ADV

ADV

ADVERTISEMENT CORNER

HUDUMA YA KUKATA TICKET ZA NDEGE ONLINE


SOMA HABARI

SOMA HABARI

Friday, December 20, 2013

hawana uchungu na wananchi, itakuwa tembo

african-elephant 435 600x4501 b66f7
SERIKALI kupitia kwa Waziri wa Maliasili na Utalii, ilitangaza kusitisha 'Operesheni Tokomeza' baada ya wabunge kuituhumu operesheni hiyo kuwa inakiuka misingi ya ubinadamu. Operesheni hiyo ilianzishwa na Serikali kwa ajili ya kuwasaka na kuwatokomeza majangili ambao wamekuwa wakijihusisha na bishara ya meno ya tembo, ambayo inatishia uhai wa tembo nchini kutokana na kuongezeka kwa ujangili huo. (HM)


Operesheni hiyo ilikuwa ikiwahusisha maofisa wa usalama wa taifa, polisi na kikosi cha kupambana na ujangili ndani ya Wizara ya Maliasili na Utalii.
Katika kipindi ilichofanya kazi, operesheni hiyo ilifanikiwa kuwakamata majangili sugu waliokuwa wakijihusisha na mtandao wa kuhujumu tembo wetu, ambapo pia ilibainika kuwa mtandao huo wa ujangili tembo ulikuwa ukiwahusisha vigogo na wafanyabiashara wakubwa hapa nchini wenye ukwasi wa kutosha.
Kilio kilichotolewa na wabunge wetu ndani ya Bunge kumeonyesha ni namna gani wabunge wa Tanzania wasivyo makini katika kutekeleza majukumu yao na wako mbele kutetea maslahi yao binafsi na kikundi cha watu wachache ambacho kimekuwa kikiwawezesha katika kampeni zao za ubunge katika majimbo yao.
Wabunge kadhaa waliamua kuipinga operesheni hiyo kwa madai kuwa operesheni hiyo imekiuka haki za binadamu kutokana na mateso waliyokuwa wakiyapata wananchi waliokuwa wakikamatwa pia walilalamikia kuwa baadhi ya maofisa katika operesheni hiyo waliua mifugo kama ng'ombe na mbuzi na wananchi wasio na hatia.
Katika suala la mauaji ya wananchi wasio na hatia, maofisa waliokuwa wakiendesha operesheni hiyo katika maeneo mbalimbali walikuwa na taarifa rasmi na zisizotiliwa shaka kuwa watu fulani wanashiriki katika kuwaua tembo wetu na wamekuwa wakimiliki silaha kinyume cha sheria ambazo wamekuwa wakizitumia kufanikisha ujangili wao huo.
Katika mazingira ya namna hiyo ni jambo la kawaida kwa wahusika katika operesheni hiyo kuchukua tahadhari mapema kabla ya kuwafikia wahusika ambao ndio hao hao wamekuwa wafadhili wa fedha na michango mbalimbali katika kampeni za wabunge.
Nawapa pole wananchi ambao walifariki katika operesheni tokomeza na ni vyema vyombo vya dola vikachunguza na kuwachukulia hatua maofisa ambao walisababisha vifo vya wananchi wasio na hatia katika operesheni hiyo.
Pia tunawapa pole wananchi wote ambao walipoteza mifugo yao na mali zao kadha wa kadha katika operesheni hiyo ambapo tunaitaka Serikali ihakikishe inaandaa utaratibu maalumu wa kushughulikia matatizo yaliyowapata wananchi hao na kuangalia namna ya kuwafidia japo nusu ya mali walizopoteza.
Kama alivyozungumza Rais Jakaya Kikwete wakati akihutubia Bunge kuwa operesheni hiyo ilikuwa muhimu katika kuhakikisha taifa linatokomeza ujangili katika mbuga zetu za wanyama na mapori ya akiba ili kulinda wanyama asili.
Pia Rais Kikwete aliwataka wabunge kuwaelimisha wananchi juu ya madhara ya kuingia katika mbuga za wanyama pamoja na mapori ya akiba ili kuepuka madhara mbalimbali ambayo yanaweza kuwapata pindi wanapokutana na askari wa wanyama pori.
Wakichangia katika mjadala huo juu ya kusitisha operesheni tokomeza baadhi ya wabunge walionyesha chuki binafsi dhidi ya Waziri wa Maliasili na Utalii, Khamis Kagasheki pamoja na Serikali kwa ujumla badala ya kujadili hoja.
Baadhi ya wabunge wetu katika siku za hivi karibuni wamejikita zaidi katika kupambana na kila jambo jema linalofanywa na viongozi wa Serikali kwa kisingizio cha kuwatetea wananchi, huwezi ukajitoa mhanga kuwatetea wananchi wakati wewe mwenyewe ndie kikwazo cha wananchi kupata maendeleo.
Wabunge wetu siku hizi hawakai majimboni wala hawafanyi ziara majimboni kwao kwa kuogopa kuombwa fedha na wananchi ambao waliwapatia kura ili waweze kula, wapiga kura wamebaki kama watoto yatima.
Wabunge wetu ili wasikike kuwa wanawatetea wananchi wamekuwa wakilitumia Bunge letu tukufu kama sehemu ya kujionyesha kwa wapiga kura wao kuwa wapo na wanawatetea ili hali wabunge hao baadhi yao wana miezi zaidi ya sita hawajaonekana katika majimbo yao ya uchaguzi.
Wawakilishi hao wa wananchi wamekimbilia katika majiji na miji mikubwa pamoja na familia zao, wamekuwa wakipiga kelele kupitia luninga wakiwa bungeni au kwa kuitisha mikutano na waandishi wa habari na kutoa dukuduku lao basi, hawataki kuonana na wananchi wao wala kuyajua yanayowasibu.
Ukiwauliza wabunge wetu kuwa ni mara ngapi wanayoyazungumza bungeni wametumwa na wapiga kura wao baada ya kufanya mikutano kabla ya kwenda bungeni kwa ajili ya kupata maoni na matatizo ambayo yanawakabili.
Asilimia kubwa ya mambo ambayo wabunge wetu wanayazungumza bungeni hayana uhusiano na mambo ya wapiga kura wao, mengi yanayozungumzwa na wabunge wetu ni hisia na mawazo yao binafsi na wakati mwingine huwatumikia wenye fedha katika masuala mbalimbali ambayo wenye fedha wanahitaji msukumo wa Bunge. Chanzo: Mtanzania

No comments:

Post a Comment

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...