ADV

ADV

ADVERTISEMENT CORNER

HUDUMA YA KUKATA TICKET ZA NDEGE ONLINE


SOMA HABARI

SOMA HABARI

Thursday, November 28, 2013

Tanzania, DRC, Burundi zaanzisha ushirikiano

Burundiclip_efd99.jpg
Wakati Kenya, Rwanda na Uganda zimeunda umoja unaoitwa 'Umoja wa Walio Tayari' , Tanzania, Burundi na Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo (DRC) nazo zimeanzisha ushirikiano baina yao.
Katika siku za karibuni kumekuwa na mtikisiko ndani ya Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) baada ya Tanzania na Burundi kutengwa na wenzao wa Kenya, Rwanda na Uganda katika baadhi ya masuala muhimu ya ushirikiano hasa wa kiuchumi.
Tanzania, Burundi na DRC nazo zimekutana ikiwa ni utekelezaji wa ahadi ya Waziri wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Samuel Sitta ambaye aliliambia Bunge lililopita kuwa Tanzania inafikiria kushirikiana na nchi hizo.
Mkutano wa ujirani mwema
Akizungumza na waandishi wa habari baada ya mkutano wa Ujirani Mwema uliofanyika mjini Bujumbura, Burundi jana, Sitta alisema Tanzania, Burundi na Kongo zimekubaliana kuendeleza miundombinu ya barabara, reli, anga na usafiri wa maji katika Ziwa Tanganyika.
Alisema mkutano huo ulilenga kuboresha miundombinu ya usafiri katika Ziwa Tanganyika ambalo linaziunganisha Burundi Tanzania, DRC na Zambia.
"Pia tumepanga kuendeleza reli ya kati kutoka eneo la Uvinza, Tanzania hadi Msongati, Burundi na pia kuunganisha Barabara ya Manyoni - Tabora - Kigoma kupitia Bujumbura hadi Kivu ya Kusini, DRC," alisema Sitta.
Mkutano huo ulihudhuriwa na Sitta pamoja na Waziri wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki wa Burundi, Leontine Nzeyimana na Waziri wa Uchukuzi wa DRC, Jack Lukeba.
"Pia tulitembelea Bandari ya Kalindo iliyoko katika Ziwa Tanganyika upande wa Burundi kwani tunataka kuboresha bandari za ziwa hilo," alisema Sitta.
Waziri huyo alisema Tanzania na Burundi zitaunganishwa na Barabara ya Manyoni – Tabora - Kigoma na Barabara ya Manyovu - Mgina, Mabanda - Bujumbura itakayounganishwa mpaka Kivu ya Kusini, DRC.
Kuhusu usafiri wa anga, Sitta alisema nchi hizo zinaangalia uwezekano wa kuanzisha safari za ndege za Dar es Salaam mpaka Bujumbura.
Muungano wa Walio Tayari
Marais Paul Kagame wa Rwanda, Uhuru Kenyatta wa Kenya na Yoweri Museveni wa Uganda wamefanya vikao vitatu mwaka huu kujadili ushirikiano miongoni mwa nchi zao ambao umepewa jina la Muungano wa Walio Tayari. Kwanza walikutana Juni 24 – 25, mjini Entebbe, Uganda kisha Agosti 28, mjini Mombasa, Kenya na Oktoba 28, mjini Kigali, Rwanda.
Katika vikao vyao iliamuliwa nchi hizo zishirikiane katika kuboresha miundombinu, uanzishwaji wa himaya moja ya ushuru wa forodha, uhamiaji na kuundwa kwa shirikisho kisiasa.
Tanzania yaja juu
Akilihutubia Bunge Novemba 7, mwaka huu mjini Dodoma, Rais Jakaya Kikwete alieleza Tanzania kutofurahishwa na nchi hizo kuanzisha umoja huo na kuitenga bila ya kuwapo kwa sababu za msingi.
Alisema nchi hizo za Kenya, Uganda na Rwanda zimekuwa zikidai kuwa Tanzania haikuwa tayari kutekeleza mambo ya ushirikiano wa EAC ndiyo maana zikaamua kuanzisha ushirikiano baina yao.
Alisema jambo hilo si la kweli huku akidokeza kwamba huenda sababu za nchi hizo kuchukua hatua hiyo ni kutokana na kutofautiana kimsimamo na Tanzania katika masuala ya ardhi, ajira na uhamiaji.
Rais Kikwete alisema nchi hizo zilikuwa zinavunja mkataba wa EAC kwa kukubaliana kushirikiana katika baadhi ya maeneo yaliyokubaliwa na jumuiya.
Aliliambia Bunge kuwa nchi hizo zilikuwa zimekubaliana maeneo manane lakini kati ya hayo, manne yalikuwa yanatakiwa kushughulikiwa ndani ya EAC.
Chanzo:Mwananchi

No comments:

Post a Comment

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...