Mwanasheria Mkuu wa Serikali, George Masaju
Mwanasheria
Mkuu wa Serikali (AG), George Masaju amesema madai ya wadau ya kutaka
Tume Huru ya Uchaguzi, mgombea binafsi na haki ya kupinga matokeo ya
uchaguzi wa urais mahakamani, yatafanyiwa kazi iwapo Katiba
Inayopendekezwa itapitishwa kwenye Kura ya Maoni Aprili 30.
Jambo
hilo ni mtihani mgumu kwa Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) ambao
umetangaza kususia kuipigia kura Katiba Inayopendekezwa huku ikitaka
mambo hayo matatu yafanyiwe kazi kabla ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka huu.
Katika
mazungumzo yake na wahariri na viongozi wa magazeti yanayochapishwa na
kampuni ya Mwananchi Communications Limited (MCL) ya Mwananchi,
Mwanaspoti na The Citizen jana, Masaju pia alitumia takribani saa mbili
kutoa ufafanuzi wa kina kuhusu suala la kuanzishwa kwa Mahakama ya
Kadhi.
Akizungumza
kwenye ofisi za makao makuu ya Mwananchi Communications Tabata Relini
jijini Dar es Salaam jana, Masaju alisema mambo hayo ni muhimu sana
katika kipindi hiki na hivyo ni muhimu kwa wananchi kupitisha Katiba
Inayopendekezwa ili masuala hayo yaandaliwe utaratibu wa kutumika kwenye
Uchaguzi Mkuu ujao.
Katika
mkutano wa pamoja na Rais uliofanyika mwishoni mwa mwaka jana, vyama vya
upinzani, vikiongozwa na Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), vilitoa
hoja ya kutaka mchakato wa Katiba Mpya uahirishwe hadi baada ya Uchaguzi
Mkuu wa Oktoba na kwamba katika kipindi hiki Katiba ya sasa ifanyiwe
marekebisho ili Tume ya Uchaguzi iwe huru, kuingiza mgombea binafsi na
haki ya kupinga mahakamani matokeo ya uchaguzi wa Rais.(P.T)
"Mambo
haya matatu yametambuliwa Katiba Inayopendekezwa na tunaweza kuyawekea
mfumo wa kisheria ili yatekelezwe kama Katiba Inayopendekezwa itakuwa
imepitishwa. Kama itapitishwa Aprili 30 na Uchaguzi Mkuu ni Oktoba,
halafu tukiiweka Katiba hii kabatini (tusiitumie), tutapata shida,"
alisema Masaju, ambaye aliisifu Katiba Inayopendekezwa kuwa ina mambo
mengi mazuri.
"Ushauri wangu kwa Serikali, kama Katiba imepigiwa kura na watu wakaipitisha, basi tuanze kutekeleza yale yanayowezekana."
Akizungumzia
kipindi cha mpito cha miaka minne ambacho kimewekwa kwa ajili ya kuanza
utekelezaji wa Katiba hiyo alisema si lazima Katiba Inayopendekezwa
ianze kutumika baada ya kipindi hicho.
"Huo ni
muda tu umewekwa na si lazima ufike. Kuna mambo ya msingi ya kuzingatia.
Mfano, Katiba hii imezungumzia masuala ya haki mbalimbali. Haki hizi
utekelezaji wake utategemea na bajeti iliyopo. Jambo hili linahitaji
muda kidogo. Kuna mambo ambayo hatuwezi kuyafanya kwa sasa, mfano ni
hili la haki ya wananchi kupata maji au kuwa na zahanati kwa kuwa
linahitaji bajeti kuliandaa," alisema.
Alisema
yale ambayo yanahitaji bajeti kidogo au kutohitaji kabisa, kama suala la
kuwapo kwa Tume Huru ya Uchaguzi, yanaweza kuanza kutekelezwa.
"Katiba
ikipita kuna mambo tunayoweza kuyafanya hasa yale yanayohusu uchaguzi.
Ni mambo ya msingi sana ambayo kama mkiyaacha watu watawashangaa,"
alisema.
"Kama
watu walitaka mgombea binafsi na leo unakwenda kufanya uchaguzi na
Katiba imepitishwa (inatambua mgombea binafsi), halafu huitumii, wengi
watakushangaa."
No comments:
Post a Comment