TAARIFA YA KAMATI YA KUDUMU YA BUNGE YA ARDHI, MALIASILI NA MAZINGIRA
 KUHUSU TATHMINI YA MATATIZO YALIYOTOKANA NA OPARESHENI TOKOMEZA ; 
 1.0 UTANGULIZI
 Mheshimiwa Spika, wakati Bunge likijadili hoja ya kuahirisha shughuli 
za Bunge ili kujadili jambo muhimu la dharura kwa mujibu wa Kanuni ya 47
 ya Kanuni za Kudumu za Bunge, Toleo la 2013, iliyowasilishwa na Mhe. 
Said Nkumba, Mbunge wa Sikonge kuhusu Mgogoro kati ya Wafugaji na 
Wakulima, Hifadhi na Uwekezaji, Mheshimiwa Spika alitoa Uamuzi ‘Speakers
 Ruling’ kuwa Kamati ya Ardhi, Maliasili na Mazingira ishughulikie kazi 
ya kutathmini na kuangalia jinsi Mpango wa Kupambana na Majangili 
ulivyopangwa na kutekelezwa na Serikali kupitia ‘Operesheni Tokomeza’. 
 Kwa mujibu wa kumbukumbu za Taarifa Rasmi za Bunge za tarehe 1 Novemba 
2013, wakati Bunge likihitimisha Hoja ya Kuairisha Shughuli za Bunge, 
Mhe. Spika alitoa uamuzi ufuatao:- 
 …Kamati ile ya kawaida ya 
Maliasili itaendelea na kazi yake ya kufanya tathmini ya kuangalia jinsi
 mpango ule wa Kupambana na Majangili ulivyopangwa na ndani yake 
itashughulikia kama kulikuwa na uzembe ama kuna watu wanahusika katika 
kuondoa maisha ya watu kwa sababu za uzembe … 
 1.1 Kuundwa kwa Kamati Ndogo ya Uchunguzi
 Mheshimiwa Spika, kufuatia uamuzi ulioutoa tarehe 01 Novemba, 2013 
Kamati ya Ardhi, Maliasili na Mazingira, ilikutana Dodoma tarehe 9 
Novemba, 2013 kwa lengo la kujadili utaratibu wa kutekeleza jukumu hilo.
 Katika kikao hicho Kamati iliazimia kuunda Kamati Ndogo kwa mujibu wa 
Kanuni ya 117(18), ya Kanuni za Kudumu za Bunge, Tole la 2013 ili iweze 
kushughulikia suala hilo kikamilifu. 
 1.2 Hadidu za Rejea, Wajumbe wa Kamati na muda wa kazi
 Mheshimiwa Spika, Kamati Ndogo ya Ardhi, Maliasili na Mazingira 
iliyoundwa na Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Mazingira
 kwa agizo lako la tarehe 01 Novemba, 2013, ilipewa Hadidu za Rejea Nne 
(4) zifuatazo:- 
 1) Kutathmini na kuangalia jinsi Mipango ya Kupambana na Majangili ilivyopangwa; 
 2) Kuangalia kasoro zilizojitokeza katika kutekeleza mpango huo; 
 3) Kutathmini iwapo kulikuwa na uzembe katika kutekeleza Operesheni 
Tokomeza ambao ulisababisha watu wasio na hatia kupoteza maisha na mali 
zao; na 
 4) Kuchunguza migogoro ya Ardhi inayohusu Wakulima, Wafugaji na Wawekezaji kwenye maeneo yanayozunguka hifadhi.
 Mheshimiwa Spika, Kamati hii ya uchunguzi iliundwa na Wajumbe Tisa (9) kama ifuatavyo:- 
 i. Mhe. James Daudi Lembeli, Mb.
 ii. Mhe. Abdulkarim Esmail Shah, Mb.
 iii. Mhe. Susan Limbweni Kiwanga, Mb.
 iv. Mhe. Kaika Sanin’go Telele, Mb.
 v. Mhe. Dk. Henry Daffa Shekifu, Mb.
 vi. Mhe. Amina Andrew Clement, Mb.
 vii. Mhe. Haji Khatibu Kai, Mb.
 viii. Mhe. Muhammad Amour Chomboh, Mb.
 ix. Mhe. Dk. Mary Mwanjelwa 
 Mheshimiwa Spika, Sekretarieti iliyohudumia Kamati Ndogo ya Uchunguzi iliundwa na Wajumbe wafuatao:-
 i. Ndg. Theonest K. Ruhilabake
 ii. Ndg. Gerald S. Magili
 iii. Ndg. Chacha T. Nyakega
 iv. Ndg. Stanslaus W.Kagisa 
 Mheshimiwa Spika, Kamati Ndogo ya Ardhi, Maliasili na Mazingira 
ilitakiwa kutekeleza majukumu yake na kuwasilisha ripoti katika Mkutano 
wa Kumi na Nne (14) wa Bunge. Hivyo basi, baada ya uteuzi huo, Wajumbe 
wa Kamati Ndogo walipanga kuanza kazi tarehe 25 Novemba, 2013 na 
kuikamilisha ifikapo tarehe 15 Desemba, 2013. 
 1.3 Njia zilizotumika katika kukamilisha kazi
 Mheshimiwa Spika, Kamati Ndogo ya Ardhi, Maliasili na Mazingira 
ilitekeleza majukumu yake kwa kuongozwa na Hadidu za Rejea ilizopewa kwa
 kufanya rejea na kuzingatia yafuatayo:- 
 a) Kusoma na kuchambua
 nyaraka zilizoandaliwa na Wizara ya Maliasili na Utalii katika kuandaa 
na kutekeleza Operesheni Tokomeza nchini. Nyaraka hizo ni hizi 
zifuatazo:-
 i. Mpango Kazi wa Operesheni Tokomeza (Concept Paper)
 ii. Tathmini ya Utekelezaji wa Operesheni Tokomeza.
 iii. Sheria ya Kinga, Maadili na Madaraka ya Bunge (Na.3) 1988
 iv. Sheria ya Wanyamapori (Na. 5) 2009
 v. Kanuni za Kudumu za Bunge, Toleo la mwaka 2013 
 b) Kufanya mahojiano na watu mbalimbali:-
 i. Waziri wa Maliasili na Utalii
 ii. Katibu Mkuu Wizara ya Maliasili na Utalii
 iii. Mkurugenzi wa Idara ya Wanyamapori
 iv. Mkurugenzi Msaidizi Kikosi wa Dhidi ya Ujangili
 v. Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi
 vi. Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Hifadhi za Taifa (TANAPA)
 vii. Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro (NCAA)
 viii. Mkurugenzi Mtendaji wa Wakala wa Hifadhi za Misitu (TFS)
 ix. Mahojiano na baadhi ya Waheshimiwa Wabunge 
 c) Kuzuru maeneo yaliyoanishwa katika Taarifa ya Wizara kuhusiana na 
utekelezaji wa Operesheni Tokomeza na yale yenye migogoro kati ya 
Wakulima au Wafugaji na Wawekezaji katika maeneo ya hifadhi kwa lengo la
 kuhakiki (verify) masuala yaliyoainishwa kupitia uchambuzi uliofanywa 
na Kamati. 
 2.0 KUPOKEA NA KUCHAMBUA NYARAKA MBALIMBALI ZILIZOHUSU OPERESHENI TOKOMEZA 
 Mheshimiwa Spika, Hadidu Rejea ya kwanza iliitaka Kamati Ndogo ya 
Ardhi, Malisili na Mazingira, kufanya tathmini na kuangalia jinsi 
mipango ya kupambana na majangili ilivyopangwa. Ili kukamilisha jukumu 
hilo, Kamati ilifanya yafuatayo:- 
 a) Kupitia na kuchambaua Mpango Kazi wa Operesheni Tokomeza (Concept Paper) ulioandaliwa na Wizara
 b) Kupitia na kuchambua Tathmini ya Utekelezaji wa Operesheni Tokomeza. 
 2.1 Uchambuzi kuhusu Mpango Kazi wa Operesheni Tokomeza
 Mheshimiwa Spika, katika kuchambua Mpango Kazi wa Operesheni Tokomeza 
kwa lengo la kupata uelewa zaidi wa namna operesheni hiyo ilivyopangwa 
na kutekelezwa, Kamati ilibaini kuwa, mpango huo uliandaliwa na Wizara 
ya Maliasili na Utalii na ulikuwa na mambo yafuatayo:- 
 i. Ukubwa wa tatizo la ujangili
 ii. Aina za ujangili na sababu za ukuaji wake
 iii. Maeneo yaliyoathiriwa zaidi na ujangili
 iv. Malengo ya Operesheni Tokomeza
 v. Njia zilizotumika kutekeleza operesheni
 vi. Maeneo ya operesheni na gharama za utekelezaji
 vii. Tamko la Serikali kusitisha Operesheni Tokomeza 
 2.1.1 Ukubwa wa tatizo la ujangili
 Mheshimiwa Spika, Kamati ilibaini kuwa, tatizo la ujangili ni kubwa na 
limekuwa likisababisha idadi ya Tembo iendelee kupungua nchini. Takwimu 
zinaonesha kuwa, idadi ya Tembo imepungua kutoka 350,000 (miaka ya 1970)
 hadi kufikia 55,000 (mwaka 1989). Juhudi za kukabiliana na hali hiyo 
kupitia Operesheni zilizowahi kutekelezwa huko nyuma zilisaidia kuongeza
 idadi ya
 Tembo hadi 141,000 (mwaka 2006) ingawa ilishuka tena hadi kufikia 110,000 (mwaka 2009). 
 2.1.2 Aina za ujangili na sababu za ukuaji wake
 Mheshimiwa Spika, kwa mujibu wa Taarifa ya Serikali, vitendo vya 
ujangili vinavyofanyika nchini vimegawanyika katika makundi mawili 
yafuatayo:- 
 i. Ujangili wa Kujikimu (subsistance poaching)
 
Aina hii ya ujangili inahusisha watu wenye kipato kidogo na hulenga 
zaidi katika kujipatia kitoweo na fedha kwa ajili ya kukidhi mahitaji 
mengine. Ujangili wa aina hii huathiri zaidi wanyama wanaoliwa na si 
Tembo. 
 ii. Ujangili wa Biashara (commercial poaching)
 Aina 
hii ya ujangili inahusisha zaidi watu wenye uwezo mkubwa wa kifedha na 
hulenga kupata nyara zenye thamani kubwa. Wanyama wanaoathiriwa zaidi na
 aina hii ya ujangili ni pamoja na Tembo, Faru, Simba na Chui. 
 
