Mji wa Goma
Waasi wa M23 wakipita pembeni mwa vikosi vya UN kuelekea Goma bila kufanywa chochote na vikosi hivyo
Msemaji wa kundi la M23,
Kanali Vianney Kazarama ameliambia shirika la habari la AP kwa njia ya
simu kwamba sasa waasi wanapambana kuudhibiti mji wote wa Goma, baada ya
kufanikiwa kuudhibiti uwanja wa ndege na kwamba sasa wako ndani ya mji
wa Goma.
Pia akizungumza
leo, Mbunge wa jimbo la Kivu Kaskazini, Mayombo Omary Bin Fikira
amethibitisha kwamba waasi wameutwaa uwanja huo wa ndege. Mbunge huyo
anasema kwa sasa hali ni ya kutatanisha katika mji wa Goma na milio ya
risasi imekuwa ikisikika.
Wakati huo huo, Baraza la usalama la Umoja wa
Mataifa limepitisha kwa kauli moja azimio linalolaani kutekwa kwa mji wa
Goma nchini Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo na waasi wa M23.
Azimio hilo pia linamtaka katibu mkuu wa Umoja
huo kuripoti kuhusu madai ya uungwaji mkono wa mataifa ya kigeni kwa
makundi ya uasi yaliyoanza harakati zao nchini Congo miezi minane
iliyopita.
Baraza la usalam la Umoja wa mataifa limelaani vikali kitendo cha waasi wa M23 kuuteka mji wa Goma.
Baraza la usalama la Umoja wa mataifa tayari
limeidhinisha vikwazo dhidi ya mkuu wa kundi hilo na limesema limenuia
vikwazo hivyo vitawalenga viongozi zaidi wa waasi .
Wajumbe wa baraza hilo wameelezea hofu kubwa juu
ya shutuma kuwa waasi hao wanaungwa mkono kutoka nje hatua iliyopelekea
waasi wa M23 kuwa na uwezo mkubwa zaidi wa kijeshi
Baraza hilo limemtaka katibu mkuu wa Umoja huo kuchunguza ripoti kuhusiana na shutuma hizo .
Wataalamu wa Umoja wa mataifa wamesema kuna
ushahidi wa kutosha kuwa Rwanda inawaunga mkono waaasi hao na makundi ya
haki za kibinadamu kwa kushindwa kutuma onyo kwa utawala wa Kigali kama
wahusika.
Wakati huo huo maafisa wa Uganda wanasema rais
Joseph Kabila wa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo na rais Paul Kagame wa
Rwanda wamekutana nchini Uganda kujadili Mzozo huo unaoendelea Mashariki
mwa Congo .
Mkutano huo wa siku mbili umekuja baada ya waasi wa M23 kuuteka mji wa Goma Mashariki mwa nchi hiyo.
Waasi hao wanaoaminiwa kuungwa mkono na Rwanda ,
wanasema wako tayari kusonga mbele hadi mji mkuu Kinshasa kwa kile
walichokitaja kuwa ni kukomboa nchi hiyo kutoka kwa utawala wa sasa.
Baraza la usalama la Umoja wa mataifa limelaani kukamatwa kwa mji wa Goma
No comments:
Post a Comment