Dodoma.
Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo na Mbunge wa
Musoma Vijijini, Nimrod Mkono wameingia katika mvutano baada ya ujumbe
wa maandishi wa kutaka kukwamisha bajeti ya wizara hiyo kusambazwa kwa
wabunge.
Habari
za uhakika zilizopatikana jana zilieleza kuwa kiini cha mgogoro huo ni
ujumbe mfupi (SMS) ambao unamtuhumu Mkono kula njama za kutaka
kukwamisha bajeti ya Wizara ya Nishati na Madini.
Gazeti
hili limedokezwa kuwa, SMS hiyo inadaiwa kutumwa na Waziri Muhongo
kwenda kwa baadhi ya wabunge akimtuhumu Mkono kuwahonga baadhi ya
wabunge Sh3 milioni kila mmoja ili kukwamisha bajeti hiyo.
Ujumbe
huo unasomeka "Mhe Spika wa Bunge la Jamhuri, Sisi wabunge waadilifu
tunakiri kwamba Mhe Mkono ametufuata na kutupatia fedha kila mmoja
milioni 3 ili tukwamishe bajeti ya Nishati na Madini
Ujumbe huo umeanza pia kusambaa kwenye mitandao ya kijamii ikiwamo Jamii Forums .
Mkono
Mkono
ambaye pia ni Mwanasheria mashuhuri nchini, alipoulizwa jana kama ni
kweli amelalamika kwa Spika juu ya jambo hilo, alikiri na kusema
alichofanya ni kulalamika kwa Spika na amemwachia alishughulikie.
"Ni
kweli nimelalamika kwa Spika. Unajua taratibu za Bunge ni kuna any
complaint (lalamiko) unaliwasilisha officially (rasmi) kwa Spika... hilo
jambo lipo nimelifikisha kwa Spika wao ndiyo watafuatilia kwa taratibu
zao,"alisema.
Profesa Muhongo
Alipotafutwa
kwa njia ya simu ili alitolee ufafanuzi suala hilo, Waziri wa Nishati
na Madini, Profesa Sospeter Muhongo alituma ujumbe kwa simu ukisema:
"Tutavuka
tukiwa na ushindi wa maskini na wanyonge wa nchini mwetu. Tutaendelea
kujenga uchumi imara utakaotoa ajira mpya na matumaini mapya kwa vijana,
maskini na wanyonge wa nchini mwetu. Watanzania wamechoshwa na wizi,
udalali, ubabaishaji na rushwa."
Mkurugenzi
wa shughuli za Bunge, John Joel alipotafutwa jana alisema yeye hana
taarifa juu ya jambo hilo akisema kama lipo, basi huenda likawa mikononi
mwa Spika mwenyewe
Mvutano
huo unakuja siku chache baada ya Sakata la IPTL lililoibuliwa Bungeni
Ijumaa iliyopita na mbunge wa Kigoma Kusini, David Kafulila ambaye
alisema kuna ufisadi wa zaidi ya Sh200 bilioni katika akaunti ya Escrow
iliyopo chini ya Benki kuu ya Tanzania (BoT).
Akaunti
hiyo ilikuwa ni ya pamoja kati ya IPTL na Shirika la Umeme Tanzania
(Tanesco) kuhifadhi malipo ya kila mwezi kwa IPTL katika kipindi chote
cha mgogoro kati IPTL na Tanesco ambao uliishia mahakamani.
Tayari
Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania limemwagiza Mdhibiti na
Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) na Taasisi ya Kuzuia na
Kupambana na Rushwa (Takukuru) kuchunguza sakata hilo.
Alhamisi
wiki hii, Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Jaji Frederick Werema
aliliambia Bunge kuwa wapo watu wanaonunua mashahidi kuhusiana na sakata
hilo ingawa hata hivyo hakuwataja kwa majina.
Serikali yahaha kutafuta fedha
Wakati
mvutano huo ukiendelea, Serikali inahaha kutafuta fedha ili kuinusuru
bajeti ya Serikali na sasa kamati ya Bunge ya Bajeti chini ya Mwenyekiti
wake, Andrew Chenge imekuwa ikikutana na Hazina karibu kila siku.
Habari
zilizopatikana jana, zilidokeza kuwa bajeti inayoiumiza kichwa zaidi ni
ile ya Wizara ya Maji ambayo baadhi ya Wabunge wameapa kuikwamisha
endapo Serikali haitakuja na majibu ya kuridhisha.
Kwa
mujibu wa vyanzo mbalimbali, Wabunge wamepania kukwamisha bajeti hiyo
baada ya kugundulika kuwa wizara hiyo ilipatiwa asilimia 30 tu ya bajeti
yote ya maji iliyopitishwa na Bunge mwaka jana.
