Mwenyekiti wa CHADEMA Arusha, Samson Mwigamba asimamishwa uongozi, baada ya kukiri kusema uongo

Mwenyekiti wa CHADEMA Mkoa wa Arusha, Ndugu Samson
Mwigamba amesimamishwa nafasi ya uongozi hiyo mara moja kuanzia leo na
Baraza la Uongozi la Kanda ya Kaskazini, huku taratibu zingine za
kinidhamu zikiendelea kwa kufuata katiba, kanuni, maadili, miongozo na
taratibu za chama.
Kikao hicho kimechukua hatua hizo mara moja baada ya Ndugu Mwigamba
kukiri kwa maandishi kuwa ameandika kwa kutumia jina bandia na kutuma
kwenye mitandao ya kijamii, kutoa tuhuma za uongo na kupotosha umma
dhidi ya chama na viongozi, kinyume na katiba, kanuni, maadili, miongozo
na taratibu za chama.
Hatua hiyo ya kukiri na kusimamishwa uongozi, ilifuatia baada ya Ndugu
Mwigamba kutuhumiwa kusambaza katika mitandao tuhuma za uongo,
upotoshaji na uchonganishi, ambapo kikao kilimwagiza kusalimisha
kompyuta yake ili wataalam wa masuala ya IT wa CHADEMA, Kanda ya
Kaskazini, waweze kufanya uchunguzi juu ya tuhuma hizo.
Wataalam hao wa masuala ya IT, wakitumia ushahidi uliokuwa katika
bandiko hilo, hasa jina la kiongozi huyo, walibaini pasi na shaka kuwa
andiko lililosambazwa kwenye mitandao ya kijamii, kwa kutumia jina
bandia liliandikwa na kuhifadhiwa kwenye kompyuta ya Mwigamba kisha
kupostiwa leo.
Ndugu Mwigamba ametuhumiwa kusambaza andiko hilo
akiwa katikati ya kikao, baada ya amemaliza kuwasilisha taarifa ya hali
ya chama katika mkoa wake wa Arusha, ambapo alikisifia chama na
uongozi wa taifa kwa kutekeleza maagizo ya vikao vya chama na kubuni
mipango na mikakati mbalimbali ya kukiendesha chama ili kuiondoa CCM
madarakani.
Kikao hicho cha Baraza la Uongozi, chini ya uenyekiti wa Mh. Israel
Natse, Mwenyekiti wa Kanda ya Kaskazini (Tanga, Manyara, Kilimanjaro na
Arusha), kiliazimia kwa kauli moja kumsimamisha Mwigamba, huku taratibu
zingine za kushughulikia masuala ya kinidhamu zikifuata.
No comments:
Post a Comment