MBUNGE
wa Kigoma Kaskazini, Bw. Zitto Kabwe (CHADEMA), amesema hafikirii
kugombea urais kwa tiketi ya chama hicho wala ubunge katika Uchaguzi
Mkuu mwaka 2015.
Alisema
mwaka 2015, ndio mwaka wa mwisho kujihusisha na siasa ambapo dhamira
yake ni kutafuta chuo ambacho ataweza kufundisha masomo ya uchumi na
maliasili.
Bw. Kabwe aliyasema hayo hivi
karibuni katika mahojiano maalumu na gazeti hili siku chache baada ya
viongozi 105 kutoka Vyuo Vikuu 30 nchini, kupendekeza majina ya
wanasiasa wanaofaa kuwania urais mwaka 2015.
Jina la Bw. Kabwe, lilishika nafasi ya pili katika mchujo huo ambapo
Mbunge wa Bumbuli, mkoani Tanga ambaye pia ni Naibu Waziri wa
Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia, Bw. January Makamba, alishika nafasi
ya kwanza kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mwanasiasa aliyeshika
nafasi ya tatu katika mchujo huo alikuwa Mbunge wa Ubungo, Dar es
Salaam, Bw. John Mnyika (CHADEMA).
"Hiki ni kipindi cha mwisho kwangu kujihusisha na siasa kwani
nimechoka nazo, nitatafuta chuo nikafundishe na kama nitakosa ni bora
nikalime michikichi... sihitaji urais," alisema.
Katika mkutano wa wanafunzi hao, walisema Bw. Makamba ana sifa zote
za kuwa rais wa nchi kamaatagombea nafasi hiyo mwaka 2015 ili aweze
kulikomboa Taifa ambalo hivi sasa linakabiliwa na matukio mengi ya
uvunjifu wa amani.
Wanafunzi hao walikwenda mbali zaidi na kuyataja baadhi ya matukio
hayo kuwa ni pamoja na vurugu, kutekwa kwa watu wasio na hatia,
kufanyiwa vitendo vya ukatili, kumwagiwa tindikali na kupungua kwa
mtangamano wa kijamii.
Mwenyekiti wa mkutano huo ambao ulifanyika mkoani Morogoro ambaye pia
ni Rais wa Serikali ya Wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Mzumbe, Kampasi ya
Mbeya, Bw. Theonest Theophil, alisema Bw. Makamba alipata kura 72 ambapo
Bw. Kabwe alipata kura 20.
Bw. Theophil alisema sifa za kiongozi wanayemtaka kwanza awe kijana
mwenye fikra mpya, atakayeleta matumaini mapya, kuwaunganisha
Watanzania, asiyeendekeza siasa za kikanda, mdini na mkabila.
Sifa nyingine ni kiongozi mwadilifu asiye na rekodi ya kutuhumiwa
mahali popote kwa vitendo viovu, mtulivu, mwenye busara na anayepima
kauli zake.
Source: Majira
No comments:
Post a Comment