Waziri
Magufuli akizungumza na viongozi wa mkoa wa Iringa, idara ya ujenzi mkoa
wa Iringa na wataalamu mbalimbali kutoka wizara ya ujenzi na
miundombinu ya barabara.
WAZIRI wa ujenzi Mh. John Magufuli
amesema anafurahishwa sana na salamu ya chama cha demokrasia na
maendeleo, CHADEMA kwakuwa kila neno katika salamu hiyo lina maana kubwa
na linaashiria ushindi.Waziri Magufuli ameyasema hayo wakati akizungumza na viongozi wa sekta ya miundombinu ya barabara mkoa wa Iringa, katika kikao kilichofanyika katika ukumbi wa ofisi za mkuu wa mkoa wa Iringa dr. Christine Ishengoma, kwa madai kuwa neno "People" ni Watanzania waliompigia kura rais Jakaya Kikwete na akapata kura nyingi, "Power" likiwa ni neno linalomaanisha Nguvu, na kuwa hakuna mwenye nguvu zaidi ya rais.(P.T)
Akizungumzia juu ya nidhamu ya fedha, Magufuli amesema kumekuwa na matumizi yasiyostahili dhidi ya fedha za miradi ya barabara (Road Fund) huku baadhi ya wakurugenzi wakitumia fedha hizo kulipana posho za vikao mbalimbali, jambo ambalo linakwamisha vipaumbele vya wananchi.
Aidha Magufuli amesema Halmashauri za mkoa wa Iringa zitapatiwa zaidi ya shilingi Bilioni 5.6 ambazo zitasaidia kuboresha miundombinu ya barabara za Wilaya za mkoa huo, na hatua hiyo itasaidia kupunguza adha kwa wananchi.
Magufuli ameitaka Manispaa ya Iringa kubuni barabara za pembezoni ya mji huo ili kupunguza msongamano wa magari katika barabara kuu, kwa madai kuwa kukamilika kwa barabara ya Iringa -Dodoma - kutachangia msongamano mkubwa wa magari ya mikoa ya kusini na nje ya nchi, kama Cape town Afica Kusini, Zambia, Malawi nk.
Pia ameitaka Manispaa ya Iringa kujenga Kituo kikubwa cha mabasi ili kukabilina na msongamano wa magari katikati ya mji.
Akitoa ufafanuzi wa ujenzi wa barabara ya Iringa Dodoma, meneja wa wakala wa Barabara (Tanroad) mkoa wa Iringa Injinia Paul Ryakurwa amesema barabara ya kutoka Kihesa kilolo kupitia chuo kikuu cha Tuamaini, barabara yenye urefu wa km 7.3 itakuwa imekamilika mwishoni mwa mwezi huu Septemba.
"Mh. waziri mpaka mwisho wa mwezi barabara ya Kihesa Kilolo hadi Chuo kikuu cha tumaini tunakata milima ina urefu wa km 7.3, na kwa ujenzi unaofanywa ukijumlisha njia ya kupanda naza waenda kwa miguu Jumla ni km 12.3," Alisema Ryakurwa.
Naye mkuu wa mkoa wa Iringa Dr. Christine Ishengoma amemuomba waziri huyo kulichukulia uzito suala la upanuzi wa barabara ya Mlima Kitonga, kwa madai kuwa ufinyu wa barabara hiyo imekuwa ikichangia usumbufu mkubwa pindi magari yanapokwama na hivyo kuziba barabara hiyo na kusababisha msongamano mkubwa.
Majibu ya meneja huyo wa Tanroad injinia Ryakurwa ni ishara ya kuwa tayari mkoa wa Iringa umeanza kujiandaa kwa ujenzi wa barabara za pembezoni ili kuyafanya magari mengine yapite katika njia hizo mpya na kupunguza msongamano.
Ujenzi wa barabara ya Iringa- Dodoma yenye urefu wa km 261 inajengwa chini ya ufadhiri wa Jaica, Banki ya maendeleo ya Afrika (Africa development Bank), pamoja na serikali ya Tanzania huku ujenzi wa barabara hiyo ukigawanywa katika vipande vitatu, cha awali kikiwa na urefu wa km 95.2 ya pili 93.8 na kipande cha tatu kikiwa na urefu wa km 70.9.
No comments:
Post a Comment