Mheshimiwa Spika, taarifa ilibainisha kuwa, kuongezeka kwa masoko haramu
 katika nchi za Asia na Mashariki ya Kati ambayo yanatoa bei kubwa ya 
nyara hizo, imekuwa ni chachu ya kuimarika kwa mitandao inayojihusisha 
na ujangili (ndani na nje ya nchi) na hivyo kusababisha ongezeko kubwa 
la vitendo vya ujangili. 
 2.1.3 Maeneo yaliyoathiriwa zaidi na ujangili
 Mheshimiwa Spika,Mpango Kazi waKupambana na Ujangili ulilenga kujikita 
katika maeneo yaliyoathiriwa zaidi na ujangili wa wanyamapori na misitu.
 Mpango huo ulioelezewa kuwa niwa muda mrefu na kusimamiwa na kikosi 
kazi cha Taifa (national task force),umeanisha maeneo yafuatayo kuwa 
ndiyo yaliyoathirika zaidi:- 
 i. Pori la Akiba Selous
 ii. Hifadhi ya Taifa Serengeti, Pori la Akiba Maswa na Pori Tengefu la Loliondo.
 iii. Hifadhi ya Taifa Katavi na Mapori ya Akiba Rukwa na Lukwati.
 iv. Hifadhi ya Taifa Mikumi
 v. Hifadhi ya Ngorongoro na Hifadhi za Taifa Tarangire na Ziwa Manyara.
 vi. Mapori ya Akiba Burigi, Biharamuro, Ibanda na Rumanyika.
 vii. Mapori ya Akiba Moyowosi, Kimisi, Ugalla na Hifadhi ya Misitu Luganzo. 
 2.1.4 Malengo ya Operesheni Tokomeza
 Mheshimiwa Spika, Operesheni Tokomeza ambayo ilizinduliwa rasmi tarehe 04 Oktoba, 2013 ilikuwa na malengo yafuatayo:- 
 i. Kuzuia vitendo vya ujangili ndani na nje ya Hifadhi za Taifa, Mapori
 ya Akiba, Mapori Tengefu, Mamlaka ya Hifadhi Ngorongoro na Misitu ya 
Hifadhi na kufanya operesheni maeneo yote yaliyoathiriwa na ujangili. 
 ii. Kuwatambua mapema majangili na kujua nyendo zao ndani na nje ya maeneo ya hifadhi. 
 iii. Kuwakamata na kuwafikisha kwenye vyombo vya sheria wafanyabiashara haramu wa nyara za Serikali na mazao ya misitu. 
 iv. Kuvunja mitandao ya wafadhili, wanunuzi wadogo na wakubwa pamoja na
 mawakala wa biashara haramu ya nyara za Serikali na mazao ya misitu. 
 v. Kufuatilia na kukamata mali za majangili zilizotokana na biashara haramu ya nyara za Serikali na mazao ya misitu. 
 2.1.5 Njia zilizotumika kutekeleza Operesheni Tokomeza
 Mheshimiwa Spika, Kamati ilibaini kuwa, Mpango Kazi wa Serikali 
kuhusiana na Operesheni Tokomeza, uliainisha kuwa operesheni hiyo 
itaendeshwa kwa kutekeleza mambo yafuatayo:- 
 i. Kufanya 
uchambuzi wa kina wa watuhumiwa wa mtandao wa ujangili wa nyara za 
Serikali na wavunaji na wasafirishaji haramu wa mazao ya misitu. 
 ii. Kuwakamata watuhumiwa wote waliobainishwa kwenye taarifa za kiintelijensia. 
 iii. Kupiga picha na kuchora ramani ya eneo la tukio kwa kila mtuhumiwa (sketch map). 
 iv. Kuhoji na kuandika maelezo ya watuhumiwa wa ujangili wa nyara za 
Serikali na wavunaji na wasafirishaji haramu wa mazao ya misitu. 
 v. Kukusanya na kuhifadhi vielelezo vyote vitakavyokamatwa kutoka kwa majangili kwa ajili ya kujenga ushahidi mahakamani. 
 vi. Kuandika maelezo ya mashahidi na askari wakamataji kwa ajili ya kujenga ushahidi mahakamani. 
 vii. Kuandaa mashitaka dhidi ya watuhumiwa na kuwapeleka mahakamani ili sheria ichukue mkondo wake. 
 2.1.6 Maeneo ya Operesheni na gharama za utekelezaji
 Mheshimiwa Spika,Mpango Kazi wa Operesheni Tokomeza ulianisha kuwepo 
awamu mbili za utekelezaji ambazoni; Mpango Kazi wa Muda Mfupi na Mpango
 Kazi wa Muda Mrefu. 
 Katika Mpango Kazi wa Muda mfupi 
itafanyika operesheni maalum katika maeneo yote ya ndani na nje ya 
hifadhi za wanyamapori na misitu nchi nzima. Maeneo hayo yaligawanywa 
katika kanda 12 za utekelezaji kama ifuatavyo:- 
 i. Selous, Mikumi, Udzungwa, Lukwika/ Lumesule na Liparamba,
 ii. Burigi/Biharamuro, Ibanda/Rumanyika na Rubondo,
 iii. Moyowosi, Ugalla na Lugazo,
 iv. Serengeti, Loliondo, Maswa, Ikorongo na Kijeshi,
 v. Kilimanjaro, Arusha, Mkomazi/Umba, Simanjiro na Longido,
 vi. Tarangile, Manyara, Karatu/Ngorongoro, Swagaswaga na Mkungunero,
 vii. Rungwa, Ruaha, Mpanda – Kipengele,
 viii. Rukwa, Lukwati, Katavi, Lwafi, Piti na Wembere,
 ix. Mahale na Gombe,
 x. Saadani na kwenye maeneo yenye misitu ya mikoko,
 xi. Pori Tengefu la Handeni, Kilindi na Mkinga na
 xii. Msitu wa Kazimzumbwi, Kisarawe, Rufiji na Mkuranga, 
 Mheshimiwa Spika, ilianishwa kuwa, awamu ya kwanza ya Mpango Kazi wa 
muda mfupi ingegharimu jumla ya Tshs. 3,968,168,667/= ambazo 
zingechangwa na Taasisi za wanyamapori (WD, TANAPA, NCAA na TFS) kwa 
kila moja jumla ya Tshs. 992,042,167/= 
 2.1.7 Tamko la Serikali kusitisha Operesheni
 Mheshimiwa Spika, kufuatia michango na malalamiko ya Waheshimiwa 
Wabunge wakati wakichangia hoja iliyotolewa na Mhe. Said Nkumba Mbunge 
wa Sikonge, pamoja na maagizo ya Bunge kutaka Serikaliitoe maelezo 
kuhusu hoja zilizotolewa na Waheshimiwa Wabunge, Serikali ilitoa Tamko 
la kusitisha Operesheni Tokomeza tarehe 01 Novemba, 2013. 
 2.2 Uchambuzi wa Taarifa ya awali ya Utekelezaji wa Operesheni Tokomeza
 Mheshimiwa Spika, taarifa hii ya awali kuhusiana na utekelezaji wa Operesheni Tokomeza ilikuwa na mambo yafuatayo:-
 i. Washiriki wa operesheni
 ii. Awamu za operesheni
 iii. Mafanikio ya operesheni
 iv. Idadi ya watuhumiwa na kesi zilizofunguliwa
 v. Changamoto za operesheni 
 2.2.1 Washiriki wa Operesheni
 Mheshimiwa Spika, Operesheni Tokomeza ilihusisha jumla ya washiriki 
2,371 kutoka vyombo vya Ulinzi na Usalama kwa mgawanyo ufuatao:- 
 i. Wanajeshi (885) kutoka Jeshi la Wananchi wa Tanzania,
 ii. Askari (480) kutoka Jeshi la Polisi,
 iii. Askari (440) kutoka Kikosi Dhidi ya Ujangili (KDU)
 iv. Askari Wanyamapori (383) kutoka Shirika la Hifadhi za Taifa (TANAPA)
 v. Askari (99) kutoka Wakala wa Huduma za Misitu (TFS)
 vi. Askari Wanyamapori (51) kutoka Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro (NCAA)
 vii. Waendesha Mashitaka (23) na
 viii. Mahakimu (100) 
 2.2.2 Awamu za Operesheni
 Mheshimiwa Spika, Operesheni Tokomeza ilipangwa kutekelezwa katika awamu Nne (4) kama ifuatavyo:-
 i. Awamu ya kwanza ambayo ililenga kusaka Silaha za Kivita na Meno ya 
Tembo kutoka miongoni mwa wanaojihusisha na vitendo vya ujangili.
 
