MAMLAKA YA MAWASILIANO TANZANIA
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
MATUMIZI MABAYA YA MAWASILIANO NA UDANGANYIFU KATIKA USAJILI WA NAMBA ZA SIMU ZA MKONONI NCHINI NIKOSA LA JINAI
1. Huduma
za mawasiliano nchini katika kipindi cha miaka kumi iliyopita zimekuwa
sana na kuwafikia watu wengi zaidi. Ni ukweli usiopingika kuwa
watanzania wengi hivi sasa wanafaidika kwa huduma za mawasiliano,
hususani katika mawasiliano ya simu za mikononi, utangazaji, intaneti na
huduma za ziada kama kutuma na kupokea fedha kwa kutumia mitandao na
simu za mkononi. Wananchi wengi wanapata huduma za kibenki kwa kutumia
simu zao, wanawasiliana kwa kutumia simu zao kupitia sauti, SMS na
kadhalika.
2. Aidha kumekuwa na ongezeko la matumizi ya intaneti kwa
watanzania walio wengi hususani matumizi ya mitandao ya kijamii kama
vile Facebook, twitter, BBM, LinkedIn na blog mbalimbali. Matumizi haya
yamewanufaisha watanzaia kwani ni fursa murua ya kujifunza kupitia
mitandao hiyo ya kijamii kwa kupata habari mpya, kujifunza na
kuelimishana kuhusu shughuli za maendeleo na kuleta amani miongoni mwa
watanzania.
3. Pamoja na maendeleo haya chanya kwa nchi yetu, kumekuwepo na
baadhi ya watu wachache wanaotumia mawasiliano ya simu, mitandao ya
kijamii, redio, TV na mawasiliano mengine kwa lengo la
kuvuruga
amani, kuchocheo ugomvi, kuchonganisha watu, kusababisha ugomvi,
kuwaumiza wengine kwa mambo yasiyo na ukweli, kupotosha jamii na hata
kuvuruga maendeleo kwa ujumla.
4. Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) inawatahadharisha
wananchi kwamba ni kosa la jinai kutumia mawasiliano vibaya kama
ilivyoainishwa katika sheria ya Mawasiliano ya Kielectroniki na Posta
(EPOCA) ya mwaka 2010. Wananchi wanashauriwa kuhakikisha wanatumia
mawasiliano vizuri na kuhakikisha tunadumisha amani na upendo miongoni
mwa watanzania.
5. Aidha mamlaka inapenda kuwakumbusha wananchi kuwa kusajili
laini yako ya simu, kwa kutumia utambulisho wa udanganyifu pia ni kosa
la jinai. Mtumiaji wa huduma za mawasiliano unatakiwa kwenda kwa mtoa
huduma au wakala wake ukiwa na kitambulisho sahihi chenye picha yako na
kutoa taarifa sahihi. Sheria ya Mawasiliano ya Kielektroniki na Posta
(EPOCA) ya mwaka 2010, kifungu cha 131, kimeainisha kuwa ni kosa la
jinai kutumia au kuwezesha kutumika namba ya simu isiyosajiliwa. Adhabu
ya faini ya shilingi laki tano (Tshs 500,000.00) au kifungo cha miezi
mitatu itatolewa kwa yeyote atakayekiuka sheria hii.
6. Kuanzia tarehe 1 Juni 2013 saa sita usiku,
laini zote za simu ambazo hazijaanza kutumika zilifungwa (locked) na
haziruhusiwi kutumika hadi mtumiaji atakapoisajili laini yake mpya kwa
watoa huduma. Kama kuna mwananchi atakaenunua laini, na kuweza kuitumia
bila ya kuisajili, anaombwa kutoa taarifa kwa Mamlaka ya Mawasiliano
Tanzania (TCRA).
7. Watumiaji wote wa simu za mkononi ambao hawakuwa wamesajili
namba zao za simu wafanye hivyo mara moja. Ifahamike kwamba ilipofika
tarehe 10 Julai 2013 saa sita usiku, laini za simu ambazo zilikuwa zinatumika na zilikuwa bado hazijasajiliwa hadi wakati huo, zilifungwa.
Kufungua laini iliyofungwa, mtumiaji atapaswa kwenda kwenye ofisi ya
mtoa huduma wake au wakala wake kusajili upya na kuthibitishwa ili laini
yake ifunguliwe.
8. Watumiaji wa simu za mkononi na wananchi wanashauriwa kuunga
mkono juhudi zinazofanyika ili kufanikisha usajili wa namba za simu kwa
ajili ya kudumisha na kuendeleza amani na usalama na kuharakisha
maendeleo ya sekta na ya Taifa kwa ujumla.
9. Faida za kusajili laini ya simu ni nyingi zikiwemo usalama
katika huduma za kutuma na kupokea pesa kwa mitandao ya simu. Kununua na
kulipia gharama mbalimbali zikiwemo za bili za umeme, maji, na ushuru
na pia kusaidia upelelezi iwapo kuna matumizi mabaya ya simu.
10. Mamlaka inapenda kuukumbusha umma kuwa ni kosa la jinai:
a) Kuuza
laini za simu kama wewe si wakala wa mtoa huduma: Iwapo mtu atakamatwa
na kutiwa hatiani akiuza laini za simu ikiwa yeye si wakala wa kampuni
ya simu atahukumiwa kulipa faini ya shilingi milioni saba au kufungwa
jela miaka miwili au adhabu zote mbili kwa pamoja.
b) Kutumia simu isiyosajiliwa: Mtu yeyote anayetumia simu
isiyosajiliwa anatenda kosa la jinai na akitiwa hatiani atahukumiwa
kulipa faini isiyozidi shilingi laki tano, au kifungo cha miezi mitatu
jela.
c) Kutoa taarifa za uongo wakati wa kusajili namba ya
simu: Mtu yeyote atakayetoa taarifa za uongo akijua kuwa taarifa hizo si
za kweli anatenda kosa la jinai na akitiwa hatiani atahukumiwa kulipa
faini ya shilingi milioni tatu au kifungo cha miezi kumi na miwili au
adhabu zote kwa pamoja.
d) Kumsaidia mtu mwingine atende kosa kwa mujibu wa sheria za
mawasiliano naye anatenda kosa na akitiwa hatiani atahukumiwa kulipa
faini isiyozidi shilingi milioni tatu au kufungwa jela miezi kumi na
miwili au adhabu zote mbili kwa pamoja.
e) Kutumia njia yeyote ya mawasiliano kuvuruga amani, kugombanisha
watu, kufanya uchochezi wa kidini au kisiasa, kueneza chuki, kusambaza
uongo na kuleta vurugu katika jamii ni kosa la jinai na hatua kali
zitachukuliwa dhidi ya watakaobanika kufanya hivyo kwa mujibu wa sheria.
f) Mwananchi ukipokea ujumbe wowote wa kueneza chuki, unaopelekea
kuvuruga amani, uchochezi na kuvuruga amani, toa taarifa kwa vyombo
husika, kasha futa ujumbe huo. Usiueneze kwa wengine kwani utakuwa
sehemu ya uhalifu.
Imetolewa na:
MSEMAJI MAMLAKA YA MAWASILIANO
MAMLAKA YA MAWASILIANO TANZANIA
26 July 2013