Bajeti
za wizara nyingine zinazoiumiza kichwa Serikali ni Wizara ya Ujenzi
ambayo inasemekana inadaiwa mabilioni na makandarasi na pia baadhi ya
miradi hasa ya barabara haijakamilika.
Habari
zinasema Serikali inaumiza kichwa kuongeza fedha za kutoka katika
Wizara hiyo ili imalize kutekeleza miradi ya barabara ikiwamo barabara
zilizoahidiwa na Rais Jakaya Kikwete wakati wa kampeni 2010.
"Unajua
uchaguzi mkuu ni mwakani... Serikali ina kibarua kigumu cha kutekeleza
miradi ya barabara na inahofu CCM itakuwa na wakati mgumu endapo kama
ahadi za Rais hazitatimia,"alidokeza mbunge mmoja.
"Kwa
hiyo wabunge wengi tunachachamaa kwa sababu tusipopata majibu katika
Bajeti hii tumeliwa takuwa na wakati mgumu majimboni na hili
hatutalikubali kabisa,"alisisitiza mbunge mmoja kutoka kanda ya Ziwa.
Kuhusu
Wizara ya Maji, wabunge wanadai pamoja na kupitisha bajeti ya ya ziada
ya Sh184 bilioni mwaka jana, lakini bajeti iliyokwenda kutekeleza miradi
ni kati ya asilimia 30 na 40 tu.
Mbunge
wa Ubungo, John Mnyika aliituhumu Serikali kuwa ililidanganya Bunge kwa
kushindwa kuongeza Sh184 bilioni zilizotakiwa kuongezwa katika bajeti
yake ya mwaka 2013/14.
Mnyika
aliongeza kusema "Kati ya Sh184 bilioni, Serikali imeongeza Sh86
bilioni tu...Maana yake ni kwamba Sh98 bilioni hazijatoka mpaka sasa
kwenda kwenye miradi ya jamii".
Mwenyekiti
wa kamati ya kudumu ya Serikali za Mitaa (Laac), Rajabu Mmbaruk, jana
aliliambia gazeti hili kuwa kwa jinsi bajeti za wizara zinavyopigwa
panga, ni dhahiri Serikali inapitia wakati mgumu.
Hata
hivyo, mbunge wa Muleba Kaskazini, Charles Mwijage, alisema
inavyoonekana Serikali imekuja na mapinduzi makubwa ya bajeti kiasi
kwamba haitaki tena kuwasilisha bajeti zisizotekelezeka.
"Wewe
unakumbuka mwaka jana bajeti ya maji ilikwama hadi Serikali ikaongeza
fedha, lakini hizo fedha zilienda zote? Na hili ndilo linaloleta shida
hata kwenye bajeti ya mwaka huu,"alisema Mwijage.
Mwijage
aliongeza kusema" huko nyuma Serikali ilikuwa inapitisha bajeti
kuwafurahisha wabunge ili wapitishe bajeti, lakini kwa kweli nyingine
hazitekelezeki na hilo limeleta mgogoro mkubwa kwa bajeti ya Maji".
Kutokana
na upepo huo mbaya, Serikali kupitia Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri
Mkuu (Sera,Uratibu na Bunge), William Lukuvi aliandika barua kwa Spika
akiomba bajeti ya wizara hiyo isogezwe mbele.
Katika
barua hiyo ambayo Lukuvi alilithibitishia gazeti hili kuiandika,
alipendekeza bajeti ya Wizara ya Maji na ile ya Nishati na Madini, zote
zisogezwe mbele hadi mwezi Juni badala ya kusoma mwezi huu.
"Kwa
kuwa Wizara hizi bado zipo katika mazungumzo na Wizara ya Fedha kuhusu
bajeti zao, ninaomba ukubali wizara hizi kubadilishiwa tarehe za
kuwasilisha ili ziwasilishe mwezi Juni,"inasema barua hiyo.
Barua
hiyo ya Lukuvi ya Mei 10,2014 yenye kumbukumbu 1/CEB.274/420/02
iliyotumwa kwa Spika, Anne Makinda, ilitumwa pia kwa Waziri mkuu, Waziri
wa Maji na Waziri wa Nishati na Madini.
Hata
hivyo, taarifa iliyopatikana jana, zinasema katika kujaribu kukokoa
jahazi, kamati ya bajeti, juzi ilikutana na walipa kodi wakubwa nchini
ikiwamo Kampuni ya Bia Tanzania (TBL) kubadilishana mawazo.
Taarifa
zisizo rasimi zinasema Serikali inakabiliwa na ukata mkubwa wa fedha na
hiyo inasababishwa na bajeti nyingi za wizara kupunguzwa, mfano ukiwa
wizara ya Mambo ya Ndani iliyopunguzwa kwa Sh500 bilioni.(E.L)
No comments:
Post a Comment