ii. Awamu ya pili ambayo ililenga kusaka silaha zisizomilikiwa kihalali 
na zile zinazomilikiwa kihalali lakini zinasadikiwa kutumika kwenye 
vitendo vya ujangili.
 iii. Awamu ya tatu, ambayo ililenga kutafuta 
yalipo Maghala ya Nyara, kusaka Wafadhili na Wanunuzi wa nyara hizo na 
kuwabaini watu wanaowakingia kifua wahusika wa vitendo vya ujangili.
 iv. Awamu ya nne, ambayo ililenga kukamata Nyara nyingine mbali na Meno
 ya Tembo na kuhakikisha watu walio katika makundi yafuatayo 
wanakamatwa:-
 - Wawindaji haramu,
 - Wavunaji haramu wa mazao ya misitu,
 - Watu wanaolisha Mifugo ndani ya hifadhi, na
 - Watu waliojenga ndani ya maeneo ya hifadhi 
 2.2.3 Mafanikio ya Operesheni Tokomeza 
 a) Idadi ya watuhumiwa na kesi zilizofunguliwa
 Mheshimiwa Spika, tangu kuanza kutekelezwa kwaOperesheni Tokomeza 
(tarehe 04 Oktoba, 2013 hadi ilipositishwa (tarehe 01 Novemba, 2013) 
jumla ya kesi 687 zilifunguliwa zikiwahusisha watuhumiwa 1,030 katika 
maeneo yote kama ifuatavyo:-
 i. Kanda ya Kwanza kesi 105 zikiwahusisha watuhumiwa 105
 ii. Kanda ya Pili kesi 370 ambazo zilihusisha watuhumiwa 375
 iii. Kanda ya Tatu kesi 165 zilizohusisha watuhumiwa 498
 iv. Kanda ya Nne kesi 47 zilizohusisha watuhumiwa 52 
 Mheshimiwa Spika, hadi wakati Operesheni Tokomeza inasitishwa tarehe 01
 Novemba, 2013 kati ya Kesi 687 zilizokuwa zimefunguliwa ni 132 tu ndiyo
 zilikuwa zimetolewa maamuzi na 555 bado zilikuwa katika hatua ya 
kusikilizwa. (Tazama Kiambatisho Na. 1) 
 i. Kukamatwa kwa meno 
ya Tembo 211 yenye uzito wa kilo 522, meno ya Ngiri 11, Mikia ya wanyama
 mbalimbali 36, Ngozi za wanyama mbalimbali 21, Pembe za Swala 46, 
Mitego ya wanyama 134, ng’ombe 7,621 Baiskeli 58, Pikipiki 8 na Magari 
9. 
 ii. Kupungua kwa kasi ya mauaji ya Tembo kutoka wastani wa 
Tembo wawili (2) kwa siku hadi tembo wawili tu katika kipindi chote cha 
operesheni (siku 29). 
 iii. Hadi kufikia tarehe 11 Novemba, 2013
 jumla ya Bunduki za Kijeshi 18 zilikamatwa, Bunduki za kiraia 1579, 
Risasi 1964, Mbao vipande 27,913, Mkaa Magunia 1242, Magogo 858 na 
Misumeno 60. Vyote hivyo vilikamatwa katika Kanda ya Nne. 
 2.2.4 Changamoto za Operesheni Tokomeza 
 a) Vifo vilivyotokea wakati wa Operesheni
 Mheshimiwa Spika,Taarifa ya Serikaliiliainisha vifo kamachangamoto 
kubwa iliyojitokeza wakati wautekelezaji wa Operesheni Tokomeza kutokana
 na watumishi 6 na watuhumiwa 13 kupoteza maisha. (Tazama Kiambatisho 
Na. 2) 
 b) Hujuma dhidi ya Operesheni
 Mheshimiwa Spika, 
taarifa ya Serikali ilifafanua kuwa,utekelezaji wa Operesheni Tokomeza 
ulikumbwa na vitendo vya hujuma kutoka kwa baadhi ya makundi ya jamii 
kama ifuatavyo:-
 i. Mamluki miongoni wa washiriki wa Operesheni. 
Mfano; kukamatwa kwa Askari Polisi na Askari Wanyamapori wakisindikiza 
gari lenye Meno ya Tembo, na gari la Serikalikutumika kusafirisha Meno 
ya Tembo.
 ii. Vyombo vya Habari kutumika kuvuruga operesheni 
kwakueneza propaganda zilizolenga kushawishi wananchi kupinga operesheni
 hiyo.
 iii. Baadhi ya wamiliki wa silaha kutuhumiwa kutoa silaha zao ili zitumike kwa ajili ya vitendo vya ujangili. 
 C) Tuhuma dhidi ya Operesheni
 Mheshimiwa Spika, taarifa ya Serikai ilifafanua kuwa,ingawa lengo la 
operesheni lilikuwa ni kupambana na vitendo vya ujangili dhidi ya 
raslimali za Taifa, utekelezaji wake ulikumbwa na tuhuma kadhaa zikiwemo
 zifuatazo:-
 i. Mateso dhidi ya watuhumiwa yaliyosababisha maumivu, 
kupata ulemavu wa kudumu na hata wengine kupoteza maisha (Mfano; 
Marehemu Emiliana Gasper Maro wa Gallapo – Babati).
 ii. Matumizi mabaya ya Silaha (Mfano; Mzee wa miaka 70 kuuawa kwa kupigwa risasi 3).
 iii. Nyumba za wananchi kuchomwa moto (Mfano; Kijiji cha Kabage Wilaya ya Mpanda – Katavi).
 iv. Mifugo kuuawa kikatili kwa kuchomwa moto na kupigwa risasi (Mfano; Ng’ombe 60 kuuawa kwakupigwa risasi).
 v. Kukosekana kwa mwongozo wa utoaji wa taarifa jambo lililosababisha 
viongozi husika wa Serikali kutopewa taarifa muhimu za utekelezaji wa 
Operesheni. (Mfano; Waziri wa Maliasili naUtalii, Waziri wa Mambo ya 
Ndani ya Nchi, Waziri wa Ulinzi na Wakuu wa Mikoa na Wilaya).
 vi. Askari waliotuhumiwa kukiuka taratibu kukataa kutoa ushirikiano wa kutosha pale walipohitajika kufanya hivyo.
 vii. Kutoshirikishwa kwa viongozi wa Mamlaka za Utawala katika ngazi za Mikoa na Wilaya. 
 3.0 MAHOJIANO BAINA YA KAMATI NA WIZARA PAMOJA NA WABUNGE
 Mheshimiwa Spika, Kamati ilifanya mahojiano na makundi yafuatayo:-
 i. Wizara ya Maliasili na Utalii pamoja na Taasisi zake
 ii. Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi
 iii. Waheshimiwa Wabunge 
 3.1 Mahojiano baina ya Kamati na Wizara ya Maliasili na Utalii pamoja na Taasisi zake 
 Mheshimiwa Spika, ili kuhakikisha wajumbe wa Kamati wanapata uelewa wa 
kutosha kuhusiana na Operesheni Tokomeza, Kamati liagiza uongozi wa 
Wizara ya Maliasili na Utalii ukiongozwa na Waziri, kufika mbele ya 
Kamati ili kueleza namna Operesheni Tokomeza ilivyoandaliwa na 
kutekelezwa hadi ilipositishwa kupitia tamko la Serikali lililotolewa 
Bungeni tarehe 01 Novemba, 2013. 
 Mheshimiwa Spika, Kamati 
ilikutana na Waziri wa Maliasili na Utalii pamoja na timu yake kwa siku 
tatu, tarehe 28- 29 Novemba, na tarehe 01 Desemba, 2013. Katika vikao 
hivyo, Waziri aliieleza Kamati juu ya Mpango Kazi wa Operesheni 
Tokomeza, raslimali (watu na fedha) pamoja na tathmini iliyofanyika kwa 
kipindi ambacho Operesheni Tokomeza ilitekelezwa. 
 Mheshimiwa 
Spika, katika mahojiano na Waziri wa Maliasili na Utalii Mhe. Balozi 
Khamis Kagasheki, Mb na watendaji wake Kamati ilifahamishwa yafuatayo:- 
 i. Kwamba Operesheni Tokomeza ilikuwa ya kijeshikama alivyonukuliwa 
katika Taarifa Rasmi za Bunge (Hansard) akisema: “…Operesheni ilikuwa ya
 kijeshi. Ilikuwa ya kijeshi kwa sababu ilitekelezwa kwa amri ya jeshi 
Namba 0001/13 iliyotolewa tarehe 28 Septemba, 2013 na kusainiwa na Mkuu 
wa Majeshi ya Ulinzi…” 
 ii. Kwamba, kinadharia inaonekana 
kwamba, Waziri wa Maliasili na Utalii ndiye alikuwa Msemaji Mkuu, lakini
 kiuhalisia hakuwa msemaji mkuu wa Operesheni Tokomeza kama 
alivyonukuliwa katika Taarifa Rasmi za Bunge akisema; “…kinadharia 
inaweza ikasemekana kwamba mimi ndiye msemaji mkuu, lakini mimi sikuwa 
msemaji mkuu wa Operesheni Tokomeza …” 
 iii. Utekelezaji wa Operesheni Tokomeza ulisimamiwa na Jeshi la Wananchi wa Tanzania. 
 iv. Taarifa za mwenendo wa operesheni zilikuwa zinapelekwa moja kwa 
moja kwa Mkuu wa Majeshi na kwamba, hazikumfikia Waziri wa Maliasili na 
Utalii. 
 v. Operesheni Tokomeza iliingiliwa na Wanasiasa. 
 vi. Pamoja na Mpango kazi huo kuandaliwa na Wizara ya Maliasili na 
Utalii, kwa namna ambayo haieleweki Waziri hakuuona wala kuidhinisha 
rasimu ya mwisho ya Mpango huo. Hiyo ilidhihirika mbele ya Kamati 
kutokana na Waziri kukiri kwamba hakuuona wala kuudhinisha 
 3.1.1 Tathmini ya Kamati kuhusu majibu ya Waziri wa Maliasili na Utalii pamoja na watendaji wa Wizara 
 Mheshimiwa Spika,kwa kutumia tathmini ya awali ya nyaraka 
zilizowasilishwa pamoja na mahojiano na Waziri ilionekana kwamba, 
Operesheni Tokomeza iliandaliwa na Wizara ya Maliasili na Utalii kwa 
kushirikiana na taasisi zilizo chini yake na kushirikisha vyombo vya 
Ulinzi na Usalama. 
 Mheshimiwa Spika, licha Mpango wa Operesheni
 Tokomeza kuandaliwa na Wizara ya Maliasili na Utalii, hata hivyo 
utekelezaji wake ulisimamiwa na kuongozwa na Jeshi la Wananchi wa 
Tanzania. 
 Hatua ya jeshi kuchukua jukumu la kuongoza Operesheni
 Tokomeza, lilifanya viongozi wa Wizara kujiengua katika jukumu la 
kuongoza (ead agency) na badala yake kuacha jukumu hilo kwa Jeshi pekee 
jambo lililotafsiriwa kwamba, Operesheni Tokomeza ilikuwa ya kijeshi. 
 Mheshimiwa Spika, kupitia mahojiano ilibainika kwamba, hakukuwa na 
utaratibu mzuri wa kupashana habari kuhusiana na mwenendo mzima wa 
Operesheni Tokomeza jambo lililofanya baadhi ya wahusika kutotambua 
kikamilifu wajibu waokatika Operesheni hiyo.Mfano mzuri ni kwamba, licha
 ya kuelezwa kwenye Kanuni za Utendaji (Operational Guidelines)za 
Operesheni Tokomeza kwamba, Waziri wa Maliasili na Utalii ndiye atakuwa 
Msemaji Mkuu wa Operesheni Tokomeza, bado Mhe. Waziri hakutekeleza 
jukumu hilokwani alikwishatoa mapendekezo katika rasimu kwamba Msemaji 
Mkuu awe ni Mkurugenzi wa Wanyamapori. 
 Aidha, Kamati ilibaini 
kuwa baadhi ya Watendaji wa juu wa Wizara walidaiwakukwamishautekelezaji
 wa maagizo ya Waziri wa Maliasili na Utalii kutokana na kuingilia 
mawasiliano aliyokuwa anayafanya na baadhi ya Watumishi. Mfano ni 
majibizano kwa njia ya barua pepe kati ya Waziri na Katibu Mkuu, Waziri 
na Mkurugenzi wa Wanyamapori na pia Katibu Mkuu na Mkurugenzi wa 
Wanyamapori. Kwa mujibu wa majibizano hayo Waziri anaonekana kushangazwa
 na hatua ya Katibu Mkuu kuhoji hatua ya yeye kumuita mmoja wa mtumishi 
wa Wizara ofisini kwake. (Kiambatisho Na. 3) 
 Mheshimiwa Spika, 
kukosekana kwa mfumo mzuri wa kupashana habari kwa pande husika kuhusu 
mwenendo mzima wa Operesheni Tokomeza, kulionekana kuathiri utaratibu 
mzima wa viongozi husika akiwemo Waziri wa Maliasili na Utalii, kupata 
taarifa zinazotakiwa kwa wakati. Hali hiyo ilichangia utekelezaji wa 
Operesheni Tokomeza kukumbwa na athari ambazo zingeweza kuepukika iwapo 
kungekuwa na mfumo mzuri wa mawasiliano. 
 Mheshimiwa Spika, 
kupitia mahojiano pia Kamati ilibaini uwepo wa hujuma kutoka kwa 
viongozi wa kisiasa na Serikali ambao kwa namna moja au nyingine 
walionekana kuhusishwa na Operesheni Tokomeza ama wao binafsi au ndugu 
zao. 
 Mheshimiwa Spika, miongoni mwa hujuma ambazo Kamati 
ilizibaini kupitia mahojiano naWaziri wa Maliasili na Utalii na 
Watendaji wake ni pamoja na:-
 i. Baadhi ya watuhumiwa wenye 
mahusiano na viongozi wa kisiasa kutumia majina ya viongozi hao 
kuingilia utekelezaji wa Operesheni Tokomeza. 
 ii. Baadhi ya Waheshimiwa Wabunge kutuhumiwa kujihusisha navitendo vya ujangili na biashara haramu ya nyara za Serikali. 
 iii. Baadhi ya Mawaziri kutoa kauli zenye kuingilia utekelezaji wa 
Operesheni Tokomeza. (Mfano: kutoa maelekezo kwa wahusika wa Operesheni 
Tokomeza kwamba wasiguse viongozi wa kisiasa wa ngazi zote). 
 
