Mvumbuzi wa boti isiyotumia nahodha, Emmanuel Bukuku akitoa
ufafanuzi wakati wa Maonyesho ya 38 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam
(DITF) yanayofanyika katika Viwanja vya Mwalimu Julius Nyerere jijini Dar es
Salaam
Dar es Salaam. Mamlaka ya Mafunzo na Ufundi Stadi (Veta)
imevumbua boti inayojiendesha bila nahodha ambayo ina uwezo wa kutuma taarifa
za kijasusi na kujilinda dhidi ya mashambulizi au uharibifu unaoweza kufanywa
na watu wenye nia mbaya.
Akizungumza wakati wa Maonyesho ya 38 ya Biashara ya
Kimataifa ya Dar es Salaam (DITF) katika Viwanja vya Mwalimu Julius Nyerere
jijini hapa jana, Mvumbuzi wa mashine hiyo, Immanuel Bukuku alisema kuwa
imemchukua miezi sita kufanikisha uundaji wa mashine hiyo.
Alisema uvumbuzi huo umeambatana na majaribio ambayo
yamefanyika katika Pwani ya Kigamboni na yameonyesha mafanikio makubwa na ipo
tayari kwa ajili ya matumizi ikiwa na kamera za kutosha kwa ajili ya uchunguzi
na kupeleka taarifa.
“Uvumbuzi umekamilika na boti ipo tayari kwa ajili ya
matumizi na wadau wanakaribishwa kwa ajili ya kusaidia ufanikishaji wa
utengenezaji wa boti nyingine zaidi,” alisema na kuongeza kuwa boti hiyo
itakuwa inaongozwa na mashine nyingine itakayo kuwa sehemu maalumu.
Bukuku ambaye ni mwalimu wa masuala ya Sayansi na Teknolojia
katika Chuo cha Veta Chang’ombe alisema amevumbua boti hiyo ambayo
imetengenezwa kwa kutumia vifaa rafiki na mazingira ya bahari na inatumia mfumo
wa umeme jua na mashine za kuzalisha umeme.
“Ina uwezo wa kuhisi kuwapo kwa mtu au chombo kingine jirani
yake na kutoa taarifa katika sehemu ambako kinaratibiwa, pia ina uwezo wa
kushambulia kwa kutumia mitutu na ina uwezo mkubwa katika masuala ya ulinzi na
usalama,” alisema.
Alisema pia amefanikiwa kutengeneza injini ya ndege ambayo
imeonyesha mafanikio kwa kiasi kikubwa na wakati wowote inaweza kutumika na
mafanikio hayo yanachangiwa kwa kiasi kikubwa na mpango wa Veta wa kuwa na
Kitengo cha Masuala ya Ufundi na Ubunifu.
“Kuna mashine na teknolojia nyingi ambazo zimevumbuliwa
hapa, ni dalili njema na tuna matumaini kuwa uvumbuzi zaidi unafuata kutokana
na tafiti nyingi kuonyesha dalili za mafanikio,” alisema na kuongeza kuwa
kitengo hicho kimepania kubadili mwelekeo mzima wa Veta kwa hivi sasa.