WATU 15 WATIWA MBARONI KWA SHAMBULIO LA TINDIKALI HUKO ZANZIBAR
WATU 15 wanashikiliwa na polisi Zanzibar kwa tuhuma za kuhusika na
matumizi haramu ya tindikali. Kukamatwa kwa watu hao kunatokana na tukio
la mwishoni mwa wiki la kumwagiwa tindikali Padri wa Kanisa Katoliki
Parokia ya Machui, Joseph Mwang’amba katika maeneo ya Mlandege mjini
Zanzibar.
Kamanda wa Polisi wa Mjini Magharibi Zanzibar, Mussa Ali Mussa
hakutaka kutaja majina yao jana kwa vile uchunguzi unaendelea.
Alisema katika operesheni hiyo jeshi hilo linawahoji waliopata
vibali vya kuwa na tindikali wamepewa na nani waweze kuwakamata na
kuwafikisha katika vyombo vya sheria.
“Tunawaomba wananchi
waendelee kutuunga mkono katika mapambano haya kwa kutupa taarifa za
watu wanaojihusisha na uhalifu wa kutumia tindikali kwa kuwadhuru watu
wengine.
“Mapambano dhidi ya jinamizi la tindikali ni makubwa na
ni zaidi ya wengi wanavyofikiria. Tuvumiliane kwani upo uwezekano mkubwa
wa mapambono haya kuwahusu jamaa zetu na wakati mwingine hata viongozi
katika serikali,” alisema.
Alisema matukio yaliyopita ya
kuwamwagia tindikali watu wasiokuwa na hatia ikiwamo kesi ya Sheikh
Soraga, upelelezi wake umekamilika na jalada limefikishwa kwa mkurugenzi
wa mashtaka kwa ushauriwa sheria.
Kamanda Mussa alisema suala la raia wawili wa Uingereza upelelezi wake upo hatua za mwisho.
Alisema
jeshi la polisi kwa kushirikiana na ofisi ya mkemia mkuu na taasisi
nyingine imeanzisha operesheni maalum yenye lengo la kupunguza matumizi
holela ya tindikali nchini.
Kamanda alisisitiza kuwa operesheni hiyo itawalenga waingizaji tindikali nchini, wasambazaji, wauzaji na watumiaji holela.
Hata
hivyo, alisema bado kuna changamoto kubwa kuhusu udhibiti wa moja kwa
moja wa tindikali ikizimgatiwa inatumika katika viwanda na sehemu
nyingine za mitambo.
No comments:
Post a Comment