iv. Baadhi ya viongozi wavyombo vya Ulinzi na Usalama kushiriki 
kudhoofisha utekelezaji wa Operesheni Tokomeza kwa kusindikiza au 
kusaidia watuhumiwa wa ujangili kutoroka. (Mfano; viongozi wa Polisi wa 
Wilaya na Mikoa) 
 Mheshimiwa Spika, kubainika kwa hujuma hizo ni
 ishara tosha kwamba hata ndani ya Serikali yenyewe hakukuwa na dhamira 
ya dhati kwa baadhi ya kwa viongozi na watendaji katika kuhakikisha vita
 dhidi ya vitendo vya kijangili inapiganwa kikamilifu. 
 Hali 
hiyo ilisababisha utekelezaji wa operesheni kukumbwa na athari nyingi 
kama vile; wananchi kupoteza maisha, mifugo kuuawa kwa kuchomwa moto, 
njaa, kiu au kupigwa risasi), upotevu wa mali, nyumba kuchomwa moto na 
vitendo vya ukatili dhidi ya wananchi ambavyo vilikiuka haki za 
kibinadamu. Hali hiyo imesababisha utekelezaji wazoezi la Operesheni 
Tokomeza kutafsiriwa kwamba ulilenga wananchi wasio na hatia na kuacha 
wahusika wa ujangili. 
 3.2 Mahojiano baina ya Kamati na Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi
 Mheshimiwa Spika, mnamo tarehe 30 Novemba, 2013 Kamati ilikutana na 
kufanya mahojiano na Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi ili kubaini namna 
ilivyoshiriki katika Operesheni Tokomeza. 
 Waziri wa Mambo ya 
Ndani ya Nchi Mhe. Dk. Emmanuel Nchimbi, Mb alieleza kuwa, operesheni 
hii ilikuwa na lengo la kutimiza azma (Commitment) ya Serikali iliyoitoa
 Bungeni kwamba, inakusudia kufanya Operesheni ya kupambana na 
majangili. Wizara yake ilishiriki kwa kutoa Askari Polisi 504 pamoja na 
baadhi ya vyombo vya usafiri na kwamba vyombo vya Ulinzi na Usalama vya 
nchi vilikuwa vikikutana mara kwa mara kwa lengo la kuandaa mkakati wa 
namna ya kushirikiana katika kutekeleza mpango huo wa vita dhidi ya 
ujangili. 
 Mheshimiwa Spika,Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi 
alikiri kuwa, licha ya lengo la operesheni kuwa zuri, kulijitokeza 
changamoto kadhaa zilizotokana na baadhi ya washiriki wa operesheni 
kwenda kinyume na malengo yaliyokusudiwa kama vile; ukatili dhidi ya 
mifugo na vitendo vya unyanyasaji wa wananchi kwa kuwatesa kiasi cha 
kuwasababishia ulemavu wa kudumu au vifo. 
 Pia Mheshimiwa Waziri
 alikiri kwamba, kutokuwepo mfumo mzuri wa mawasiliano na Operesheni 
kuongozwa na jeshi, iliashiria kwamba taarifa za operesheni zilikuwa 
zinakwenda kwa Mkuu wa Majeshi – CDF moja kwa moja na hivyo kufanya 
pande zingine zinazohusika zisijue kinachoendelea. 
 3.2.1 Tathmini ya Kamati kuhusu majibu ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi na watendaji wake 
 Mheshimiwa Spika, Kamati ilibaini kuwepo kwamawasiliano hafifu kati ya 
Wizara ya Maliasili na Utalii na Wizara nyingine zilizoshiriki katika 
operesheni hii.Pia,kukosekana kwa mfumo mzuri wa mawasiliano, 
kuliikosesha Wizara ya Maliasili na Utalii ambayo iliandaa na kugharamia
 Operesheni Tokomeza,fursa ambazo zingeiwezesha kufanya tathmini kuhusu 
utekelezaji wa Operesheni hii. 
 Aidha, Kamati ilibaini kwamba, 
hatua ya kutoshirikisha Kamati za Ulinzi na Usalama za Wilaya ililenga 
kutovujisha siri dhidi ya watuhumiwa wa ujangili. Hatua hiyo 
ilisababisha usumbufu mkubwa kwa viongozi wa mamlaka za utawala za 
Wilaya na Mikoa kutokana na kulaumiwa na wananchi kwa kushindwa 
kuwasaidia pale walipokumbwa na matatizo. 
 3.3 Mahojiano baina ya Kamati na Waheshimiwa Wabunge
 Mheshimiwa Spika, kwa kuwa suala hili liliibukia Bungeni baadaya 
wawakilishi wa wananchi kupaza sauti kuhusu athari zilizowakumba wapiga 
kura wao, Kamati iliona ni busara kuhoji baadhi ya Waheshimiwa Wabunge 
waliochangia hoja hii. Wabunge hao walitoa taarifa muhimu kuhusu vitendo
 vilivyofanyika katika maeneo yao wakati wa operesheni. 
 
Mheshimiwa Spika, Waheshimiwa Wabunge walieleza kusikitishwa na namna 
ambavyo Operesheni Tokomeza ilikiuka malengo yaliyokusudiwa na badala 
yake ikanyanyasa wafugaji kwa kuangamiza mifugo yao na kuwaharibia mali 
zao kama vile; kuchoma moto nyumba, kupora fedha na vitu vingine. Mbunge
 mmoja alinukuliwa katika Taarifa Rasmi za Bunge akisema:-
 “…badala ya Operesheni Tokomeza kusaka majangili, ikageuka kuwa Operesheni Tokomeza Ufugaji…” 
 Mheshimiwa Spika, Waheshimiwa Wabunge waliieleza Kamati kuwa, siyo 
jambo la kawaida kwa watu wanaoagizwa kufanya jambo fulani kwenda 
kinyume na maagizo. Wakashauri kuwa, wahusika wote waliotenda kinyume 
namaagizo wachukuliwe hatua stahiki ili kuepusha vitendo vya aina hiyo 
visijirudie katika operesheni zitakazofuata. Pia Waheshimiwa Wabunge 
walishauri kasoro zilizojitokeza zirekebishwe na operesheni iweze 
kuendelea ili kutowapa mwanya majangili kujipanga upya. 
 3.3.1 
Tathmini ya Kamati kuhusu majibu ya Waheshimiwa Wabunge Mheshimiwa 
Spika, kimsingi Waheshimiwa Wabunge wanaunga mkono Operesheni Tokomeza 
ambayo ililenga kukomesha vitendo vya kijangili na kunusuru raslimali za
 nchi hasa wanyamapori na misitu. Hata hivyo, walieleza kusikitishwa na 
vitendo vilivyojitokeza wakati wa utekelezaji wa operesheni na walisema 
haviwezi kuvumilika. 
 Mheshimiwa Spika, baada ya kupata taarifa 
mbalimbali kutoka kwa Waheshimiwa Wabunge, mahojiano na viongozi na 
watendaji wa Wizara na kuzingatia taarifa zilizowasilishwa na Serikali, 
Kamati iliazimia kuzuru baadhi ya maeneo yaliyoathiriwa na Operesheni 
Tokomeza ili kufanya uhakiki. 
 4.0 KAMATI KUZURU MAENEO YALIYOATHIRIKA KWA AJILI YA KUHAKIKI (VERIFICATION/OUTREACH) 
 Mheshimwa Spika, kutokana na wingi wa maeneo pamoja na ufinyu wa muda, 
Kamati ilijigawa katika makundi matatu ili yaweze kutembelea baadhi ya 
maeneo yaliyoainishwa katika Taarifa ya Serikali ili kufanya tathmini 
(verification) kwa utaratibu ufuatao:- 
 4.1 Kundi la kwanza 
lilielekea Kanda ‘C’iliyohusisha maeneo yaliyoathiriwa na Operesheni 
Tokomeza katika Mikoa ya Shinyanga, Kagera, Tabora, Kigoma, Rukwa, 
Katavi na Singida. 
 Mheshimiwa Spika, kundi hili liliundwa na Wajumbe wafuatao:-
 Mheshimiwa James Daudi Lembeli, Mb, Mheshimiwa Haji Khatibu Kai, Mb na Mheshimiwa Susan Limbweni Kiwanga, Mb. 
 4.2 Kundi la pili lilielekea Kanda ‘B’iliyohusisha maeneo 
yaliyoathiriwa na Operesheni Tokomeza katika Mikoa ya Simiyu, Mara, 
Arusha na Manyara.
 Mheshimiwa Spika,kundi hili liliundwa na wajumbe 
wafuatao, Mheshimiwa Abdulkarim E. Shah, Mb, Mheshimiwa Henry Daffa 
Shekifu, Mb na Mheshimiwa Amina Andrew Clement, Mb. 
 4.3 Kundi 
la tatu lilielekea Kanda ‘D’iliyohusisha maeneo yaliyoathiriwa na 
Operesheni Tokomeza katika Mikoa ya Pwani, Morogoro, Iringa, Ruvuma na 
Mtwara. 
 Mheshimiwa Spika, kundi hili liliundwa na wajumbe 
wafuatao; Mheshimiwa Kaika Saning’o Telele, Mb, Mheshimiwa Muhammad 
Amour Chomboh, Mb na Mheshimiwa Dkt. Mary Mwanjelwa, ambaye hata hivyo 
hakushiriki kutokana na dharura. 
 Mheshimiwa Spika,kama 
ilivyoainishwa hapo juu lengo la Kamati kutawanyika Mikoani lilikuwa 
kutathmini athari zilizotokana na Operesheni Tokomeza ambayo iliendeshwa
 nchini kuanzia tarehe 04 Oktoba, 2013 hadi tarehe 01 Novemba, 2013. 
 Mheshimiwa Spika, ili kutimiza jukumu hilo kikamilifu, Kamati iliongozwa na taarifa zifuatazo;
 i. Mpango Kazi wa Operesheni Maalum ya kupambana na Ujangili nchini,
 ii. Taarifa ya Utekelezaji wa Operesheni Tokomeza iliyotolewa na Serikali.
 iii. Michango ya Waheshimiwa Wabunge kama ilivyonukuliwa katika Taarifa Rasmi za Bunge (Hansard).
 iv. Madai yaliyotolewa na Wabunge kuhusiana na athari zilizotokana na utekelezaji wa Operesheni Tokomeza.
 v. Maelezo yaliyotolewa na Mashahidi ambao walihojiwa na Kamati.
 vi. Vielelezo vilivyowasilishwa na Mashahidi waliofika mbele ya Kamati. 
 5.0 MAKUNDI YA KAMATI YALIVYOTEKELEZA MAJUKUMU YAKE
 Mheshimiwa Spika, katika kutekeleza jukumu hili, Kamati ilikutanana makundi yafuatayo:-
 i. Kamati za Ulinzi na Usalama za Mikoa na Wilaya
 ii. Waheshimiwa Madiwani
 iii. Waathirika wa Operesheni Tokomeza 
 5.1 Kamati za Ulinzi na Usalama za Mikoa na Wilaya
 Mheshimiwa Spika, Kamati ilikukutana na Kamati za Ulinzi na Usalama za 
Mikoa na Wilaya na kupokea taarifa iliyohusu hali ya Ulinzi na Usalama 
hususan wakati wa utekelezaji wa Operesheni Tokomeza.
 Mheshimiwa 
Spika, kwa sehemu kubwa taarifa za Ulinzi na Usalama za Wilaya 
zilisaidia kuanisha maeneo na matukio yaliyojiri wakati wa Operesheni 
Tokomeza na athari zilizojitokeza. Wajumbe wa Kamati walitumia uchambuzi
 wa taarifa hizo kupata uelewa zaidi kuhusiana na utekelezaji wa 
Operesheni hiyo kabla ya kukutana na wananchi walioathirika ili kupata 
maelezo zaidi. 
 5.2 Waheshimiwa Madiwani
 Mheshimiwa 
Spika,katika baadhi ya Wilaya, Kamati ilikutana nabaadhi ya Madiwani 
wakiwa ni wawakilishi wa wananchi katika ngazi ya halmashauri ili kupata
 maelezo zaidi kuhusu utekelezaji wa Operesheni Tokomeza kabla ya 
kukutanana waathirika wa Operesheni. 
 5.3 Waathirika wa Operesheni Tokomeza
 Mheshimiwa Spika, Kamati ilikutana nabaadhi ya wananchi walioathirika 
na Operesheni Tokomeza na kupokea maelezo na malalamiko yao kuhusu namna
 walivyoathiriwa na uekelezaji wa Operesheni.
 Mheshimiwa Spika, wapo
 baadhi ya waathirika walitoa ushahidi/vielelezo vya maandishi na picha 
ili kuthibitisha yale waliyokuwa wakiyaeleza mbele ya Kamati. Wengine 
walikwenda mbali kiasi cha kuonesha majerahana makovu waliyoyapata 
katika miili yao kutokana na mateso waliyopata kwenye kambi maalum za 
mahojiano zilizoandaliwa na waendeshaji wa Operesheni Tokomeza. 
 5.4 Kuzuru maeneo yaliyoathirika zaidi na Operesheni
 Mheshimiwa Spika, Kamati ilipata fursa ya kutembelea baadhi ya maeneo 
yaliyokumbwa na athari za operesheni Tokomeza kwa lengo la kushuhudia 
mabaki ya vielelezo ili kujiridhisha iwapo tuhuma za athari zilizotolewa
 kuhusu maeneo hayo zilikuwa zakweli. 
 6.0 YALIYOBAINIKA KATIKA ZIARA ZA KAMATI 
 6.1 Vikao na Kamati za Ulinzi na Usalama za Mikoa/Wilaya
 Mheshimiwa Spika, katika vikaona Kamati za Ulinzi na Usalama za Mikoa/ 
WilayaKamati ilibaini kuwa utekelezaji wa Operesheni Tokomeza 
haukushirikisha viongozi wa maeneo hayo ya utawala. 
 Kulikuwa na
 manung’uniko kwamba licha ya Wakuu wa Wilaya na Mikoa kuwa wawakilishi 
wa Rais, waliachwa kando na Operesheni kuendeshwa katika maeneo 
wanayosimamia hadi malalamiko ya wananchi waliokamatwa yalipowafumbua 
macho kwamba walikuwa wanateswa na kufanyiwa vitendo vya udhalilishaji 
na watekelezaji wa Operesheni. Aidha,
 Kamati ilielezwa kwamba 
utekelezaji wa Operesheni Tokomeza ulisababisha hofu miongoni mwa 
wananchi na viongozi na kusababisha baadhi yao kukimbia makazi. Mfano; 
Mkuu wa Wilaya ya Ulanga alikiri kujihifadhi kwenye Hoteli moja nje ya 
Wilaya yake ambako alikutana na baadhi wananchi wake waliokimbia adha za
 Operesheni Tokomeza. 
 Viongozi hao walieleza kwamba, kimsingi 
hawapingi Operesheni Tokomeza Majangili kwaniililenga kunusuru raslimali
 za nchi hasa wanyamaporina misitu visitoweke kutokana nakushamiri kwa 
vitendo vya ujangili. Hata hivyo, walieleza kuwa hatua ya 
kutowashirikisha imelifanya zoezi hilo kuwa na kasoro nyingi pamoja na 
udhalilishaji hata kwa viongozi waliochaguliwa na wananchi. 
 6.2 Vikao vya Kamati na Waathirika wa Operesheni Tokomeza
 Mheshimiwa Spika, Kamati ilifanya mikutano mbalimbali katika baadhi ya 
maeneo ilikofanyika Operesheni Tokomezakwa lengo la kuwasilikiliza 
waathirika na kubaini mambo yafuatayo:- 
 Watuhumiwa kupekuliwa, kudhalilishwa na baadhi kutojulikana walipo
 i. Mheshimiwa Spika, badhi ya wananchi wakiwemo viongozi, Madiwani na 
Wenyeviti wa Vijiji na Vitongoji na Watumishi wa Serikali walikamatwa na
 kudhalilishwa mbele ya wananchi wanaowaongoza. Baadhi ya watuhumiwa 
waliokamatwa walikuwa hawajulikani walipo hadi Kamati ilipozuru maeneo 
hayo. Mfano; Vijana watatu wa Kijiji cha Osteti, Kata ya Chapakazi, 
Wilayani Kiteto, walituhumiwa kujihusisha na biashara ya Meno ya Tembo. 
Vijana hao ni Nyafuka Ng’onja, Ng’onja Kipana na Mswaya Karani. 
 ii. Baadhi ya watuhumiwa waliokamatwa walidai kudhalilishwa mbele ya 
wanafamilia kwa kupewa adhabu wakiwa uchi na wanawake kushikwa sehemu za
 siri bila ridhaa yao. Mfano; ndugu Ali Nyenge (38) wa Kata ya Iputi, 
Wilaya ya Ulanga alidai kuvuliwa nguo, kumwagiwa maji yaliyochanganywa 
na chumvi na kuchapwa viboko huku mwanae wa kiume (11) akishuhudia. 
 Pia alidai kulazimishwa kuchora picha ya Chatu kwa kutumia wembe kwenye
 paja lake. Vilevile, Bi. Neema Moses wa Babati alidai kuvuliwa nguo na 
kulazimishwa afanye mapenzi na wakwe zake na pia kuingizwa chupa sehemu 
zake za siri. 
 Aidha, baadhi ya akina mama walidai kubakwa na 
kulawitiwa. Mfano; katika Kata ya Iputi, Wilaya ya Ulanga, mwanamke 
mmoja alidai kubakwa na Askari wawili (2) wa Operesheni Tokomeza 
Ujangili mida ya usiku. Vilevile, mama mmoja mkazi wa Kata ya Matongo 
Wilayani Bariadi, alibakwa na askari watatu (3) wa Operesheni Tokomeza 
Ujangili huku akiwa ameshikiwa mtutu wa bunduki 
 iii. Watuhumiwa
 waliokamatwa walifanyiwa upekuzi bila kuhusisha viongozi wa Serikali za
 maeneo husika na kutokuwepo kwa mashahidi na hati za upekuzi. 
 
