri Jeshi
Mkuu na hiyo ndiyo kauli ya nchi...hivyo alichosema ni sawa," alisema
Dkt. Mkumbo.
Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri,
Absalom Kibanda, alisema ameridhishwa na kauli ya Rais Kikwete, kwani ametumia
lugha sahihi katika kueleza hali halisi, hivyo Watanzania wote wanatakiwa
kumuunga mkono.
Alisema kwa hali ilivyo ni lazima
Watanzania waungane katika masuala kama hayo ili kuleta mshikamano wa
nchi.
Mwenyekiti wa Tanzania Labour Party
(TLP) Augustino Mrema, alisema anamuunga mkono Rais Kikwete, kwa kauli yake
hiyo.
Alisema Rais Kagame ameanza chokochoko
dhidi ya Tanzania na kwamba hivyo, ndivyo alivyoanza hata Idd
Amin. "Siungi mkono vita vitokee, lakini kama atatuchokoza basi tuwe
wa mwisho kujibu mapigo," alisema Mrema.
Aliyekuwa Mhadhiri UDSM, Dkt.
Azaveri Lweitama, amezitaka nchi za Afrika Mashariki kukaa chini ili kuangalia
jinsi ya kutatua mgogoro huo.
Alisema kuipiga Rwanda ni kazi ndogo
sana, lakini hauwezi kumaliza tatizo kwa kutumia bunduki na badala yake ni
vyema nchi hizo zikaangalia namna ya kumaliza mgogoro.
"Unajua mnaweza kuingia katika
vita mkamuondoa Rias wa Rwanda, lakini bado mkatengeneza matatizo mengine kwa
rais ajaye," alisema.
Alisema Kongo kuna waasi wa Rwanda na
hata Rwanda pia kuna waasi wa kutoka Kongo, hivyo ni lazima kutafuta njia nzuri
ya kutatua tatizo hilo.
Kwa upande mwingine, Dkt. Lweitama,
alivitaka vyombo vya habari kutopotosha taarifa zinazozungumzia vita vikitokea
hakuna mtu atakayebaki salama.
"Vyombo vya habari vijitahidi
kuandika habari zisizo za uchochoezi, kwani hata ninyi pia ni Watanzania,
naamini vita ikitokea hakuna mhariri wala mwandishi atakayebaki
salama," alisema.
Alisema vyombo vya habari pia vina
nafasi ya kukaa chini na kutafakari namna ya kumaliza mgogoro kwa kuwa vina
nafasi kubwa kwa mustakabali wa taifa.
Uhusiano wa Tanzania na Rwanda
unaelekea kupata mtikisiko baada ya Rais Kikwete kutoa ushauri kwa Serikali ya
Rwanda kuzungumza na mahasimu wao.
Rais Kikwete alitoa ushauri huo
kwa nia njema kwa kuwa bado anaamini kuwa kama jambo linaweza kumalizwa kwa
njia ya mazungumzo njia hiyo ni vyema itumike.
Ushauri ule aliutoa pia kwa Serikali ya
Kongo na kwa Serikali ya Uganda. ambapo katika mkutano ule Rais Yoweri Museveni
wa Uganda aliunga mkono kauli hiyo.
Tangu atoe ushauri huo viongozi wa
Rwanga wamekuwa wakitoa kauli za kejeli dhidi ya Tanzania na Rais Jakaya
Kikwete. Katika hotuba yake Rais Kikwete, alisema uhusiano wa Tanzania na
Rwanda unapitia katika kipindi kigumu
No comments:
Post a Comment