WAKATI Chama Cha Demokrasia na Maendeleo
(CHADEMA) kikimwandikia Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe barua
ya kumtaka ajieleze dhidi ya tuhuma zinazomkabili, yeye ameamua
kukimbilia polisi akimshitaki mmoja wa viongozi wenzake.
Habari za kuaminika zimedai kuwa Zitto
ambaye hivi karibuni alivuliwa cheo chake cha unaibu katibu mkuu wa
CHADEMA, inadaiwa amefungua mashitaka polisi akimtuhumu Katibu wa
CHADEMA Mkoa wa Dar es Salaam, Henry Kileo kwa madai ya kusambaza waraka
katika mitandao ya kijamii.
Akithibitisha tukio hilo, wakili wa
Kileo, Peter Kibatara, alisema kuwa mteja wake amemriwa kufika makao
makuu ya Jeshi la Polisi leo Jumatano saa nane mchana na kuonana na
mmoja wa maofisa wa juu wa jeshi hilo, aliyetajwa kwa jina moja tu la
Mbutta, kufuatia mashitaka yaliyofunguliwa na Zitto dhidi yake.
Akizungumza kwa njia ya simu na
mwandishi wetu, Kileo alikiri kuitwa polisi, ingawa alidai hajui ni
waraka gani anaotuhumiwa kuusambaza unaomchafua Zitto.
“Kwa kweli sijui hata mimi ni waraka
gani, ingawa hivi karibuni kulikuwa na waraka wa siri uliodaiwa kutoka
CHADEMA, na ambao ulijaa tuhuma za usaliti. Lakini huo tuliishaukana
siku nyingi. Labda kuna mwingine,” alisema Kileo.
Zitto kutwa nzima ya jana hakuweza
kupatikana kwa njia ya simu kufafanua mashitaka aliyofungua polisi. Simu
zake zote za kiganjani zilikuwa zimezimwa.
No comments:
Post a Comment