Mfano; Ndg. Abdallah Pata naBi. Flora Mwarabu wa Kata ya Iputi Wilayani 
Ulanga na Ndg. Elias Cosmas Kibuga wa Gallapo Babati, walipekuliwa bila 
kufuata utaratibu. 
 Ukatili na Udhalilishaji katika Kambi za Mahojiano
 iv. Mheshimiwa Spika, baadhi ya watuhumiwa waliopelekwa katika kambi za
 mahojiano walidai kutwezwakwa adhabu zinazokiuka haki za binadamu. 
Mfano; Diwani wa Kata ya Sakasaka wilaya ya Meatu Ndg. Peter Samwel, 
alidai kuadhibiwa akiwa mtupu kwa kupewa adhabu za kijeshi kama 
kuning’inizwa kichwa chini miguu juu, kupigwa kwa vyuma na kulazimishwa 
kufanya mapenzi na mti. 
 Mheshimiwa Spika, kutokana naukatili 
uliopitiliza, baadhi ya kambi za mahojiano zilipewa majina kama vile 
Guantanamo (Ruaha), Goligota (Ngorongoro), Duma na Andajega (Serengeti). 
 Upotevu wa mali za watuhumiwa na faini zisizoeleweka
 v. Mheshimiwa Spika, ilidaiwa kuwa wakati wa utekelezaji wa Operesheni 
TokomezaUjangili, baadhi ya watuhumiwa walipoteza mifugo, mali na fedha 
zao. Mfano; katika Wilaya ya Ulanga Kata ya Iputimwananchimmoja alidai 
kuporwa sanduku la VICOBA lenye shilingi laki saba na nusu (750,000/=) 
pamoja na simu ya mkononi na Askari wa Operesheni Tokomeza waliovamia 
nyumbani kwake. Vilevile Ndugu Musa Masanja wa Sakasaka Wilaya ya Meatu,
 alidai kuporwa shilingi laki tatu 300,000/= pamoja na simu 2 za mkononi
 na Askari Askari wa Operesheni. 
 Mheshimiwa Spika,Pia ilidaiwa 
kuwa mifugo ya watuhumiwa ilikamatwa na kuingizwa ndani ya maeneo ya 
hifadhina kufa kwa kupigwa risasi au kukosa maji na malisho kutokana na 
kuzuiliwa kwa muda mrefu. 
 Baadhi ya mifugo ilitozwa faini bila 
stakabadhi au stakabadhi kuonesha viwango vidogo ikilinganishwa na fedha
 halisi iliyolipwa. Mfano:Ndugu Sosoma Shimula mwenye Ng’ombe 1700 
Wilayani Kasulu alidai kwamba alitakiwa kulipa faini ya shilingi Milioni
 thelathini (30,000,000/=, alipowasihi alipunguziwa hadi Milioni kumi na
 mbili (12,000,000/=) hata hivyo aliweza kulipa Milioni kumi 
(10,000,000/=). 
 Alionesha Kamati stakabadhi inayoonesha kuwa 
amelipa faini ya shilingi milioni moja tu (1,000,000/=). Stakabadhi hiyo
 ilijazwa sehemu ya tarakimu, lakini hakuna kilichoandikwa katika sehemu
 ya kiasi cha fedha kwa maneno. (Tazama Kiambatisho Na. 4) 
 Watuhumiwa kuteswa na kuumizwa
 vi. Mheshimiwa Spika, baadhi ya watuhumiwa walidai kupigwa na kuumizwa 
na askari wa Operesheni na wengine kupata ulemavu wa kudumu. Mfano; 
katika Wilaya ya Itilima,Kijiji cha Mbogo NdgSita Rumala alidai kupigwa 
na kuvunjwa mkono alionesha wajumbe mkono uliokuwa umefungwa bandeji 
ngumu (P.O.P). 
 Aidha, Diwani Peter Samwel Ndekija wa Kata ya 
Sakasaka, Wilaya ya Meatu, alidai kupigwa na kuumizwa vibaya mgongoni na
 alionesha kwa wajumbe wa Kamati makovu aliyoyapata. Vilevile,ilielezwa 
kuwa Ndugu Munanka Machumbe (24) ambaye ni bubu alipigwa risasi 
3zilizomjeruhi mapajani na kuharibu sehemu za siri wakati akijaribu 
kuwahoji Askari wa Operesheni kwa ishara sababu za kumtesa baba yake. 
 Aidha, katika tuko lingine Shekhe Mkuu wa Wilaya ya Ulanga Ali Mohamed 
(70) aishiye kijiji cha Iputi, alidai kurushwa kichura na 
kutandikwabakora na Askari wa Operesheni Tokomeza.Pia,Ndg. Nyasongo 
Magoro Serengeti waKata ya Majimoto wilaya ya Mulele alidhalilishwa 
mbele ya wananchi wake. (Tazama Kiambatisho Na. 5) 
 Mifugo kuingizwa hifadhini nawatuhumiwa kubambikwa kesi
 vii. Mheshimiwa Spika,wakati wa Operesheni, mifugo mingi ilikuwa 
hifadhinilakini hata ile iliyokuwa nje ya hifadhi iliingizwa na askari 
wa hifadhi na wafugaji kutakiwa walipe faini ya shilingi Milioni tatu 
(3,000,000/=) hadi Sita (6,000,000/=) kwa idadi ya ng’ombe 30 hadi 
ng’ombe 100 na aliyeshindwa kulipa faini mifugo yake iliuawa au kupigwa 
mnada na mfugaji kufilisiwa. 
 Walioshindwa kulipa faini mifugo 
ilipigwa mnada na wafugaji hawakuruhusiwa kununua wala kukaribia eneo la
 mnada, na katika mnada mifugo iliuzwa kwa bei ya chini kuliko faini 
iliyotozwa Mfano; shilingi elfu sitini (60,000/ kwa kila ng’ombe. 
 Watuhumiwa kubambikwa kesi
 viii.Ilidaiwa kwamba, baadhi ya watuhumiwa walidai kubambikwa makosa 
ambayo hawahusiki nayo kama vile kumiliki silaha kinyume na sheria, 
kukutwa na bangi au nyara za Serikalimfano; Bw. Elias Cosmas Kibuga wa 
Gallapo Babati alidai kubambikiwa kesi ya kumiliki bunduki kukutwa na 
mkia wa twiga kinyume cha sheria. 
 Mheshimiwa Spika, pia Bibi 
Zuhura Ali wa Kilombero alidai kuteswa huku akilazimishwa kutoa silaha 
ambayo hakuwa nayo. Aidha, Bw. Melkzedeck Abraham Sarakikya wa Itigi 
alidai kuteswa akilazimishwa atoe silaha. 
 Mateso na vifo kwa Watuhumiwa
 ix. Mheshimiwa Spika, baadhi ya wananchiwalidai kuwa ndugu zao 
waliteswa kikatili kwa muda mrefuna bila kupatiwa huduma za lazima kama 
chakula, maji na matibabu (siku 1 -2) hadi mauti yalipowafika. Kwa 
mfanoNdg. Kipara Issa wa Wilaya ya Kaliua na ndugu Emiliana Gasper Maro 
wa Gallapo, Wilaya ya Babati. 
 Aidha, wananchi hao walidaikuwa 
mahojiano kwa watuhumiwa yaliambatana na mateso makali kwa muda mrefu 
kiasi cha kusababisha vifo. (Tazama Kiambatisho Na. 6). 
 
Vilevile, watuhumiwa wengine waliodaiwa kupoteza maisha wakati wa 
Operesheni Tokomeza ni Ndg. Wegesa Kirigiti wa Kijiji cha Remagwe na 
Ndg. Peter Masea wa Kijiji cha Mrito (Tarime), Ndg. Mohamed Buto 
(Masasi) na Gervas Nzoya (Kasulu). 
 Mheshimiwa Spika, pamoja na 
uthibitisho wa picha zilizotolewa na wananchi kuhusu kuteswa hadi kufa 
kwa Bi Emiliana Gasper Maro, Serikali kupitia Mkurugenzi wa Wanyamapori 
ilitoa Taarifa kwa Umma ikipinga Taarifa iliyorushwa na kituo cha 
luninga cha ITV tarehe 19 Oktoba 2013 kuhusu mauaji ya kutisha 
yaliyofanywa na Askari wa kupambana na ujangili. 
 Taarifa hiyo 
ya Serikali inapinga kuwa Askari wa Operesheni Tokomeza hawauski na kifo
 cha mtajwa. Taarifa hiyo imeonekana kukosa umakini kutokana na 
kujichanganya juu ya watu inaowazungumzia. Taarifa hiyo inazungumzia 
majina mawili tofauti (Evelyn Gasper na Mariana Gaspar Mallo wa eneo la 
Olongadiola) wakati muathirika halisi ni Bi. Emilliana Gasper Maro wa 
Kijiji cha Orngadida, Gallapo. (Tazama kiambatisho Na.7) 
 Ukatili dhidi ya Wanyama
 x. Mheshimiwa Spika, kuhusu vitendo vya ukatili kwa wanyama ilidaiwa 
kwamba ng’ombe walipigwa risasi, na ndama walikufa kwa kukosa maziwa 
kutokana na mama zao kukamatwa na kuzuiwa kwenye mazizi yaliyopo maeneo 
ya hifadhi kwa muda mrefu. (Tazama Kiambatisho Na.
 Rushwa kwenye Mapori ya Akiba 
 xi. Mheshimiwa Spika,Wananchi walidai kukithiri kwa vitendo vya rushwa 
kwa watumishi wanaosimamia mapori ya akiba ya Maswa, Kigosi Moyowosi, 
Burigi, Kimisi na Mkungunero kwa kutaja majina ya baadhi ya watumishi 
wanaowatuhumu. Mfano; Ndg. Kileo mtumishiwa pori la Maswa, alidaiwa kuwa
 na tabia ya kutoza wananchi faini bila stakabadhi au kutoa stakabadhi 
kinyume na faini iliyotolewa au kutoa stakabadhi bandia. 
 Aidha,
 katika pori la Kigosi-moyowosi, watumishi wafuatao walidaiwa 
kujihusisha na vitendo vya rushwa; Ndg. Msocha, Alfred, Kobelo na 
Odhiambo. 
 Aidha, ilidaiwa kuwa katika mapori ya Kigosi Moyowosi
 na Kimisi zaidi ya wafugaji 100 wenye ng’ombe wanaokadiriwa kuwa 50,000
 wanalipia kuchungia ng’ombe wao kwenye mapori hayo ya hifadhi tangu 
mwaka 2000 kwa malipo maalum na hata Operesheni Tokomeza haikuwagusa.
 Aidha, ilidaiwa kuwaNdg. Msocha (Meneja wa Pori la Akiba la Kigosi 
Muyowosi), alituhumiwa na baadhi ya wananchi kuwa amekuwa akiwakodisha 
wafugaji hao kwa vipindi vya miezi mitatu, na wafugaji huruhusiwa kulipa
 tena muda unapoisha. Aidha, Mfugaji ambaye hulipa kiasi kidogo 
hulazimishwa kulipa huku akipigwa namifugo yake kuuawa kwa kupigwa 
risasi. 
 Ilielezwa kuwa, Wafugaji na Askari Wanyamapori 
huwasiliana kwa simu ilil kutekeleza makubaliano ya malipo kwa malisho 
yao. Nambaza simu zinazodaiwa kuwa za Askari Wanyamapori zimeorodheshwa.
 (Tazama Kiambatisho Na. 9) 
 Mahusiano kati ya wananchi na Askari wa mapori ya Akiba
 xii. Mheshimiwa Spika, wananchi wanaoishi kwenye Mapori ya Akiba yanayo
 wazunguka walidai kuwa katika mahusiano mabaya naAskari wa mapori hayo.
 Mfano;wananchi wa kijiji cha Kimotorok, Wilaya ya Simanjiro na Askari 
wa pori la akiba la Mkungunero kiasi cha kufikia hatua ya kutishiana 
maisha. Vitendo hivyo pia vipo kwa jamii zinazopakana na mapori ya 
Gurumeti. 
 Mahakama na Magereza kuzidiwa uwezo
 
xiii.Mheshimiwa Spika, kutokana na Operesheni Tokomeza ilidaiwa kuwa 
vyombo Mahakama na Magereza katika maeneo husika vilizidiwa uwezo 
kutokana na wingi wa kesi na idadi ya Mahabusu. Mfano;Gereza la Wilaya 
ya Bunda lenye uwezo wa kuchukua jumla ya wafungwa na mahabusu 217 
lililazimika kuchukua hadi watu 411. 
 Baadhi ya watuhumiwa 
waliokamatwa wanalazimika kusafiri umbali mrefu kuhudhuria kesi zao. 
Mfano; katika wilaya ya Serengeti baadhi ya watuhumiwa walifunguliwa 
kesi Wilaya za Tarime, Bunda na Bariadi.
 Watumishi wa Umma kuhusishwa na Ujangili 
 xiv.Mheshimiwa Spika, ilidaiwa kuwa baadhi ya Watumishi waSerikali na 
vyombo vya dola (Polisi) wanajihusisha na ujangili. Mfano niDereva wa 
OCD, Wilaya ya Ngorongoro aliyetuhumiwa kujihusisha na ujangili wa Meno 
ya Tembo. 
 Askari huyo alihojiwa na viongozi wa Operesheni 
Tokomeza katika kituo chake cha kazi. Vilevile, Ndg. Mohamed Ismail, 
Afisa Wanyamapori (W) Meatu anatuhumiwa kukutwa na nyara zaSerikali. 
 Aidha,Askari Polisi wawili (2)Cpl. Isaack na PC Sixbert wa Mugumu Wilayani Serengeti walikamatwa wakiwa na meno ya Tembo.
 Mheshimiwa Spika, pia ilidaiwa kuwa baadhi ya Maofisa wa Serikali 
wamekuwa wakitumia magari ya Umma ama kusafirisha au kusindikiza 
watoroshaji wa nyara za Serikali. Mfano nigari la Serikali lililokamatwa
 likifaulisha meno ya Tembo kutoka kwenye gari jingine huko Mkuranga kwa
 lengo la kuyasafirisha kwenda Dar es Salaam. 
 Sambamba na hilo 
baadhi viongozi wa jeshi la Polisi wametuhumiwa kusaidia watuhumiwa wa 
vitendo vya kijangili kutoroka na kuepuka mkono wa sheria. 
 Migogoro kuhusu mipaka ya Maeneo ya Hifadhi
 xv. Mheshimiwa Spika,wananchi walidai kuwa baadhi ya Mapori ya Akiba 
naHifadhi yamekuwa yakipanua mipaka yake bila kushirikisha wananchi wa 
maeneo yanayowazunguka. Mfano; wananchi wa Wilaya ya Bunda wanaopakana 
na Pori la Akiba la Gurumeti. 
 Pia, wananchi wa vijiji vya 
Kegonga na Masanga, katika Kata ya Nyanungu, Wilayani Tarime wako katika
 mgogoro wa mpaka na TANAPA wakidai kuwa bonde la Nyanungu limemezwa na 
eneo la Hifadhi kutokana na TANAPA kuongeza mipaka yake bila 
kushirikisha wananchi wa maeneo hayo.
 Aidha, katika Wilaya ya Ulanga kuna mgogoro katika kata za Iputi na Lupiro dhidiHifadhi ya Selous. 
 Idara za Wanyamapori katika Halmashauri kukosa vitendea kazi
 xvi.Mheshimiwa Spika, kutokana na silaha za Idara ya Wanyamapori katika
 baadhi ya Halmashauri kuchukuliwa wakati wa Operesheni Tokomeza kwa 
ajili ya uchunguzi, wananchi wamedai kupata shida kutokana na wanyama 
hasa Tembokuvamia mashamba na kuharibu mazao pamoja na kujeruhi au kuua 
watu na mifugo. 
 Wanasiasa kushawishi wananchi kuishi kwenye maeneo ya Hifadhi
 xvii. Mheshimiwa Spika, wakati wa kutekeleza Operesheni Tokomeza 
ilidaiwa kuwa nyumba na maboma ndani ya mapori ya akiba zilichomwa moto.
 Mfano; Wilaya ya Sumbawanga kijiji cha Msila Kata ya Mfinga na kijiji 
cha Kabage Wilaya ya Mpanda. Hata hivyo baadhi ya wananchi wameanza 
kurejeakatika baadhi ya maeneo ya hifadhi kutokana na ushawishi wa 
wanasiasa. 
 Mfano; katika Pori la Hifadhi ya Jamii Ubende Wilaya
 ya Mpanda walichangishwa shilingi laki moja (100,000/ kwakila kaya kwa 
ajili ya kupatiwa huduma za kisheria iwapo mamlaka husika zitajaribu 
kuwaondoa ndani ya hifadhi. Aidha, Kamati ilipata taarifa kuwa, baadhi 
ya viongozi wa Vyama vya Siasa wamekuwa wakigawa kadi za vyama vyao kwa 
wananchi wanaoishi katika maeneo ya hifadhi na kwa ahadi kwamba, vyama 
walivyojiunga nga navyo vitawatetea wasiondoke katika maeneo hayo. 
 Tatizo la Vibali vya Wakulima wa Muda
 xviii. Mheshimiwa Spika, Kamati ilielezwa lipo tatizo la raia wa nchi 
jirani kuingia nchini na kupewa vibali vyakuendesha shughuli za 
kilimo(Peasant Permit)kwa muda, ambavyo hutolewa bilakubandika picha ya 
mhusika/mwombaji hasa maeneo ya Karagwe. 
 Raia hao wanadaiwa 
kutumia nakala za vibali hivyo kuingiza nchini wahamiaji haramu ambao 
baadhi yao huingiza makundi makubwa ya mifugo hasa ng’ombe na wengine 
kutumia mwanya huo kuingiza silaha na kujihusisha na vitendo vya 
ujangili katika baadhi ya mapori ya akiba. Mfano; Pori la Akiba la 
Ibanda Rumanyika. 
 Vilevile kuna tatizo la majangili kutumia 
vivuli va wafugaji kuingia kwenye hifadhi huku wakiwa wameficha silaha, 
na hivyo kuwepo mazingira ya kushindwa kutofautisha kati ya majangili na
 wafugaji hususan katika maeneo ya hifadhi ya Ruaha. 
 
xix.Mheshimiwa Spika, kuna mgogoro katika eneo la Ushoroba (Buffer Zone)
 katika Kata za Lupiro, Mbugana Iputi Wilaya ya Ulanga, maeneo ambayo 
jamii imejenga miundombinu kwa miaka mingi ikiwa ni pamoja na shule, 
nyumba, mashamba, misikiti na makanisa huku Serikali ikiwa kimya kwa 
muda mrefu.Hata hivyo, wakati wa Operesheni Tokomeza wananchi hao 
walilazimishwa kuhama bila kuelekezwa waende wapi. 
 Michango ya Waheshimiwa Wabunge kuhusu Operesheni
 xx. Mheshimiwa Spika, Kamati ilibaini kuwa baadhi ya michango 
iliyotolewa na Waheshimiwa Wabunge wakati wakichangia Hoja ya Mhe. Saidi
 Nkumba haikuwa imefanyiwa utafiti wa kutosha kwani baadhi ya madai 
waliyoyatoa hayakuwa na uhusiano na Oparesheni Tokomeza. 
 Kwa 
mfano;ni kweli kwamba ng’ombe 51 walitumbukia katika mto Rubana Wilayani
 Bunda na kufa, hata hivyo tukio hilo lilitokea mwezi April, 2013 ikiwa 
ni miezi 6 kabla ya Operesheni. Aidha, ni kweli kuwa Wakazi wa Vijiji 
vya Kabage Wilayani Mpanda na Luchima Wilayani Mulele walihamishwa 
kutoka katika maeneo ya hifadhi na nyumba zao kuchomwa moto katika 
utaratibu uliofanywa na Halmashauri hizo mwezi Septemba, 2013 kwa lengo 
la kuwapeleka kwenye maeneo rasmi ya makazi. 
 
 7.0 MAONI NA USHAURI WA KAMATI KUHUSU TATHMINI YA UTEKELEZAJI WA OPERESHENI TOKOMEZA 
 Mheshimiwa Spika, baada ya Kamati kuchambua nyaraka husika kuhusiana na
 utekelezaji wa Operesheni Tokomeza, kuwahoji viongozi mbalimbali wa 
Wizara na Waheshimiwa Wabunge, pamoja na kufanya ziara mikoani kwa lengo
 la kuhakiki yaliyojiri kutokana na Operesheni Tokomeza, Kamati inapenda
 kutoa maoni na ushauri ufuatao:- 
 i. Kwa kuwa, lengo la 
Operesheni Tokomeza lilikuwa kunusuru raslimali za nchi hususani 
Wanyamapori na hasa Tembo na Misitu, na kwa kuwa Waheshimiwa Wabunge na 
Wananchi wameiunga mkono mbali na matatizo ya kiutendaji yaliyojitokeza,
 hivyo basi, Bunge linaazimia kwamba, Serikali irekebishe haraka kasoro 
zilizojitokeza katika utekelezaji wa Operesheni Tokomeza ili kuendeleza 
na kukamilisha awamu zote za operesheni kama zilivyo kwenye mpango na 
kunusuru raslimali za Taifa hasa wanyamapori na misitu ambayo inatishiwa
 kutoweka kutokana na vitendo vya ujangili. 
 ii. Kwa kuwa,Kamati
 imejiridhishakwamba matatizo na upungufu uliojitokeza katika 
utekelezaji wa Operesheni Tokomeza yamechangiwa na maandalizi mabaya ya 
Mpango kazi ambao Waziri Mwenye dhamana hakuidhinisha, na kwa kuwa, 
imedhihirika kuwepo hali ya sintofahamu (kwa mujibu wa hansard) 
iliyosababishwa na watendaji wakuu wa Wizara kwa makusudi kuamua 
kutomshirikisha kikamilifu Waziri katika hatua za mwisho za maandalizi 
ya Mpango kazi, hivyo basi Bunge linaazimia kwamba, Serikali iwachukulie
 hatua stahiki za kinidhamu Wasaidizi Wakuu wote wa Waziri walioshiriki 
katika Mpango kazi huo. 
 iii. Kwa kuwa, Kamati imebaini kwamba 
pale Jeshi la Wananchi (JWTZ) linaposhirikishwa katika Operesheni 
ufanisi mkubwa hupatikana, na kwa kuwa, bado iko haja ya kuendeleza 
Operesheni Tokomeza kwa maslahi ya Taifa, na kwa kuwa ushahidi wa 
mazingira ‘circumstantial evidence’ unaonesha kuwa Jeshi lilichukua 
uongozi wa operesheni baada ya kugundua kuwa washiriki kutoka Vikosi 
vingine (Polisi, TANAPA, TSF na NCAA) kwa kushirikiana na wafugaji wenye
 ushawishi wa kifedha pamoja na wanasiasa, walihujumu operesheni hiyo 
kwa kutoa taarifa kwenye mtandao mkubwa wa kijangili ambao umejengeka 
kuanzia Wizarani hadi kwenye maeneo ya Hifadhi na kusaidia ‘majangili 
papa’ wasikamatwe, hivyo basi, Bunge linaazimia kwamba:- 
 - Serikali kuchukua hatua za makusudi kuuvunja mtandao huo na pia;
 - Kuandaa operesheni nyingine ambayo itapangwa na kutekelezwa na Jeshi la Wananchi wa Tanzania na Idara ya Usalama wa Taifa. 
 iv. Kwa kuwa, kumekuwepo na operesheni kadhaa kabla ya Operesheni 
Tokomeza ambazo zililenga kupambana na ujangili, na kwa kuwa, Operesheni
 Tokomeza imeshindwa kupata mafanikio yaliyotarajiwa, na kwa kuwa, 
ushahidi wa mazingira unaonesha wazi kwamba, Kikosi Dhidi ya Ujangili 
(KDU) kimeshindwa kutimiza wajibu wake, hivyo basi, Bunge linaazimia 
kwamba, Serikali iimarishe kikosi hicho kwa kukifanyia tathmini na 
kukiunda upya ikiwa ni pamoja na kukiwezesha kwa rasilimali (Watu, 
fedha, magari, silaha za kisasa na vifaa vya mawasiliano kama redio na 
simu). 
 Serikali iunde chombo ambacho kitakuwa na jukumu la 
kusimamia na kutathmini utendaji kazi wa KDU. Iwapo utaratibu huo 
utazingatiwa ni wazi vitendo vya ujangili vitadhibitiwa bila kutumia 
operesheni kubwa kama Uhai na Tokomeza. 
 v. Kwa kuwa, Kamati 
imebaini kuwepo kwa vitendo vya utesaji na ukatili wa hali ya juu, 
ukiukwaji wa haki za binadamu na uzembe miongoni mwa Askari wa 
Operesheni Tokomeza (ushahidi wa wahusika upo), hali ambayo imesababisha
 baadhi ya Wananchi kupoteza maisha, kupata ulemavu wa kudumu pamoja na 
kupoteza mali zao. Hivyo basi, Bunge linaazimia kwamba:- 
 - 
Serikali Iwabaini wote waliohusika na vitendo vya kinyama, mateso na 
udhalilishaji dhidi ya watuhumiwa, iwachukulie hatua stahiki na 
kuwasilisha taarifa ya utekelezaji wa agizo hili katika Mkutano ujao wa 
Bunge. 
 - Ifanye tathmini ya kina kwa kupitia Wakuu wa Mikoa na 
Wilaya ili kujua athari za Operesheni hii na kutafuta njia ya kutoa 
kifuta machozi kwa waathirika, ili kurejesha imani ya Wananchi kwa 
Serikali yao. 
 vi. Kwa kuwa, Kamati imebaini kuwa Operesheni 
Tokomeza ilikuwa haikutengewa fedha katika Bajeti ya Wizara ya Maliasili
 na Utalii katika mwaka wa fedha wa 2013/2014 na kwa kuwa kiasi cha 
fedha Tshs. 3,968,168,667/= kilichopatikana kutoka Idara na Mashirika 
Tanzu ya Wizara haikutosheleza mahitaji ya fedha ya Operesheni Tokomeza 
kutokana na ukubwa wa eneo la Operesheni, hivyo basi, Bunge linaazimia 
kwamba, Serikali itenge Bajeti Maalum ya kutosheleza mahitaji ya 
Operesheni Tokomeza. 
 Serikali kutenga Bajeti kwa ajili ya 
kuendeleza shughuli za uhifadhi katika maeneo ya Hifadhi ikiwa ni pamoja
 na kuweka raslimali watu ya kutosha na miundombinu mingine muhimu. 
 vii. Kwa kuwa, Kamati imebaini kuwa Taarifa kwa Umma iliyotolewa kwa 
Vyombo vya Habari na Mkurugenzi wa Idara ya Wanyamapori tarehe 23 Oktoba
 2013, haikuwa sahihi na pia ililenga kuudanganya Umma kwa kuficha 
mazingira na sababu za kifo cha Bi Emilliana Gasper Maro, hivyo basi, 
Bunge linaazimia kwamba, Serikali ichukue hatua za kumwajibisha 
Mkurugenzi wa Idara ya Wanyapori kwa kuudanganya umma kwa kujaribu 
kuficha ukweli. 
 viii.Kwa kuwa, Kamati imebaini kuwa kumekuwapo 
mchezo mchafu unaofanywa na baadhi ya Maafisa Wanyamapori, Maafisa 
Misitu katika mapori ya akiba, Misitu ya Serikali na katika baadhi ya 
Hifadhi za Taifa wa kupokea rushwa, kutesa wananchi, kuwabambika kesi na
 kujihusisha na ujangili,na kwa kuwa Kamati inayo majina na vielelezo 
vya wahusika, hivyo basi, Bunge linaazimia kwamba, Serikali ifanye 
tathmini nchi nzima kwa lengo la kutambua kiwango cha vitendo vya rushwa
 miongoni mwa watumishi hao, na kuwachukulia hatua stahiki za kinidhamu 
wale watakaobainika kuhusika ikiwa ni pamoja na kuwawajibisha na 
kuwafikisha kwenye vyombo vya sheria. 
 ix. Kwa kuwa, Kamati 
imebaini kuwa baadhi ya viongozi wa kisiasa na Serikali waliingilia 
utekelezaji wa Operesheni Tokomeza kwa manufaa yao binafsi, kwa mfano, 
agizo la kuwataka wahusika wa Operesheni Tokomeza kutowagusa Viongozi wa
 Kisiasa wa ngazi zote, kauli ambayo ilitafsiriwa kuathiri utekelezaji 
wa Operesheni Tokomeza kwa kubagua Watanzania katika makundi ya Viongozi
 na Wananchi wa kawaida, hivyo basi, Bunge linaazimia kwamba, Serikali 
ihakikishe kuna uwajibikaji wa pamoja pale inapoamua kutekeleza jambo la
 Kitaifa kama Operesheni Tokomeza. 
 x. Kwa kuwa, Kamati 
imethibitisha kuwa, baadhi ya wanasiasa wamekuwa wanawadanganya wananchi
 waliothibitika kufanya shughuli za uchumi kwenye maeneo ya hifadhi, na 
kuwaahidi kuwatetea pindi Serikali inapochukua hatua za kuwaondoa katika
 sehemu hizo, ikiwa ni pamoja na kuwapa kadi za vyama vyao vya siasa, 
hivyo basi, Bunge linaazimia kwamba, serikali ihakikishe kwamba, 
wananchi hawaendeshi shughuli za kiuchumi kwenye maeneo ya hifadhi na 
kuwaonya wanasiasa waache kuwalaghai wananchi kwa maslahi yao binafsi. 
 xi. Kwa kuwa,Kamati imebaini kwamba katika baadhi ya maeneo ya mipakani
 mfano Karagwe, Idara ya Uhamiaji hutoa vibali kwa raia wa nchi jirani 
vya kuishi na kulima hapa nchini, vibali ambavyo havina udhibiti wala 
tija kwa nchi, na kusababisha migogoro ya mara kwa mara kati ya wakulima
 na wafugaji lakini pia uharibifu wa mazingira kwa kuingiza mifugo 
hifadhini, hivyo basi, Bunge linaazimia kwamba, Serikali isitishe mara 
moja zoezi la kutoa vibali hivyo, kufuta vilivyopo na kuwataka raia hao 
wa kigeni wenye vibali kuondoka Nchini mara moja. 
 xii.Kwa kuwa,
 Kamati imebaini kwamba zaidi ya asilimia 25 ya eneo la Nchi ni hifadhi,
 namipaka ya maeneo mengi yaliyohifadhiwa haijaainishwa, na kwa kuwa 
Serikali haina uwezo wa (raslimali watu na fedha) wa kusimamia na 
kulinda mipaka ya maeneo haya kikamilifu, hivyo basi, Bunge linaazimia 
kwamba, Serikali kufanya yafuatayo:- 
 • Kuridhia Idara ya 
Wanyamapori na Wakala wa Huduma ya Misitu kuajiri idadi ya watumishi 
wanaotakiwa kama Serikali bado inaendelea kuyahifadhi maeno hayo.
 • 
Kuainisha mipaka ya mapori yote ya akiba, hifadhi za taifa na Misitu ya 
Serikali kwa alama maalumu na za kudumu ili kuepusha Wananchi kuingia 
katika maeneo hayo kwa kutojua mipaka.
 • Kuyaachia mapori ya 
Serikali ambayo yamekosa sifa, ili yatumike kwa kilimo na ufugaji kwa 
kuzingatia mpango wa matumizi bora ya ardhi. 
 xiii.Kwa kuwa,yapo
 maeneo ya mapori na Hifadhi ambayo yana migogoro ya muda mrefu ambapo 
wananchi wameishi katika maeneo hayo kwa muda mrefu, hivyo basi, Bunge 
linaazimia kwamba, Serikali irekebishe mipaka husika au iwahamishie 
Wananchi hao kwenye maeneo mengine yenye miundombinu. Serikali iwaagize 
Mawaziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Maliasili na Utalii na
 Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa kutembelea maeneo yote yenye 
migogoro nchini na kuitafutia ufumbuzi ili wananchi waweze kuelewa hatma
 yao katika maeneo hayo kwani wamekuwa katika hali ya sintofahamu kwa 
muda mrefu. 
 xiv.Kwa kuwa, Kamati imebaini kuwepo kwa migogoro 
baina ya Wananchi, Wawekezaji na hifadhi katika maeneo ya Meatu, Tarime,
 Bunda na ile ya Loliondo na Kimotorok ambayo inashughulikiwa na Ofisi 
ya Waziri Mkuu, hivyo basi, Bunge linaazimia kwamba, Serikali ihakikishe
 inamaliza (kama ilivyoahidi) migogoro iliyopo Loliondo na Kimotorok na 
maeneo mengine mapema iwezekanavyo. 
 Kurekebisha haraka kasoro 
zote za kisheria zilizokiukwa kwa makusudi na Idara ya Wanyamapori kiasi
 cha kusababisha mgogoro baina ya Halmashauri ya Wilaya ya Meatu na 
mwekezaji katika Pori la Hifadhi ya Jamii la Makao pamoja na 
kuwawajibisha Watendaji wa Idara ya Wanyamapori waliosababisha mgogoro 
huo. 
 xv.Kwa kuwa, Kamati imebaini kwamba, migogoro 
wanayokumbana nayo wafugaji kutokana na kuingiza mifugo kwenye maeneo ya
 hifadhi pamoja na kero nyingine ni kutokana na kukosekana kwa 
miundombinu sahihi na endelevu kwa ajili ya ustawi wa mifugo, na kwa 
kuwa, Mheshimiwa Rais aliunda Wizara mahsusi kwa ajili ya kuendeleza 
Sekta ya Mifugo nchini akitambua umuhimu wa Sekta hii kwa uchumi wa 
Taifa, na kwa kuwa, Tanzania ni ya pili kwa wingi wa mifugo Barani 
Afrika, ni wazi kwamba adha wanazokumbana nazo wafugaji ni matokeo ya 
kutokuwepo sera na mipango madhubuti ya muda mfupi na mrefu. 
 
Hivyo basi, Bunge linaishauri Serikali kumtaka Waziri wa Maendeleo ya 
Mifugo na Uvuvi, kujipima na kuona iwapo bado anastahili kuendelea 
kuhodhi wadhifa alionao. 
 xvi.Kwa kuwa, Kamati imebaini kuwa 
baadhi ya madai yaliyotolewa na Waheshimiwa Wabunge Bungeni wakati 
wakichangia Hoja ya Mhe. Saidi Nkumba ilikuwa ni ya kweli; na kwa kuwa 
yaliyoelezwa katika madai hayo hayana uhusiano na Operesheni Tokomeza 
kwani yalitokea kabla ya Operesheni hiyo; hivyo basi, Bunge linaazimia 
kwamba, Waheshimiwa Wabunge kuwa makini zaidi na kufanya utafiti kwa 
lengo la kuhakikisha michango yao inakuwa sahihi na inalenga hoja 
mahsusi iliyo mbele ya Bunge. 
 8.0 HITIMISHO 
 Mheshimiwa
 Spika, jukumu uliloikabidhi Kamati hii lilikuwa zito na lilihitaji 
umakini mkubwa na muda wa kutosha katika kulitekeleza. Kutokana na 
ufinyu wa muda na mazingira magumu wakati wa kutekeleza jukumu hilo, 
Kamati inakiri kwamba haikuweza kutembelea maeneo yote yaliyoathirika na
 zipo lawama kutoka kwa baadhi ya wananchi kwamba, Kamati haikuweza 
kupita katika maeneo yao. 
 Mheshimiwa Spika, Kamati inapenda 
kuwahakikishia wananchi wote kuwa, kupitia taarifa mbalimbali za 
viongozi na wawakilisihi wa waathirika mbele ya Kamati, malalamiko yao 
yamezingatiwa na kufanyiwa kazi. 
 Mheshimiwa Spika,kama 
tulivyoeleza katika maelezo yetu ya utangulizi, Kamati inaamini na kote 
tulikopita wananchi wanakiri kuwa, lengo na azma ya Serikali kuanzisha 
Operesheni Tokomeza Ujangili lilikuwa jema kwani lililenga kunusuru 
maliasili zetu kwa ajili ya maendeleo endelevu na heshima ya Taifa letu. 
 Mheshimiwa Spika, Kamati inaamini maelezo yote yaliyotolewa na wananchi
 pamoja na viongozi wao yalikuwa na dhamira njema. Aidha, mapendekezo 
yaliyotolewa na Kamati yanalenga kuisaidia Serikali kuchukua hatua za 
makusudi na haraka kurekebisha kasoro zilizojitokeza wakati wa 
utekelezaji wa Operesheni Tokomeza Ujangili, ili kuepuka kutokea kwa 
vitendo vinavyoashiria ukiukwaji wa misingi ya haki za binadamu na 
Utawala Bora nchini. 
 Mheshimiwa Spika, napenda kukushukuru wewe
 binafsi kwa dhati kutokana na kuiamini Kamati yangu na kuikabidhi 
jukumu hili zito. Hii ni ishara tosha kwamba una imani na Wabunge wako 
na kwamba wanaweza kufanya kazi kwa niaba yako. 
 Mheshimiwa 
Spika, pia nitoe shukrani za dhati kwa Katibu wa Bunge, Dkt. Thomas 
Didimu Kashilillah, kwa kuiwezesha Kamati hii kufanya kazi yake vizuri 
na kuikamilisha kwa wakati. Aidha, kwa namna ya pekee napenda 
kuwashukuru makatibu walioihudumia Kamati hii wakiongozwa na Ndugu 
Theonest K. Ruhilabake ambao ni Ndugu Gerald Magili, Ndugu Chacha 
Nyakega na Ndugu Stanslaus Kagisa. 
 Aidha, ninapenda kuwashukuru
 viongozi wa Mikoa, Wilaya, Kata na Vijiji ambao walionyesha ushirikiano
 mkubwa Kamati ilipotembelea maeneo yao. 
 Mheshimiwa Spika, 
mwisho lakini si kwa umuhimu Kamati inawashukuru watumishi wafuatao; 
Ndugu Silva Chindandi, Ndugu Ndigwako Mwaigaga, Ndugu Victoria Mizengo, 
Ndugu Germina Magohe na watumishi wengine ambao kwa namna moja au 
nyingine walishiriki katika kuihudumia Kamati hii hadi inakamilisha 
taarifa hii. 
 Mheshimiwa Spika, naomba kutoa hoja. 
 James Daud Lembeli, Mb
 MWENYEKITI KAMATI YA KUDUMU YA BUNGE YA ARDHI, MALIASILI NA MAZINGIRA
 
 
 
 
 
 



 
 

No comments:
Post a Comment